Liwale/Arusha. Uharibifu mkubwa wa mali ulifanywa juzi usiku
Mjini Liwale, Lindi baada ya wananchi wenye hasira kuchoma moto nyumba za viongozi waandamizi, makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya na maghala ya mazao kutokana na kuchukizwa kushushwa kwa bei ya korosho.
Nyumba zilizochomwa moto ni za Mbunge wa Liwale
(CCM), Faith Mtambo, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja, Hassan
Myao na Makamu wake, Hassan Mpako, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Liwale,
Amina Mnocha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas
Chigogola ambaye pia ng’ombe wake tisa walikatwakatwa mapanga na
kuachiwa ndama watatu.
Nyingine ni nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya
ya Liwale, Mohamed Ng’omambo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Lindi,
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Minali, Mohamed Limbwilindi na Katibu wa
chama hicho, Juma Majivuno.
Wakati hayo yakitokea Lindi, huko Arusha, vurugu
kubwa za wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu zilizuka jana baada ya kuuawa kwa
mwanafunzi Henry Kago (22), juzi usiku.
Kago, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili,
anadaiwa kuwa alifariki juzi saa nne usiku baada ya kuchomwa kisu na
watu wasiojulikana, akiwa njiani eneo la Kanisa la Wasabato akitokea
chuoni hapo kujisomea.
Ghasia za Liwale
Ghasia hizo zilianza juzi mchana katika Kijiji cha Liwale B na ziliendelea usiku kucha hadi jana asubuhi.
Ghasia hizo zilianza juzi mchana katika Kijiji cha Liwale B na ziliendelea usiku kucha hadi jana asubuhi.
Watu walioshuhudia ghasia hizo walisema chanzo ni
wakulima kudai kulipwa Sh600 na siyo Sh200 za mauzo ya korosho kwenye
Chama cha Msingi Minali.
Bei ya kilo moja ya korosho waliyokubaliana
wakulima na chama hicho ni Sh1,200 na mara ya kwanza kiliwalipa Sh600
kwa kilo na kuahidi kulipa nusu nyingine baadaye.
Hata hivyo, viongozi wa Ushirika walibadili uamuzi
na kulipa Sh200 kwa maelezo kuwa mauzo hayakuwa mazuri kitendo ambacho
kiliwakasirisha wakulima hao ambao waligoma kupokea fedha hizo.
Baadaye ilielezwa kuwa viongozi wa Minali
walipeleka fedha hizo polisi ili malipo yafanyike huko, lakini ghasia
zikaibuka na wakaamua kusitisha malipo hayo na ndipo wananchi wakaamua
kuingia mitaani.
Mmoja wa mashuhuda alisema “Polisi walijaribu
kuwadhibiti watu hao, lakini walipoona wanazidiwa nguvu, wakawaachia
wafanye wanavyotaka ndiyo maana kumekuwa na uharibifu mkubwa.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga
alisema kwa kifupi: “Hali imetulia na vurugu zimemalizika lakini bado
tuko kwenye kikao kuzungumzia suala hili.”
Comments