Machafuko Z’bar, tatizo ni Muungano au udini?

                         Na Josephat Isango
HAIINGII akilini mtu analalamika anataja Muungano, lakini anakimbilia kanisani. Ninavyojua, hata kifalsafa kila mtu atanielewa, kanisa si kiungo cha Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika. Kanisa halikusaidia kwa namna yeyote kusainiwa Muungano. Kanisa lilikuwepo hata kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania.

Kanisa lipo sehemu nyingi duniani, lipo Kenya, Somalia, na hata Saudi Arabia alipozaliwa Mtume Mohamed SAW. Katika nchi nyingi mfano, Oman, Nigeria na Sudan kuna Wakristo wengi na haya mambo hatujawahi kuyasikia, sasa kwa nini iwe Tanzania? Kila mtu ana wajibu wa kuabudu waachwe nao waabudu ili mradi hawavunji sheria. Sasa tatizo la uwepo wa Makanisa visiwani Zanzibar linahusikaje na Muungano wa Tannganyika na Zanzibar?

Mtu hataki Muungano anavunja kanisa, anachoma gari au mali zingine za kanisa ama anaharibu shule za kanisa ambazo hazifundishi wakristo pekee. 

Mtu hataki Muungano anaharibu Kituo cha afya cha kanisa ambacho kinatoa huduma ya matibabu kwa watu wote. Hapa hoja ya Muungano inatokea wapi? Tuache uongo waliohusika na uharibifu wa makanisa, au mali za kanisa waulizwe vizuri kuna kitu zaidi ya Muungano walichokuwa wanakusudia. Kwanini kama hoja ni Muungano mbona hakuna hata jengo moja la wizara lililobomolewa wala kutupiwa jiwe? Wanaoshughulikia Muungano ni mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbona hakuna gari yao wala mali yao iliyochomwa moto? 

Mbona waandamanaji hawakujipanga kuziba barabara zinazoelekea Ikulu ya Zanzibar kama hoja ilikuwa ni Muungano? Kwanini wakimbilie makanisa?
Viongozi wa makanisa wanalalamika, wanaiambia serikali kuwa “Tumekutana na tunatoa tamko baada ya muda mrefu wa kimya na uvumilivu tuliosafiri nao kwa takribani miaka 11, kwa kumbukumbu zetu tangu mwaka 2001.

Tunajua na tunauambia umma wa wapenda amani kuwa matukio ya Mei 26 hadi 28 ni matokeo ya mahubiri na mihadhara iliyokuwa ikiendeshwa kwa makusudi kuutukana na kuukashifu Ukristo hapa visiwani Zanzibar na hivi kupandikiza hofumiongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo.

Tunashawishika kusema kuwa ufadhili na ushawishi wa vurugu na vitisho hivi vina udhamini wa ndani au nje ya nchi yetu”. Serikali ipo tayari kudhalilishwa kuonekana kuwa imeongozwa kwa udini kwa miaka 11, kama maaskofu wanavyosema?, Serikali ipo tayari kukubali kuwa matokeo ya mihadhara na mahubiri iliyoendeshwa mchana kwa vibali vya polisi ndiyo iliyosababisha hali hiyo?

Je, ina maana polisi hakuona hayo au dalili zake mpaka machafuko yalipotokea?
Kama anavyosema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamedi Shein kuwa mambo hayo waliyatazamia ila hawakuyatarajia. Je, 
walichukua hatua gani za tahadhari? Au walisubiri kuona maafa ndipo waje kusema tunajifunza kutokana na makosa? 

Ni aibu gani hii kwa serikali yenye polisi, usalama wa Taifa na makachero wa Intelijensia ambao huona maandamano ya wapinzani tu?
Serikali inakubali vipi aibu hii ya kuhusishwa na udini? 

Kama haikubali ipo tayari kukanusha tamko la viongozi hawa wa dini kwa kuonesha kuwa ilichukua hatua na kuwafikisha mahakamani watu mbalimbali waliohusika na machafuko hayo!
Pengine matukio yaliyopata kutokea visiwani Zanzibar ambapo kila mara yanapotokea matatizo ama vurugu za kiitikadi ya vyama au vinginevyo hutajwa Ubara na Uzanzibari, vitu ambavyo kwenye dini havipatikani bali kwenye mambo ya kisiasa.

Tunaomba ufuatiliji makini utendeke, ili kujua nini hasa tatizo, ni Muungano, au siasa za kijinga au udini? Na kama ni siasa kwanini zitumike kwa kusaidiwa na wafuasi wa dini? Serikali iwe makini, kuacha kuendelea kwa mambo hayo. Tuseme ukweli daima ili taifa letu linufaike na liendelee kudumu.Chanzo;Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MIKOA 10 YENYE KIPATO KIKUBWA ZAIDI KWA MTU MMOJA MMOJA

BODABODA ALIPWA PIKIPIKI BAADA KUSAFIRI KWA BODA KWA SAA 10 MBEYA HADI DAR

ASANTE GWIJI YAYA TOURE KWA KUPASUA UKWELI UKWELI KUPENDELEWA KWA MOROCCO

AINA 4 ZA WANAWAKE WASIOWEZA KUDUMISHA NDOA.

CONFIRMED HAWA NDIO WACHEZAJI WETU 12 WA KIGENI 🦾