Na Neema Mgonja
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imelazimika kuunda
kamati ndogo kuchunguza sakata la kuondolewa kwa mashine za kupimia
mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hiyo imefikiwa jana baada ya kamati hiyo kushindwa kupata
majibu ya kuridhisha kuhusiana na sakata hilo kutoka Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Vipimo
(WMA).
Awali viongozi wa TRA, TPA na WMA walionekana kujikanganya katika
maelezo yao hali iliyozua utata miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto, ndiye aliyeanza kuhoji sababu
ya kusitishwa matumizi ya mashine hizo ambazo zilikuwa zikitumiwa
kupima kiasi cha mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari hiyo, na
majibu yake kutumika katika kutoza kodi.
Akijibu suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TRA, Harry Kitilya,
alisema suala hilo lipo mikononi mwa WMA kwani ndiyo waliyotoa agizo la
mashine hizo kutofanyakazi tangu Februari 2, 2011.
Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa WMA, Magdalena
Chuwa, alisema ofisi ilitoa kibali cha kusitisha matumizi ya mashine
hizo baada ya kubaini hazifanyikazi kwa ufanisi.
Chuwa alisema zilivyofungwa mwaka 2004, WMA haikushirikishwa, lakini ilitoa kibali cha kuendelea kufanyakazi.
Alisema mwaka 2010 WMA ilipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa TRA
na wafanyabiashara wa mafuta waliokuwa wakilalamikia mashine hizo kuwa
zinahujumu.
Alisema baada ya malalamiko aliandika barua ya kuzifungia kwa vile
zilikuwa hazitendi haki kwa sababu kuna wakati zinazidisha kiwango cha
kodi na mara nyingine kupunguza.
Kauli hiyo ilianza kupingwa na wajumbe wa kamati hiyo, ambao walitaka
ufafanuzi kutoka TPA kuhusiana na mashine hizo zilizofungwa katika
bandari yao.
Hata hivyo, viongozi wa TPA walionekana kukwepa jambo hilo wakieeleza
kuwa haliko mikononi mwao bali linaihusu TRA ambayo ndiyo inayokusanya
kodi kupitia mashine hizo. Majibu hayo yalimuibua Makamu Mwenyekiti,
Deo Filikunjombe aliyemtaka Chuwa kufafanua vyema jambo hilo kwa kuwa
kuna kumbukumbu zinazoonesha aliandikiwa barua ya kuitwa na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hakwenda.
Ilielezwa katika barua hiyo kuwa Chuwa alitakiwa kukutana na CAG
pamoja na wawakilishi wa TRA na TPA kujadili suala la mashine hizo,
lakini hakutoa taarifa ya kutofika kwake.
“Tuna maelezo ya CAG hapa kuwa uliitwa katika kikao cha pamoja wewe
pamoja na TRA na TPA ili kujadili jambo hili, lakini haukufika kwenye
kikao, unaweza kueleza sababu ya kutokwenda kwenye kikao hicho?” alihoji
Filikunjombe.
Akitoa maelezo juu ya suala hilo, Chuwa alikiri kupata barua ya wito,
lakini hakwenda kwenye kikao na badala yake alimua kwenda binafsi kwa
CAG kuzungumza naye.
Alisema kilichompeleka kwa CAG ni kumpa maelezo ya kina juu ya jambo
hilo hususani maelezo ya kitaalamu yaliyosababisha WMA kusitisha
matumizi ya mashine hizo.
Hata hivyo, kauli hiyo ilizua mjadala na minong’ono miongoni mwa wabunge wa kamati hiyo, jambo lilomfanya Zitto kuingilia kati.
Zitto alihoji sababu iliyosababisha Chuwa kukimbilia kwa CAG na
kukataa kuhudhuria kikao cha wadau wote. ”Chuwa hapa kidogo
unatuchanganya, umesema ulienda binafsi kwa CAG kumuelezea na
kumfafanulia zaidi kuhusiana na jambo hilo, ilikuwaje uende binafsi na
ukaacha kusubiri kikao mlichoitiwa kutoa huo unaoita ushahidi? “alihoji
Zitto.
Akijibu jambo hilo, Chuwa alisema alishindwa kusubiri kikao hicho kwa
kuwa aliona CAG alikuwa amekosea na kwamba hakuwa na maelezo ya kutosha
kuhusiana na suala hilo.
Kauli hiyo ilizidi kuonesha mkanganyiko jambo lillilosababisha kamati
hiyo kuunda kamati ndogo kuchunguza mchakato wa kusitishwa kufanyakazi
kwa mashine hizo.
Hoja ya kuundwa kwa kamati hiyo imewasilishwa kwa Spika ili kupatiwa kibali ambapo itafanyakazi yake kwa muda wa mwezi mmoja.
Comments