CHID BENZ APANDISHWA KIZIMBANI JIJINI DAR LEO KWA SHITAKA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA,AKOSA DHAMANA, KESI YAKE KUTAJWA TENA NOVEMBA 11
MSANII wa Muziki wa Kizazi Kipya (bongo fleva), Rashidi Abdallah
Makwaro (29),maarufa kama Chid Benz, amefikishwa mahakamani akikabiliwa
na mashitaka matatu ikiwemo kukutwa na Dawa za kulevya aina ya Heroin
yenye thamani ya Sh. 38,638, bangi ya Sh. 1,720 na vifaa ya kuvutia dawa
hizo kijiko na kigae.
Chid Benz amefikishwa mapema leo saa 3:00 asubuhi katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusomewa
mashitaka yake. Saa 7:50 mchana alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Warialwande Lema aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, hakimu aliamuru msanii huyo kutolewa nje ili akave vizuri
nguo baada ya suruali aliyokuwa amevaa mlegezo maarufu kama kata kei
kuonyesha nguo yake ya ndani.
“Kwanza mtoeni nje aende akavae nguo hizo zinazodondoka…” aliamuru Hakimu.
Saa 7:54 alirejeshwa ndani ya chumba cha mahakama upande wa Jamhuri
ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono akisaidiana na
Inspekta Jackson Chidunda, ulimsomea mashitaka yake.Wakili Kombakono
alidai kuwa Oktoba 24, mwaka huu katika uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere, uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa dawa za
kulevya aina ya heroin isivyo halali zenye uzito wa gramu 0.85.Katika
shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza,
mshtakiwa alikutwa na gramu 1.72 za bangi isivyo halali.Wakili huyo wa
serikali alidai kuwa, siku na eneo la tukio la kwanza na la pili,
mshtakiwa alikutwa akiwa na vifaa vinavyotumika kuvua dawa za kulevya
aina ya heroin, kigae na kijiko huku akijua ni kosa.
Mshtakiwa alikana mashitaka yote na upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi na dhamana dhidi ya mshtakiwa.
Hakimu Lema alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa masharti ya
kuwa na wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi zinazoamini na siyo
walimu na dhamana ya Sh. Milioni moja.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na amepelekwa mahabusu hadi Novemba 11, kesi hiyo itakapotajwa.
Chanzo;michuzi blog
Comments