MADIWANI WAMKATAA DC SHINYANGA

Suzy Butondo Shinyanga.
MADIWANI wa Manispaa ya Shinyanga wamemkataa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga AnnaRose Nyambi kutokana na kitendo chake cha kushinikiza wakulima wa kijiji cha Mwamashele katika Manispaa hiyo wanyang’anywe mashamba yao na Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha 516KJ Kizumbi yaliyopo kijijini hapo.

Madiwani hao walichukua huo uamuzi katika kikao cha baraza la madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Shinyanga.

Madiwani hao walidai kukerwa na kitendo hicho na pia kukasirishwa na baadhi ya Askari wa Jeshi hilo ambao walikwenda kijijini hapo wakiwa na bunduki na kuwalazimisha wamiliki wa mashamba hayo kuruka kichura bila kosa lolote.

“Nasema sina imani na Mkuu wa Wilaya, huyu anafaa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kambi ya Jeshi ya Kizumbi na siyo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga yetu hii, hatufai kabisa kwa sababu hakuna anachotusaidia, badala ya kusaidia wananchi anawakandamiza ” alisema Sebastian Peter diwani wa kata ya Ngokolo.

Madiwani hao walidai kushangazwa na uamuzi wa Mkuu wa Wilaya hiyo kukubaliana na uongozi wa kikosi cha 516KJ kupora eneo lenye ukubwa wa hekta za mraba 850 mali ya wananchi wa kijiji cha Mwamashele ambalo linajengwa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wenye thamani ya shilingi Milioni 275.

Aidha walisema kikosi cha 516KJ Kizumbi kiliomba kupewa eneo lililoko katika Vijiji vya Mwamashele na Nhelegani kwa kufuata taratibu zote mwaka 1979 ambapo wananchi walikubali kutoa eneo hilo na lilipimwa na wataalamu wa Ardhi na kuliwekea mawe ya mipaka kati ya (JWTZ) na wananchi wa vijiji hivyo.

Walisema walishangazwa na kitendo cha askari hao mwaka usiofahamika walikwenda kung’oa mawe yaliyowekwa na wataalamu wa ardhi kutenganisha eneo la kambi ya Jeshi na vijiji na kujiongezea eneo bila ya kuwashirikisha wakazi wa Mwamashele, wataalamu wa Ardhi, au viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Walieleza pamoja na askari wa (JWTZ) kujiongezea eneo kiholela bila ya kufuata utaratibu pia walimpa kazi ya kuchora ramani ya eneo hilo askari wa Jeshi hilo aliyetambuliwa kwa jina la Ignus Valalia na kupitishwa na Wizara ya Ardhi Juni 13, mwaka 2005 huku wananchi wa kijiji cha Mwamashele wakiwa hawajui kuwa eneo lao lilikwisha porwa na askari wa kikosi cha 516KJ cha Kizumbi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamashele Daniel Sweya alikiri kuporwa kwa mashamba yao bila ya wao kujua na kuongeza kuwa eneo ambalo walilitoa kwa askari wa jeshi hilo walioko katika kikosi cha 516KJ wanalifahamu na hawana madai nalo kwa sababu hata wananchi waliokuwa ndani ya eneo hilo walikwisha lipwa fidia na Jeshi.

“Sisi tulishalipwa fidia ya maeneo yetu kisha tukahamia katika maeneo yaliyobakia, lakini tumesikitishwa sana na kitendo cha Askari wa Jeshi la Wananchi leo kuanza kudai kuwa hili ni eneo lao wakati miaka mingi tuko hapa na tumeshajenga nyumba zetu na tunaishi , inamaana waliomba kutoka kwa nani eneo hili au wanatuonea tu “ alisema Sweya. Chanzo; Mwananchi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI