· Liewig aahidi kupambana hadi mwisho
· Poppe aahidi mamilioni kwa wachezaji
· Kapombe asema Sunzu atawaua Waangola
Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul,
Angola
KOCHA
Mkuu wa Simba, Patrick Jean Elysee Liewig, amesema ana matumaini timu yake
itapata matokeo mazuri katika mchezo wa kesho baina ya Wekundu wa Msimbazi na
Libolo ya Angola.
Mechi
hiyo imepangwa kuchezwa kesho kuanzia saa tisa alasiri katika Uwanja wa Estadio
Libolo, uliopo katika mji mdogo wa Calulo jimbo la Kwanza Sul.
Katika
mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba ilifungwa 1-0 na mabingwa hao wa
Angola.
Hata
hivyo, Liewig alisema ingawa matokeo ya kufungwa nyumbani hayakuwa mazuri, ana
imani Simba nayo inaweza kufanya vizuri ugenini.
“Kama
wao walitufunga kwetu kwanini sisi tusiwafunge kwao. Ukiangalia kwenye ile
mechi ya kwanza wao walipata nafsi moja tu ya maana na wakaitumia. Sisi
tulipata nafasi kama tatu hivi na hatukutumia vizuri hata moja,” alisema.
Liewig
alisema ameridhishwa na ari na mazoezi mazuri ambayo Simba imefanya kwa wiki
nzima kujiandaa na mechi hiyo na kwamba kuna dalili kuwa timu yake inaweza
kufanya lisilotarajiwa.
Akizungumza
na wachezaji katika kikao kilichofanyika katika Hoteli ya Anisaan Ritz ambako
Simba imefikia, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Zacharia Hans Poppe,
alitoa ahadi ya Sh milioni 10 iwapo watafanikiwa kuitoa Libolo.
Aliwataka
wachezaji wa Simba kuwakumbuka mamilioni ya washabiki wao waliopo Tanzania
ambão hawalali wala kula vizuri wakati timu yao kipenzi inapokuwa na matokeo
mabaya.
Poppe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba na pia kundi la Friends
of Simba, alisema ana imani kubwa na wachezaji wa timu yake kwa vile ndiyo bora
Tanzania na kama wataamua kucheza kwa nguvu zao zote, matokeo mazuri
yanawezekana.
“Nyie
ni wachezaji wazuri sana. Kama nyote mtacheza kama timu na mkacheza kwa uwezo
wenu wote, ni wazi kwamba mnaweza kuibuka na ushindi,” alisema.
Akizungumzia
mechi ya kesho, nahodha msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe, alisema mechi baina
yao na Libolo itakuwa tofauti na ya kwanza kwa sababu ya kuwepo kwa
mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu.
“Tulimkosa
sana Sunzu kwenye mechi ya Dar es Salaam. Mipira ilikuwa haikai kule mbele na
hilo lilikuwa tatizo kubwa, kubwa sana na hiyo ni kwa sababu Sunzu hakuwepo.
Nadhani sasa tuna nafasi zaidi kuliko mara ya kwanza,” alisema.
Comments