WANANCHI WATAKIWA KUTOA TAARIFA KWA VYOMBO HUSIKA PALE UOVU UNAPOFANYIKA KATIKA JAMII ILI HATUA ZICHUKULIWE
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameungana na viongozi wa dini pamoja na watanzania kwa ujumla katika Dua na Maombi kwaajili ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano, Dua na Maombi hayo yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma leo tarehe 22 Aprili 2024.
Vilevile Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kuthamini ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Taasisi za dini nchini na itaendeleza ushirikiano huo kwa manufaa na ustawi wa Taifa.
Amewashukuru viongozi wote wa dini nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa pamoja na kuendelea kukemea maovu, kuonya, kufundisha maadili mema na kutoa huduma za kiroho na kijamii kwa Watanzania.
Aidha, amewapongeza Viongozi wa Dini kwa mchango mkubwa katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kubaki wamoja na kuendelea kushirikiana licha ya tofauti za dini, kabila, rangi, ufuasi vyama vya siasa au mahali wanapotoka.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema vijana wa sasa wana kisa sababu kuhakikisha wanaulinda, kuusimamia, kuimarisha na kutetea muungano ili uendelee kudumu daima na vizazi vijavyo viukute Muungano ukiwa salama na wenye mafanikio makubwa.
Amesema Muungano unadumisha umoja, amani, mshikamano na upendo na kutoa uhuru kwa wananchi wa pande zote mbili kuweza kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi.
Dua na Maombi hayo yameongozwa na viongozi wa dini pamoja na kujumuisha waumini, waimbaji wa muziki wa dini wa kikristo na kiislamu.
Aidha maombi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Wabunge pamoja wananchi mbalimbali.
Comments