SENDEKA ATAKA NYUMBA ZA SERIKALI ZILIZOUZWA ZIREJESHWE MARA MOJA

MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), amesema kati ya uamuzi wa makosa uliowahi kuchukuliwa na Serikali ya chama chake cha CCM, ni kuuza nyumba za umma hivyo akataka zirejeshwe Serikalini mara moja vinginevyo atawasilisha hoja binafsi Bungeni.

Hii sio mara ya kwanza kwa wabunge kuhoji kuuzwa kwa nyumba za serikali wakitishia kutoa hoja binafsi bungeni kutaka mchakato huo ukome.

Aprili 5 mwaka 2008 aliyekuwa mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), alitishia kutoa hoja binafsi bungeni kutaka watu ambao si wafanyakazi wa serikali ambao wameuziwa nyumba za serikali wanyang'anywe nyumba hizo.

Na jana Ole Sendeka aliibua tena hoja hiyo alipokuwa akichangia hoja binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM), akitaka Serikali kutunga sheria ya kudhibiti wa shughuli za upangaji nyumba za makazi.

Sendeka alisema kutokuwapo kwa sera ya nyumba kumesababisha waliokuwa na madaraka kugawana nyumba za Serikali kama chakula cha njaa na kwamba, kama kuna sehemu Serikali ya chama chake ilifanya makosa ni uamuzi huo.

“Nataraji kuja na hoja ya kulitaka Bunge liamuru nyumba hizo zirudishwe… napingana na Waziri (John) Magufuli aliposema waliovunja mkataba wamenyang’anywa nyumba, siyo kweli,” alisema Sendeka na kuongeza:

“Nina ushahidi hata wale waliopata kwa sababu ya undugu wa waliokuwa na madaraka bado hawajarejesha.”

Awali, akiwasilisha hoja hiyo, Makamba alisema inatakiwa kutungwa sheria ya kudhibiti shughuli za upangaji nyumba za makazi kwa sababu, sheria iliyokuwa ikiwalinda ilifutwa mwaka 2005, ambayo ilikuwa inatoa ulinzi kwa wanyonge ambao ni wapangaji.

“Nchi nyingi za kibepari ikiwamo Kenya, zina Sheria za Kudhibiti Pango ambapo chini ya Sheria namba 296 ni makosa kudai pango la zaidi ya miezi miwili, na Uganda, chini ya Sheria yao namba 231,” alisema Makamba.

Makamba alisema katika mageuzi ya uchumi zimeundwa taasisi nyingi zinazdhibiti bei za bidhaa mbalimbali, huku akitoa mfano wa Sumatra, Ewura na TCRA.

Alisema kama inaonekana ni sahihi kuweka udhibiti kampuni za simu za mikononi zisipandishe bei holela, lazima kuwapo kwa udhibiti wa hitaji muhimu la maisha ya mwanadamu, ili mmiliki wa nyumba asipandishe kodi holela kwa kiwango cha wakati wowote.

“Vilevile, ni muhimu nikaweka wazi kwamba sheria ninayopendekeza siyo sheria ya kuwakandamiza wenye nyumba. Sheria itakayolinda maslahi ya wote; kwani ni dhahiri kabisa wapo wapangaji ambao nao hawatimizi wajibu wao,” alisema.

Mbunge huyo alisema sheria ya hivi sasa mmiliki wa nyumba hana haja ya kwenda mahakamani kupata haki yake ya kimkataba, anaweza kuuza kitu chochote cha mpangaji, lakini mpangaji ili apate haki yake lazima aende mahakamani ambako kuna mlolongo mrefu.

Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema Serikali haijatambua kuwa sekta ya makazi ni chanzo kikubwa cha mapato na kutoa mfano wa Dubai inayopata zaidi ya asilimia 20 ya mapato yake kutoka sekta ya makazi, huku mafuta yakichangia asilimia sita.

“Kuna mapato makubwa kwenye hii sekta, lakini hakuna kinachokusanywa ndiyo maana hakuna sera ya nyumba miaka 50 tangu tupate uhuru,” alisema Mbowe.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema hoja hiyo ni muhimu na kwamba, kabla ya kutengeneza sheria inahitajika kuundwa sera ya nyumba ambayo hadi sasa haipo.

Profesa Tibaijuka alikiri tabia iliyoanzishwa na wamiliki wa nyumba kutaka kulipwa kodi ya pango kwa miezi sita au mwaka mmoja, ni kinyume na viwango vya kimataifa kuhusu makazi na kuomba Serikali ipewe muda kuifanyia kazi hoja hiyo.

Historia ya nyumba za serikali

Nyumba za watumishi wa serikali zilianza kujengwa na watawala wa Kijerumani na Waingereza. nyumba hizo ambazo sasa idadi yake inakadiriwa kufikia 10,000 ziko za daraja la tatu, pili na kwanza kulingana na nyadhifa za watumishi wa serikali.

Nyumba hizo zimejengwa maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo katika jiji la Dar es Salaam ambako nyumba mashuhuri ni zile zilizoko maeneo ya Upanga na Oysterbay.

Lengo kubwa la nyumba hizo ni kurahisisha usafiri kwa wafanyakaziwa serikali na kuwaondolea kero ya makazi, gharama za kuwalipia kodi za kupanga na kuwavutia wafanyakazi ili wafikie ufanisi kiutendaji.

Wazo la kuziuza nyumba hizo lilianza katika utawala wa serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ambaye baada ya mwenyewe kuchukulia nyumba iliyoko Sea View jijini Dar es Salaam, zingine zikaanza kuuzwa kwa mawaziri, majaji, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa jeshi, polisi na magereza.

Sababu za kuuza
nyumba hizo

Sababu za kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana. Wakati maelezo mengine yanasema kuwa hatua hiyo imefikiwa kuwasaidia watumishi wa serikali kuwa na nyumba, mengine yanasema nyumba hizo ziliuzwa kwa kuwa ni mzigo kwa serikali. (Chanzo;Gazeti la Mwananchi

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI