Mabilioni ya Uswisi – Tusigeuzwe Mazezeta
Zitto Kabwe (MB) |
Na Zitto
Kabwe
Jumanne tarehe 20 Novemba
2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari zinazohusu matamshi ya Waziri
wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni ya
Uswisi.
Waziri amesema kwamba
Serikali ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio
waweze kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo
iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba
2012.
Nimeona ni vema nitoe
kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa juu ya Azimio
la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata
za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio
jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la Serikali ya Uswisi kutaka
majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja binafsi
niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya kuiondoa hoja
ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na
kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio
la Bunge.
Watanzania wasikubali
propaganda hii ya Serikali. Bunge limeagiza Serikali kufanya uchunguzi kwa
kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali
inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha
nini? Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye
Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje
(international transfers), leo Serikali inakuja na kauli za kukakata tamaa?
Kunani?
Pili, Watanzania wajue
kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi za wizi ambazo
watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha
huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya
Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi
binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya
Swiss.
Nawakumbusha kwamba mwaka
1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule
Kongo - Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa
njia haramu! Waswiss walitaka Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola
bilioni nane za Kimarekani Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze
kuzirejesha.
Zaire ilikadiriwa kuwa na
zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya nje ya nchi
hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi inapewa.
Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi
hivi.
Hatimaye Serikali ya
Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao
walioficha fedha Uswisi. Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia
majibu yao. Bila Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku.
Tunasahau historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta.
Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania
imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha
haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka Serikali ianze uchunguzi mara
moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge.
Suala hili sio suala la
kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala
hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la Wananchi.
Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao.
Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa
kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni,
ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni
kwenye mabenki nje ya Tanzania.
Hatutakaa kimya mpaka
tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni
salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha
na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona
hawezi kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta.
Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata kusema
Comments