Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Kiwenge akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambay alifungua mkutano wa wadau wa mfuko huo wa Bima ya Afya mjini Kibaha leo |
Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo, Grace Michael akiratibu mkutano wa wadau wa NHIF Mkoa wa Pwani leo, mjini Kibaha.
Baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza na viongozi wa NHIF
Wanahabari wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa NHIF pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mahiza
Mahiza akizungumza na wanahabari baada ya kufungua mkutano huo
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NHIF, Eugen Mkongoti akielezea jinsi wadau wa mfuko huo na hasa wanachama wanavyonufaika na mfuko huo na ule wa Mfuko wa Afya ya Jamii.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa NHIF, Beatus akiwahamasisha wadau kujiunga na mfuko huo ili wanufaike nao
Mahiza akiagana na Mkurugenzi wa NHIF, Humba. Kushoto ni Grace Michael ambaye ni Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo
*Aonya kutumia muda kupiga soga badala ya huduma
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza ameonesha kukerwa na tabia ya baadhi
ya watoa huduma za afya kwa kushindwa kutoa huduma bora kwa wanachama wa Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya na wananchi kwa ujumla huku wakitumia muda wao mwingi
kupiga soga ama kunywa chai maofisini.
Amesema kuwa haki inakwenda na wajibu hivyo watoa huduma wanatakiwa
kutanguliza upendo kwa wananchi kwani wana haki ya kupata huduma kwa wakati
wanapokwenda hospitali ama kwenye vituo vya afya.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
Mkoa wa Pwani,Mahiza alisema kuna baadhi ya watoa huduma katika sekta ya afya
wanangalia zaidi maslahi yao kuliko kuangalia majukumu yao hali inayokwamisha
wananchi kuona umuhimu wa kujiunga na utaratibu wa bima za afya.
Alisema imefika mahali watoa huduma wanajifungia ofisini kupiga soga ama
kunywa chai wakati wagonjwa wanateseka kwa kupanga foleni kusubiri huduma kitu
ambacho amesema hayuko tayari kukivumilia.
"Kuna baadhi ya watoa huduma wao hawaoni umuhimu wa kuhudumia wagonjwa.
Wagonjwa wamepanga foleni nje wao wanajifungua ofisini wanakunywa chai.
"Hapana jamani naomba tubadilike, wapo baadhi ya watendaji katika sekta ya
afya wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa
wakati.Hivyo wale ambao wanaona wao ni miongoni mwa wale wasiopenda kutoa huduma
wabadilike au waache kazi kuliko kuendendelea kudharirisha wegonjwa,"alisema
Mahiza.
Hata hivyo aliwaambia watendaji na watoa huduma wote wa Mkoa wa Pwani
kutambua kuwa pamoja na kuwepo changamoto nyingi katika sekta ya afya bado
wanatakiwa kutimiza majukumu yao ili hata wanapodai haki iwe ina maana
zaidi.
Alisema kuwa kila kazi inachangamoto zake lakini bado kwa anayeifanya anayo
nafasi ya kutambua kuwa kama anaona haimfai anaweza kutafuta kazi nyingine ya
kufanya.
Aliongeza kuwa inawezekana baadhi yao wakaona anatumia lugha kali na
kumtaka kuomba radhi kitu ambacho hatakifanya kwa kuwa ameamua kutoa dukuduku
lake kwa kutaka mambo yaende sawa huku akiongeza kuwa Tanzania inajengwa na
wananchi wote.
Alisema kuwa kuna baadhi ya watendaji utawasikia wakidai haki lakini
ukiangalia majukumu yao hakuna kitu ambacho wanakifanya au kulingana na madai
yao.
Akifafanua zaidi kuhusu sekta ya afya alisema kuwa kuna baadhi ya hospitali
na vituo vya afya watoa huduma wake wanatoa huduma za matibabu kwa kumuangalia
mtu alivyovaa jambo alilolikemea na kutaka lisionekane mkoani mwake.
"Kuna siku nilienda moja ya hospitali, nilipofika pale nikakuta kuna
mgonjwa amekosa huduma kwa zaidi ya saa 12 tena amepata ajali.Kitanda alicholala
hata shuka hajapewa.Lakini akaja mtu kwasababu tu fulani akafika na kupewa
huduma.
"Kitendo cha kutoa huduma kwa kuangalia mgonjwa kavaa nini ama amepaka lip
stick ya aina gani mdomo hii si sawa.Sote ni Watanzania tunahitaji kupata huduma
iliyosawa. Kutoa huduma ya afya kwa kuangaliana usoni inawakatisha tamaa
wananchi. Tubabadikike,"aliongeza.
Pia alisema katika kuhakikisha Mkoa wa Pwani unapiga hatua katika kutoa
huduma za afya atahakikisha anafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya
afya na hospitali kwa kuenda bila kutumia gari ya Serikali.
Alisema amekuwa na kawaida ya kufanya ziara katika baadhi ya maeneo ya
kiutendaji ili kuona mambo yanavyofanyika na ambayo amekuwa akiyakuta huko
mengine hayaridhishi.
Pia alisema kuwa tatizo lingine ambalo limekuwa kero kwa wananchi ni
kukosekana kwa dawa hata panaldo changamoto inayosababisha kikwazo kwa mfuko
huo.
Alisema kuna tatizo upande wa MSD ambao ndiyo wanahusika na utoaji wa dawa
na hata halmashauri inapopeleka orodha ya dawa na fedha bado wanashindwa kupewa
kwa wakati hali ambayo inakatisha tamaa.
Alisema umefika wakati kwa MSD
kutimiza majukumu yao na kuhakikisha halmashauri zinapotoa ombi la kupatiwa dawa
wanapewa kwa wakati badala ya kushindwa kuwapatia ama kuwapa tofauti na mahitaji
yao.
"Umefika wakati kwa watendaji na watumishi wa umma kutambua majukumu
yao.Ili pale ambao wanasimama kudaia maslahi yao lakini pia wawe wametimiza
majukumu yao ikiwa pamoja na kuhudumia wananchi wao.
Maendeleo yetu yatatokana na sisi wenyewe.Tanzania ndiyo nchi yetu hakuna
nyingine.Unaweza kukuta nchi imeanza na T lakini haitakuwa Tanzania,"alisema
Mahiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, alisema
kuwa ili kuboresha huduma kwa wanachama wake, Mfuko unaandaa utaratibu wa
kuwatumia madaktari bingwa ili wakatoe huduma kwa wanachama hasa walioko katika
mikoa ya pembezoni.
Alisema Mfuko uko tayari kuhakikisha unabaoresha sekta ya afya kupitia
fursa inazozitoa ikiwemo ya Mikopo ya Vifaa tiba na ukarabati wa majengo fursa
inayolenga moja kwa moja kuwasaidia wananchi wote katika sekta ya afya.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea na mikutano yake katika mikoa
mbalimbali ambapo kesho utakuwa na mkutano Mkoani Morogoro lengo ni kutoa elimu
kwa umma ili kupanua wigo wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF).
Comments