TANZANIA KUNUFAIKA NA MAFUNZO NCHINI INDIA

*




Bunge la India limeahidi kutoa fursa zaidi za mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa umma kupitia Taasisi yake ya Utafiti na Mafunzo ya Kidemokrasia (PRIDE) inayoendeshwa na Bunge hilo. 


Ahadi hiyo imetolewa leo tarehe 23 Julai, 2024 na Spika wa Bunge la India (Lok Sabha), Mhe. Om Birla wakati wa mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika Ofisi za Bunge hilo Jijini New Delhi. 


Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Mhe. Birla amemuelezea Dkt. Tulia kuhusu maboresho yaliyofanywa na Taasisi hiyo  ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya ufadhili kwa Watumishi wa umma kutoka nchini mbalimbali Duniani hususani Wabunge na Watumishi wa Mabunge ya nchi hizo. 


Vilevile, Mhe. Birla ametoa kipaumbele mahususi kwa Watumishi wa Tanzania kwa kuzingatia urafiki, historia na uhusiano uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na India.  Aidha, kwa kutambua pia nafasi ya Dkt. Tulia kuwa Rais wa IPU, ameahidi kupitia PRIDE kushirikiana na IPU kuandaa mafunzo kwa Watumishi na Wabunge Wanachama wa Umoja huo. 


Sambamba na hilo, Maspika hao wamezipongeza Serikali zao kwa kuendelea kuimairisha uhusiano wenye kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya Nchi hizo. 


"Ushirikiano baina ya Serikali zetu umeimarika zaidi baada ya  ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mwaka jana imeongeza wigo wa ushirikiano na ndugu zetu wa India. Wajibu wa Mabunge yetu ni kushirikina kwa kuzisimamia na kuzishauri vyema Serikali zetu kutekeleza mikataba hiyo kwa manufaa ya Wananchi wetu". Amesema Dkt. Tulia


Aidha, Dkt. Tulia ametumia fursa hiyo kulishukuru Bunge la India kwa kumuunga mkono wakati wa kampeni za Uchaguzi wa Urais wa IPU pamoja na Bunge hilo kuendelea kusimamia misingi ya demokrasia, utawala bora  na kuongeza idadi ya Wabunge wanawake na makundi maalum katika Bunge hilo.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

BREAKING NEWS | MKURUGENZI MTENDAJI WA TANESCO AFARIKI DUNIA

#MAKINIKIA: HEKAYA FUPI YA MJI WA KIHISTORIA WA MOSHI MKOANI KILIMANJARO

SHEREHE ZA DKT. CHANDE KUSIMIKWA UASKOFU MKUU KANISA LA KARMELI ZAFANA

HUU NDIO UKWELI ULIVYO RAFIKI YANGU

RATIBA KAMILI YA HARUSI YA DIAMOND, ZUCHU

ZIJUE TABIA 9 ZA WANAWAKE HAWA....

BODI YA LIGI YAKIRI MAKOSA, WAIOMBA YANGA WAYAMALIZE

TANZANIA NI MIONGONI MWA NCHI 10 ZINAZOONGOZA KWA MAZAO YA KILIMO AFRIKA