Mbunge wa Jimbo la Ubungo(CHADEMA)na Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini,Mh John Mnyika
--
Katika
kipindi cha ziadi ya wiki tatu nchi imekuwa katika matatizo makubwa ya upungufu
wa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli hali yenye athari kwa uchumi wa nchi na
usumbufu na gharama za ziada kwa wananchi.
Katika
kipindi hicho viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwemo
Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na taasisi zilizochini ya Wizara hiyo hususan
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) wamekuwa wakitoa taarifa zenye
mkanganyiko kuhusu matatizo yanayoendelea.
Hivyo,
nasisitiza Waziri Mkuu kwa madaraka yake ya ibara ya 51 ya katiba ya udhibiti,
usimamiaji na utekelezaji wa shughuli za siku hata siku wa kazi za Serikali na
kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni badala ya kutoa tu kauli bungeni
aagize Waziri wa Nishati na Madini awasilishe hoja ya taarifa ya Serikali juu
ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu mafuta na hatua ambazo zimechukuliwa
na Serikali juu ya matatizo ya mafuta yanayoendelea.
Uamuzi huu
utaliwezesha bunge kutumia vizuri mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa katiba
ibara ya 63 ya kuishauri na kuisimamia Serikali katika kipindi hiki ambacho
hatma ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini haijulikani hata baada ya Spika
kukabidhiwa ripoti ya “Kamati ya Ngwilizi”.
Iwapo
Serikali itawasilisha tu kauli bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 Bunge
litafungwa na kanuni kwa kuwa kauli hizo za mawaziri hazipaswi kujadiliwa
wakati kuna masuala muhimu ambayo yanapaswa
kujadiliwa hata baada ya hatua zilizochukuliwa tarehe 02 Novemba, 2012 na Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo alipokutana na makampuni yanayohusika na biashara
ya mafuta na yenye maghala ya kuhifadhia mafuta nchini.
Serikali ieleze hatua zilizochukuliwa za
kuwawajibisha watendaji wa wizara, taasisi zake na makumpuni yaliyohusika
kusababisha hali hii kutokana na uzembe, udhaifu na uhujumu wenye athari kwa
uchumi wa nchi na maisha ya wananchi na bunge lipitishe maazimio ya hatua za
ziada za kuchukua iwapo matatizo haya yatajirudia tena katika taifa letu.
Bunge lijadili hatua iliyochukuliwa
ya kuagiza asilimia hamsini (50%) ya mafuta yaliyokuwa yanakwenda nje ya nchi
(Transit fuel) yauzwe ndani ya nchi iwapo ilitekelezwa kwa ufanisi na kwa
kuzingatia maslahi ya nchi kitaifa na kimataifa.
Bunge lipewe taarifa ya kina iwapo
meli za Miss Marelina iliyokuwa ikishusha mafuta (ikiwa na MT 22,039 za diseli
na MT 14,925 za Petroli) na Meli ya
Eskden inayoendelea kushusha mafuta (yenye MT 32,000 za dizeli) kuhakikisha
mafuta yake yanasambazwa kwa uwiano na kwa wakati mikoani kutokana na upungufu
uliopo hususan katika maeneo ya vijijini.
Serikali kupitia kwa Wizara ya
Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari (TPA) kueleza sababu za kuchelewa kujengwa kwa
Boya kubwa la kupakulia mafuta (SBM) toka mwaka 2011 na kueleza hatua
zinazochukuliwa kuhakikisha kwamba boya hilo linaanza kazi katika kipindi
kisichozidi wiki moja kuanzia sasa kama jambo la dharura.
Sababu za Serikali kutochukua hatua
dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (Petroleum
Importation Cordinator-PIC) iliyokuwepo toka mwanzoni mwa mwaka ilipolalamikiwa
na wadau na hatua zinazochukuliwa kwa haraka kufanya marekebisho ya kanuni
kukidhi mahitaji ya Mfumo wa Uagizaji wa
Pamoja ikiwemo mfumo mpya wa uundaji wa
bodi.
Serikali itoe maelezo ya hatua
iliyofikiwa katika uanzishwaji wa Mpango wa Hifadhi ya Akiba ya Mafuta ya Taifa
(Strategic Petroleum Reserve – SPR) ambao ungekuwa kinga ya nchi pale
panapojitokeza upungufu katika uingizaji wa mafuta au hujuma za mafuta kufichwa
katika maeneo mbalimbali na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Serikali kupitia Bunge iombe radhi
kwa wananchi kutokana na athari
zilizojitokeza kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na matatizo
ya mafuta kujirudia tena.
Wakati huo huo,
natoa mwito kwa EWURA pamoja na kutangaza bei mpya elekezi ieleze hatua ambazo
mamlaka hiyo imechukua mpaka sasa katika kuwafutia Leseni wafanyabiashara wote
ambao wana leseni za kuagiza mafuta lakini hawafanyi kazi hiyo na kutaja orodha
ya makampuni hayo kwa umma.
Pia EWURA
ieleze sababu za Serikali kuzidiwa nguvu
na wafanyabiashara ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji
(EWURA) inapotoa bei elekezi za kushuka
huficha mafuta kwa kisingizio cha kulalamikia kanuni ya kupanga bei safari hii
wakitarajia kupanda kwa bei jumatano ya kwanza ya mwezi tarehe 7 Novemba 2012.
Kutokana na
hujuma hizo tatizo la upungufu wa mafuta nchini limeongezeka kutokana na udhaifu
kwa kuzingatia kuwa taarifa za ndani ya maghala makubwa ya kuhifadhia mafuta zinadhihirisha kwamba pamoja za
uzembe wa uchelewaji uliotokea nchi isingekuwa katika matatizo makubwa ya
mafuta ikiwa hali hiyo ingedhibitiwa kwa Serikali
kusimamia utawala wa sheria kulinda maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Izingatiwe
kwamba EWURA ilitoa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari tarehe 5
Novemba 2012 kukanusha kuhusu mkanganyiko uliopo Waziri Mkuu Mizengo Pinda
amekiri bungeni kuwepo kwa kutofautiana kwa kauli baada ya kutakiwa kutoa
majibu na Spika kufuatia muongozo nilliomba wa kutaka Serikali itoe kauli
bungeni.
Nilieleza
kwamba pamoja na kauli ya Naibu Waziri Simbachawene tarehe 2 Novemba 2012
bungeni kuwa matatizo yamemalizika hali bado ni tete hususan mikoani hatua
ambayo ilimfanya Spika amtake Waziri Mkuu atoe majibu ambaye aliahidi kwamba
Serikali itatoa kauli kabla ya kuisha kwa shughuli za Bunge katika mkutano
unaoendelea. Hivyo, nitaendelea kuisimamia Serikali kuchukua hatua
zinazostahili kwa kadiri matatizo haya yatakavyoendelea.
Imetolewa
tarehe 6 Novemba 2012 na:
John Mnyika
(Mb)
Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini
Comments