RAIS KIKWETE KUFUNGUA MAONYESHO YA KIMATAIFA YA UTALII

indexSwahili Tourism Expol kufanyika Dar es Salaam
 
Na Mwandishi Wetu
 
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya kimataifa ya utalii yanayojulikana kama Swahili Tuorism Expo yanayotarajiwa kufanyika Dar es Salaam Oktoba mwaka huu.
 
Waziri wa Maliasili na Utalii Razaro Nyalandu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam alipozindua rasmi tovuti ya taarifa za maonyesho hayo inayojulikana kama Swahili Tourism Expo (S!TE).
 
Maonyesho hayo yatakayohusisha kampuni binafsi, taasisi za kiserikali kama Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na washirika wengine katika sekta hiyo yanatarajiwa kufanyika tarehe 1 mpaka 4 Oktoba, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam. 
Waziri Nyalandu alisema maonyesho hayo ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kupanua wigo wa sekta ya utalii ambapo nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na Sudan zinatarajiwa kushiriki lakini pia mataifa mbalimbali yataalikwa.
 
Alisema tayari 50% ya nafasi za maonyesho zimeshachukuliwa na kwamba mialiko kwa mataifa mbalimbali imeshatumwa ambapo ofisi yake itafuatilia kwa karibu mialiko hiyo na kuhakikisha nchi nyingi kwa kadri inavyowezekana zinashiriki.
 
“Kutokana na ukubwa wa tukio hili Rais Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi lakini pamoja na TTB kupewa jukumu la kuratibu pia ofisi yangu itachukua jukumu la kipekee  kufuatilia mialiko iliyotumwa nchi mbalimbali kuhakikisha zinashiriki,” alisema Waziri.
 
Aliongeza kuwa maonyesho hayo yanatarajiwa kuongeza biashara ya kitalii nchini ambapo baada ya hapo Tanzania inatarajiwa kupokea watalii zaidi ya milioni 2 kwani maonyesho hayo yataitangaza nchi husika kwa kiasi kikubwa.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTB, Balozi Charles Sanga alisema maonyesho hayo yatakuwa chachu ya kukuza utalii wa ndani na kuwajengea tabia watanzania kutembelea vivutio tulivyonavyo.
 
Alisema tumekuwa tukipokea watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja kujionea utajiri wa maliasili tulizonazo lakini idadi ya watalii wazalendo imekuwa ndogo sana ambapo pamoja na mambo mengine muamko na taarifa za vivutio hivi zimekuwa haziwafikii na hivyo maonesho hayo yatakuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii wa ndani.
 
“Maonyesho kama haya ni maarufu katika nchi za wenzetu na yamekuwa yanawasaidia sana katika kukuza sekta zao za utalii hivyo nasi tunaanza na litakuwa linafanyika kila mwaka,”
 
“Kupitia maonyesho haya sekta na biashara nyingi za kitalii zitapanuka lakini kubwa zaidi tunaamini baada ya hapo watanzania wengi watakuwa na taarifa za kutosha kuhusu maliasili tulizonazo na watahamasika na hatimaye kuongeza idadi ya watalii wa ndani ya nchi,” alisema Balozi Sanga.
 
Wizara ya Maliasili kupitia TTB imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa na mchango wa kipekee katika pato la taifa ambapo pamoja na maonyesho hayo pia ina mikataba mbalimbali ya matangazo na nchi mbalimbali duniani katika kuhakikisha taarifa za vivutio vyetu zinawafikia watu wengi zaidi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE