Njaa si siri tena

*Ukame wakumba maeneo mbalimbali 
*Vyakula vyapanda bei, wanyama wafa

Waandishi Wetu


NJAA na ukame sasa ni dhahiri nchini. Hiyo ndio hali halisi iliyoikumba mikoa kadhaa iliyosababisha ongezeko la bei za vyakula.

Uchunguzi uliofanywa na JAMBOLEO umebaini kwamba wananchi wa mikoa ya Mara, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora, Arusha, Manyara na Tanga wanalia ukame kukithiri kila kukicha.

Taarifa zinaonesha kwamba wilayani Bunda, Mara, wananchi wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula huku bei ikipanda kwa kasi.

Uchunguzi kwenye maeneo mbalimbali na kwenye masoko wilayani humo, ulibaini kuwa bei ya chakula ilipanda kuanzia Agosti na Septemba mwaka jana.

Ulionesha bei ya chakula kupanda kutoka Sh 14,500 kwa debe la mahindi hadi Sh. 20,000;  mtama kutoka Sh 10,000 hadi Sh 17,500;  unga wa muhogo kutoka Sh 12,500 hadi Sh 17,500 na ulezi unauzwa Sh 30,000 kwa debe.

Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka kwenye soko kuu la mjini humo na mji mdogo wa Kibara jimboni Mwibara, walisema bei ya chakula imepanda kutokana na upungufu mkubwa wa nafaka.

Mkazi wa eneo hilo, Esther Samson alisema hali hiyo ilisababishwa na mvua kutonyesha wilayani humo kwa kipindi kirefu na kusababisha mazao yaliyolimwa kunyauka.

Esther alisema wamekuwa wakiuza chakula wanachopata kutoka mikoa jirani kwa bei ya juu ili kurudisha mtaji na kupata faida kidogo.

“Hali ya chakula kwenye soko letu ni mbaya maana kimepanda kutokana na sisi tunavyouziwa kwa bei ya juu. Na hii hali tuseme ilianza Agosti na Septemba mwaka jana. Sasa hivi gunia la mahindi tunanunua kati ya Sh 110,000 na Sh 120,000,” alisema.

Mkazi wa kijiji cha Changuge, Juma Mabyora alisema wanakabiliwa na njaa kubwa na hali hiyo inatokana na ukame na pia baadhi ya mazao mashambani yalishambuliwa na tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti.

 “Jamani tusidanganyane, hali ya njaa katika wilaya yetu iko wazi, baadhi ya familia zinakula mlo mmoja, tena zingine zinashinda na kulala na njaa. Kwanza hata fedha hazionekani, yaani hali ni mbaya sana. Sasa angalia eti kilo tano za mahindi tunauziwa Sh 4,000,” alisema na kuongeza:

 “Tunaomba Serikali ituletee chakula hata cha bei nafuu, maana hali ni mbaya sana katika maeneo yetu.”

Diwani wa Bunda Mjini, Joash Kunaga na Diwani wa Bunda Stoo, Daud Chiruma walisema wakazi wa kata zao wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula na bei ya chakula ambacho kimekuwa kikipatikana iko juu, hali ambayo inasababisha wengine kushindwa kununua.

Diwani wa Nyamuswa, Fyeka Sumera naye kama wenzake alisema wakazi wa kata yake wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula

Kilimanjaro

Wananchi wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wamekumbwa na hofu kubwa ya kukumbwa na  njaa  muda wowote kutokana na ukame uliokithiri wilayani humo kutokana na mazao yao kukaukia mashambani, hivyo kuambulia mabua.

Walisema tatizo la chakula linaonekana kuwa kubwa kutokana na ukame ambao ni mkubwa wilayani humo kwani tangu mwaka jana hawakupata chakula cha kutosha.

Mkazi wa wilaya hiyo, Andrew Laizer alisema kwa sasa hali ni mbaya kwani mazao waliyopanda yalikaukia mashambani.

Kwa hofu hiyo kubwa ya kukumbwa na njaa waliiomba Serikali kuchukua hatua ya kuwanusuru na baa hilo ambalo litawasababisha kula mizizi.  

Mbunge wa Siha, Godwin Molel akizungumzia upatikanaji wa chakula wilayani humo, alisema ni mbaya kwani kwa mwaka jana chakula hakikupatikana, hivyo aliahidi kufikisha suala hilo ngazi husika, ili wananchi wanusuriwe na baa hilo.

Alisema ameshirikisha madiwani wa wilaya hiyo, kuangalia namna ya kukabiliana nalo lakini atahakikisha analifikisha ngazi husika kukabiliana na hali hiyo ili kunusuru wananchi hao.

"Kweli baa la njaa wilayani hapa lipo na katika kunusuru nina mpango wa kwenda kuonana na Waziri Mkuu kumweleza hali halisi ilivyo, ili waone jinsi ya kunusuru wananchi hawa ambao tayari wana hofu ya kukumbwa na njaa, ili serikali iwasaidie chakula," alisema Molel.

Pwani, Moro

Hali hiyo imeonekana pia Pwani na Morogoro ambako pamoja na wananchi kukosa chakula hata mifugo imekuwa ikifa kila siku huku bei za vyakula zikipanda.

Mfugaji Solengei Saitoti wa Morogoro alisema  ameshapoteza mifugo zaidi ya 50 huku kukiwa hakuna dalili za mvua kunyesha ili kuikoa.

Hali ya Hewa

Ikizungumzia hali ya mvua nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilisema mvua itaendelea kunyesha maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka kati ya Januari na Februari.

Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri wa Hali ya Hewa, Samwel Mbuya alisema kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, mvua za vuli zilizokuwa zinaanzia Novemba hadi Desemba mwaka jana umeshapita.

Mbuya alisema maeneo ya Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kusini Magharibi zenye mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, yanatarajiwa kupata mvua za kiwango cha wastani katika kipindi hiki.

Aidha, alieleza kuwa Kanda ya Kati yenye mikoa ya Singida na Dodoma, inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya kiwango, huku Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi itakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Mbuya alisema maeneo ya Kaskazini mwa nchi yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Simiyu na Manyara ambayo huwa na misimu miwili ya mvua kwa mwaka, msimu wa vuli umemalizika.

Aliongeza kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa pia itaendelea kupata mvua za kawaida.

Aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa, ili kujua mwenendo wa  mvua na pia ushauri wa wataalamu katika masuala hayo, ambapo alibainisha kuwa  kufanya hivyo kutawasaidia kwenye shughuli za kiuchumi na kilimo.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

LICHA YA UZURI WAKE MWANADADA ELIZABETH MICHAEL a.k.a LULU SI MALI KITU MBELE YA RAY, AMKWEPA KUOGOPA AIBU.

KWA HERI KAMANDA WETU ABBAS KANDORO

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA

YANGA SC WAANZA KAZI AFRIKA LEO…WANAKIPIGA NA U.S.M. ALGER SAA 4:00 USIKU ALGERIA

NCHI YA URUSI NDIYO NCHI INAYOONGOZA KWA KUWA NA UBORA WA ELIMU NA VYUO DUNIANI.