Timu ya Taifa ya Soka ya U17 ya Tanzania (Serengeti Boys) imevunja kambi yake leo pale Tiffany Diamond Hotel huku wachezaji wakitakiwa kuripoti kambini tarehe 4 Julai 2026 kwajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia la FIFA kwa U17.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida vijana hao walidondosha machozi jioni ya leo walipokuwa wanaongea na Kocha wao na kupata taarifa kwamba ile pesa 500M iliyoahidiwa na Serikali kupitia Waziri Mkuu bado mchakato wake haujakamilika, hivyo waondoke waache namba za akaunti zao za benki na pesa “urua” zitawekwa humo wao wakiwa majumbani kwao.
Tayari akaunti zao zinasoma 2M kila mmoja ambayo wameingiziwa na TFF, lakini mchakato wa 500M za Serikali unaendelea, wameambiwa pia kama watahitajika Bungeni watapewa taarifa pia, ila kesho baada ya chai asionekane mtu Tiffany Hotel.
Kinachowatesa ni historia kwamba mwaka 2024, wakiwa Kampala ambako walipata ushindi wa pili, waliambulia 700k, wakaambiwa waache akaunti zao urua ungewekwa baadeni, lakini hawakupewa. Mwaka 2025 waliambuliwa 500k wakaambiwa pia waache akaunti namba za benki na kwamba “mchele” ungeingizwa lakini haikuwa hivyo.
Hizo historia ndo zinawakosesha raha vijana na kuhoji kwamba ahadi ilitolewa Jumatatu na mechi ilikuwa Jumanne na wala haikuwa inasubiri matokeo ya mechi, ilisemwa kwa kufika fainali wanapata 500M na Viwanja Morogoro, kwanini mchakato haukuanza kabisa ili leo wakiwa wanavunja kambi mzigo uwe umeingia? Wanasema “mchuzi wa mbwa hunywewa ungali wa moto, ukipoa unanuka”
Binafsi naamini ni uelewa mdogo tu wa taratibu za kiserikali na kibenki (kiutendaji) kuhusiana na masuala ya kifedha, lakini vijana watapata chao, wao kukosa imani nawaelewa lakini wawe na imani na serikali, hawatopigwa changa. Ila nadhani baada ya hapa watendaji watachangamka kama jambo la dharura na vijana watashika chao baada ya muda mfupi.
Ameandika @jemedarisaid

Comments