Rais Kikwete aelekeza viongozi kushughulia njaa Kilimanjaro


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


Coat of Arms
PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais  Kikwete aelekeza viongozi kushughulia njaa Kilimanjaro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Wilaya ya Same kufanya tathmini kamili na ya haraka kujua kiwango cha njaa katika wilaya hiyo ili kuiwezesha Serikali kutoa chakula cha msaada ama cha bei nafuu kwa wananchi.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaipatia jawabu la kudumu changamoto ya maji katika maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Wilayani Same.
Rais Kikwete alitoa agizo la kushughulikia tatizo la njaa jioni ya jana, Jumatatu, Oktoba 29, 2012, wakati alipoelezwa na wananchi katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Same aliposimama mara kwa mara kusalimia wananchi kwenye siku ya pili ya ziara yake ya siku nne Mkoani Kilimanajaro.
Wananchi katika maeneo ya Hedaru na Lembeni walimwambia Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa wanakabiliwa na njaa kwa sababu ya ukame ambao umesababisha wasipate chakula cha kutosha kwa miaka mitatu iliyopita.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo hasa kuhusu njaa na ukosefu mkubwa wa maji, Rais Kikwete alisema: “Nimesikia maelezo yenu kuhusu ukosefu wa chakula na njaa. Mkuu wa Mkoa yupo hapa pamoja na Mkuu wa Wilaya na napenda kuwaagiza wafanye tathmini ya haraka kuhusu kiwango cha tatizo ili Serikali ichukue hatua ya kumaliza tatizo hili.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais: “Hakuna wasiwasi. Hakuna mtu ambaye atapoteza maisha yake kwa sababu ya njaa. Tunacho chakula cha kutosha na Serikali itahakikisha chakula kinapatikana mara tu tathmini itakapokamilika.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Chakula  kitakuwa cha  aina mbili. Kwa familia zisizokuwa na uwezo kabisa chakula kitatolewa bure. Kwa wale wanaojiweza, chakula kitatolewa kwa wananchi kuchangia fedha kidogo sana kama Sh. 50 tu.”
Rais Kikwete alisimamishwa mara tisa na wananchi ambao walikuwa na hamu ya kumwona na kusalimiana naye akiwa njiani kutoka  Mamba Miamba ambako alizindua Kiwanda cha Kusindika Tangawizi kwenda Mwanga ambako alifungua Hosteli ya Shule ya Wasichana ya Asha Rose  Migiro mjini Mwanga.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
30 Oktoba, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI