WATUHUMIWA WA SAMAKI WA MAGUFULI WAHUKUMIWA MIAKA 20

Watuhumiwa wa kesi ya kuvua samaki kinyume cha sheria eneo la Tanzania katika Bahari ya Hindi kwa kutumia meli ya uvuvi,Nahodha Hsui Chin Tai (kushoto) na Wakala, Zhao Hinguin wakiwa ndani ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Biashara),Dar es Salaam LEO, ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 20 na 10 au kulipa faini ya sh.bilioni 1 na bilioni 20.(PICHA NA DOTTO MWAIBALE)

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh20bilioni, washtakiwa wawili wa kesi ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania (EEZ) na kutaifisha meli waliyokamatwa nayo ya Tawaliq1 kwa manufaa ya umma.

Jaji Agustine Mwarija alitoa hukumu hiyo jana na kuwatia hatiani washitakiwa hao ambao ni nahodha wa meli hiyo Husu Chin Tai na wakala wa meli hiyo Zhao Hanquing lakini, akiwachia huru washitakiwa wengine watatu.

Nahodha Tai ambaye ni mshitakiwa wa kwanza alihukumiwa adhabu mbili kwa pamoja ambazo ni kwenda jela miaka hiyo 20 au kulipa faini ya Sh 1bilioni na kosa la pili, kutumikia kifungo cha miaka 10 au kulipa faini ya Sh 20bilioni.

Adhabu kama hiyo pia ilitolewa kwa mshtakiwa wa saba, Zhao Hanquing na adhabu zote zinakwenda pamoja.

Mashitaka
Washtakiwa wote watano walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili
kwa pamoja, la kwanza likiwa ni kufanya shughuli za uvuvi katika ukanda huo wa Tanzania bila kibali na kuchafua mazingira ya bahari kwa kumwaga mafuta na uchafu wa samaki majini.

Lakini, mshtakiwa wa saba Hanquing na mshtakiwa wa tisa Sheng Pao wao walikuwa wakikabiliwa na kosa jingine la kujaribu kuwaepusha wenzao na adhabu kutokana na makosa waliyokuwa wakituhumiwa .

Walioachiwa huru katika kesi hiyo ni wahandisi wawili wa meli hiyo, Cai Dong Li ambaye alikuwa mshitakiwa wa 33, Cheng Rui Hai wa 34; na mshitakiwa wa tisa, Hsu Sheng Pao kutokana na kile Jaji Mwarija alichosema ni ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma zao.

Kuhusu washtakiwa wa 33 na 34, Jaji Mwarija alisema watuhumiwa hao walikuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa meli tu kwani
wakiwa wahandisi hawakuwa na nafasi ya kujua masuala ya leseni wala mahali walipokuwa wakivua na kwamba majukumu hayo ni ya Nahodha na wakala.

Kuhusu mahali walikokuwa wakivua kama ni Ukanda wa Kiuchumi wa Tanzania au la, Jaji Mwarija alisema hilo ni jukumu la nahodha, huku akizingatia utetezi wa washtakiwa hao kuwa hawajui hata kusoma ramani.

Akimzungumzia mshtakiwa wa tisa, Pao, Jaji Mwarija alisema hana hatia kwani hakuwamo melini.

Jaji Mwarija alisema mbali na kitendo chake cha kuambatana na mshtakiwa wa saba (Hanquing), hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa mahakamani hapo unaothibitisha makosa aliyofanya.

Jaji Mwarija alisema ameridhika na ushahidi wa mazingira uliotolewa na upande wa mashtaka akiwemo shahidi wa tatu, Nahodha Ernest Bupamba ambaye ni Msimamizi wa Shughuli za Uvuvi na Sheria za Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, ambaye pia ndiye aliyewakamata washtakiwa hao, akiwa na wanadoria wenzake wa mataifa mengine matano ya Afrika.

Jaji Mwarija aliuelezea ushahidi huo wa mazingira kuwa ni pamoja na kukutwa na samaki, ambao walikuwa hawajaganda kwenye friji na kufungwa kwa madirisha madogo ya kutolea maji kwenye meli (Scuppers).

Bupamba katika ushahidi wake, aliieleza mahakama kuwa ‘scupper’ hizo huwa zinafungwa wakati wa shughuli ya uchakataji samaki na kwamba kwa mazingira hayo ilionesha kuwa shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea hata muda mfupi kabla ya kuwakamata.

Pia Jaji Mwarija alielezea kuridhika na ushahidi wa alama zilizooneshwa katika rada ya meli hiyo, ambazo zilionesha eneo walilokamatiwa baharini lilikuwa ni la Tanzania.

“Pia maelezo ya onyo ya washtakiwa wa 17 na wa 19 walikiri kuwa walipokamatwa walikuwa wakiendesha shughuli za uvuvi katika eneo la Tanzania,” alisema Jaji Mwarija na kuongeza;

“Kwa kuzingatia ushahidi huo, kosa la kuendesha shughuli za uvuvi katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania limethibitishwa,”alisema
Jaji Mwarija.

Maelezo mengine
Jaji huyo pia alisema anakubaliana na maoni ya Wazee Washauri wa Mahakama , Bernard Ntumba na Margreth Mosi kuwa washtakiwa wa kwanza na wa tisa wana hatia na wengine hawana hatia.

Kuhusu kutokuwa na leseni, Jaji Mwarija alisema ni jambo ambalo halikupingwa kuwa meli haikuwa nayo na kwamba mshatakiwa wa kwanza, (nahodha) alikubali na kisha akatoa nakala ya leseni ambayo ilikuwa imeisha muda wake.

Alisema kitendo cha mshtakiwa wa saba (wakala) kuja Dar es Salaam na kutoa nakala ya leseni kwa ofisa wa Polisi ambayo pia ilikuwa imekwisha muda wake, ni dhahiri kuwa naye alikuwa anawajibika kwa suala hilo.

“Hivyo, mshtakiwa wa kwanza na wa saba kwa pamoja wanatiwa hatiani kwa kosa hilo la kwanza,” alisema Jaji Mwarija.

Kuhusu kosa la pili la kuchafua mazingira ya bahari, Jaji Mwarija alisema kimantiki kushindwa kuleta uchafu yaani matumbo, mapezi na vichwa vya samaki mbali ya kilo tatu tu za utumbo ni dhahiri kuwa ulikuwa ukitupwa baharini.

Jaji Mwarija alisema jambo hilo halihitaji ushahidi wa kisayansi katika kulithibitisha, kama ambavyo upande wa utetezi ulivyodai wakati ukiwasilisha hoja zao za mwisho.

Kuhusu kosa la tatu la kusaidia kuwaepusha washtakiwa wengine na hatia lililokuwa likiwakabili mshtakiwa wa saba na wa tisa, Jaji Mwarija alisema kwa kuwa mshtakiwa wa saba ametiwani hatiani kwa kosa la kwanza hivyo, kosa la tatu hana hatia.

“Hivyo, mshtakiwa wa kwanza na wa saba wana hatia katika kosa la kwanza,” alisema Jaji Mwarija na kunyamaza kuwapa nafasi mawakili wa pande zote kusema lolote kabla ya kutamka adhabu.

Maelezo na hukumu
Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Muganga licha ya kukiri kuwa hawana kumbukumbu za washtakiwa hao waliotiwa hatiani kutenda makosa kama hayo, lakini aliiomba mahakama iwape adhabu kali.

Pia alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mambo ya Uvuvi na kwa mujibu wa kifungu cha 351 cha Kanuni za Adhabu, aliiomba mahakama iamuru meli hiyo iliyotumika kutenda makosa hayo itaifishwe baada ya washtakiwa kutiwa hatiani.

Hata hivyo, Kiongozi wa mawakili wa washtakiwa, nahodha Ibrahim Bendera aliyekuwa akisaidiana na John Mapinduzi aliiomba mahakama iwaonee huruma katika kutoa adhabu akidai kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kutenda kosa hilo kama alivyokiri wakili wa serikali.

Alidai washtakiwa hao wamekaa rumande kwa takribani miaka mitatu wakati kesi yao ikiendelea, hivyo kuiomba mahakama katika kutoa adhabu izingatie muda huo waliokaa rumande.

Alidai kuwa aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza (Nahodha) mwaka huu anatimiza miaka 63 na kwamba, miaka mitatu wameitumia rumande na kwa kuwa wana familia huko kwao.

Hata hivyo, aliishauri mahakama meli hiyo ifanyiwe tathmini ili ikiwezekama mwenye meli alipe fidia na kuchukua meli yake ili kuiondolea serikali mzigo wa kuikarabati.

Akitoa adhabu, Jaji Mwarija alisema amezingatia hoja za pande zote lakini akasema adhabu za makosa hayo zimeainishwa katika sheria ikiwa ni pamoja na kiwango cha chini ambacho mahakama haiwezi kukivuka.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Deep Sea, mahakama inaweza kutaifisha chombo kilichotumika kwenye uhalifu, hivyo meli hii ambayo ilikamatwa na kutolewa hapa kama kielelezo inataifishwa” alisema Jaji Mwarija.

Alisema uamuzi huo umezingatia mazingira kwamba ilifanya kazi kwa kutumia majina mengi tofauti na ilikuwa haitambuliki katika mamlaka inayosimamia Uvuvi wa Samaki aina ya Jodari katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

“Mwenendo huo huonesha kuwa walifanya makosa hayo kwa mpango. Hivyo ili kuzuia uhalifu huu usiendelee kutokea mahakama imeamuru itaifishwe,” alisema Jaji Mwarija na kuongeza;

Kuhusu amri juu ya samaki waliopatikana kwenye meli, kwa sababu waligawiwa katika taasisi mbalimbali za kijamii, hakuna amri hoyote juu ya samaki hao, washtakiwa wana haki ya kukata rufaa.

Washtakiwa hao na wenzao walikamatwa Machi 8, 2009 wakiwa samaki tani 293 aina ya Jodari.

Awali, kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 37 wenye uraia wan chi tofauti wan chi za Bara la Asia na wawili walikuwa raia wa Kenya.

Julai 14, 2011 wengine waliachiwa huru baada ya kuoneakana kuwa hawana kesi ya kujibu isipokuwa washtakiwa watano ambao walihukumiwa jana na wawili kutiwa hatinai.

Hadi wakati hukumu yao inapotolewa washtakiwa hao wamesota rumande kwa miaka miwili, miezi 11 na siku 15.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU