KASEJA:MABAO YA AL-SHANDY YALITUVUGA

NAHODHA Juma Kaseja amekiri wachezaji wote Simba walivurugikiwa kisaikolojia baada ya Al Ahly Shandy kufunga mabao matatu ndani ya dakika 15 za kipindi cha pili.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Kaseja alisema kila mchezaji alipotea uwanjani hapo.

"Tulipoteana uwanjani, hakuna kati yetu aliamini wangeweza kusawazisha yale mabao, kipindi cha kwanza tulicheza vizuri sana, ila, ndani ya dakika tano, kipindi cha pili, walitufunga magoli mawili na la tatu, hatukuamini," alisema Kaseja.

"Nawajua vizuri wachezaji wa Simba, baada ya kufungwa magoli matatu, niliwaangalia usoni na kuona wamebadilika wote," alisema.

Kilipofika kipindi cha kupiga penati, wachezaji wenzake waliogopa kupiga kwa kuogopa lawama na wengi walikuwa wamepoteza morali kabisa."

"Nikiwa kama nahodha, niliwalazimisha kupiga, kocha ananiuliza Kaseja nani anapiga, nikimtaja mtu, anaogopa, ikabidi nitumie nguvu, sababu ilibidi tupige," alisisitiza Kaseja.

"Waliweza kushinda kwa sababu penati haina mwenyewe, siku zote hata kwa timu kubwa kama Real Madrid au Barcelona wanakosa."

"Tulicheza vizuri ila makosa madogo yalikuwa chanzo, ila kwa sasa tusilaumiane, tuangalie tulipo jikwaa kwa ajili ya michuano ijayo."
Kipa huyo wa kimataifa wa Tanzania, pia alizungumzia hali ya uchovu kwa wachezaji wenzake itakuwa imechangia kwa kiasi furani.

"Kwa muda mfupi tumecheza mechi nyingi na wachezaji ni wale wale tu, kama mabadiliko ni kidogo sana."

"Na kwa hili, kocha asilaumiwe kwa kuchezesha wachezaji wale wale kwa sababu anajaribu kutengeneza timu ya pamoja, iliyokaa kwa muda mrefu na kuelewana kama vile ilivyo kwa Manchester United na timu nyingine kubwa duniani," alisema Kaseja.

Nahodha huyo wa Simba ameuomba uongozi wa klabu hiyo kutotumia kigezo cha kufungwa na kutolewa na timu ya A-Shandy kuivuruga timu katika msimu wa usajili ujao.

"Ni kweli, kwa mtazamo wangu, tunahitaji kusajili wachezaji mahiri, kutokana na mapungufu tuliyoyaona, ila tusitumie kigezo cha kutolewa katika michuano hii kuvuruga timu.

"Ili timu ielewane, inahitaji kukaa pamoja, viongozi waangalie maeneo ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu na kusajili wachezaji wazuri kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayokuja mbele yetu," alisema.

"Majina hayachezi uwanjani, tuangalie uwezo wa wachezaji katika kuisaidia timu ishinde na kufanya vizuri."

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI