WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA AHITIMISHA MAFUNZO YA CHUO CHA UKAMANDA NA UNADHIMU DULUTI
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 27 Juni, 2026 amehitimisha rasmi mafunzo ya mwaka mmoja ya Kozi ya Ukamanda na Unadhimu katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania, yaliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Duluti, mkoani Arusha.
Mahafali hayo, ambayo Dkt. Nyansaho alikuwa Mgeni Rasmi, yalihusisha jumla ya maafisa wahitimu 82 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na maafisa kutoka nchi mbalimbali rafiki. Mbali na kuhitimu Kozi ya Ukamanda na Unadhimu, wahitimu hao pia walitunukiwa Shahada za Umahiri na Stashahada katika Masuala ya Ulinzi na Usalama, mafunzo yaliyotolewa sambamba na kozi hiyo ili kuwawezesha kupata maarifa ya kina kuhusu masuala ya ulinzi, usalama na uongozi wa kimkakati.
Akizungumza katika mahafali hayo, Waziri wa Ulinzi na JKT aliwapongeza wahitimu kwa mafanikio yao, akieleza kuwa kuhitimu kozi hiyo ni ushahidi wa bidii, nidhamu, ujasiri, uthabiti na kujitolea kwao katika kipindi chote cha mafunzo. Alibainisha kuwa kozi hiyo ni miongoni mwa mafunzo ya kijeshi yanayotambulika kimataifa na kwamba wahitimu wanapaswa kujivunia mafanikio hayo makubwa.
“Mmethibitisha uwezo wa kukabiliana na changamoto za mafunzo makali na mmeonesha sifa za uongozi zinazohitajika kwa viongozi wa kijeshi wa sasa na wa baadaye. Mafanikio haya ni hatua muhimu katika safari yenu ya uongozi na utumishi kwa mataifa yenu,” alisema Dkt. Nyansaho.
Aidha, Waziri huyo aliushukuru uongozi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Stephen Mnkande, kwa maandalizi mazuri ya mafunzo hayo na kwa kumpa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 40 ya chuo hicho.
Katika hotuba yake, Dkt. Nyansaho alisisitiza kuwa majeshi ya ulinzi yanaendelea kuwa alama ya umoja wa kitaifa, uhuru na mshikamano wa mataifa. Alieleza kuwa pamoja na jukumu la msingi la kulinda mipaka na mamlaka ya nchi, majeshi ya ulinzi yameendelea kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na maafa, kujenga miundombinu, kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa pamoja na kushiriki katika operesheni za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa na taasisi mbalimbali za kikanda.
Waziri huyo pia alieleza kuwa mazingira ya usalama duniani yanaendelea kubadilika kwa kasi na kuibua changamoto mpya na ngumu zaidi za kiusalama, zikiwemo vita vya kisasa, ugaidi, uhalifu wa kimtandao, mashambulizi ya kiteknolojia na vitisho vingine vya kiusalama vinavyovuka mipaka ya nchi. Alisisitiza kuwa hali hiyo inahitaji majeshi ya ulinzi kuendelea kujiimarisha, kubadilika na kuendana na mahitaji ya wakati.
“Dunia ya leo inakabiliwa na mazingira mapya ya kiusalama ambayo yanahitaji viongozi wenye uwezo wa kufikiri kimkakati, kufanya maamuzi sahihi kwa wakati na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zisizotabirika. Elimu mliyoipata imewaandaa kwa jukumu hilo kubwa,” alisisitiza.
Kwa upande wa maafisa wanawake waliohitimu, Dkt. Nyansaho aliwapongeza kwa mafanikio yao na kueleza kuwa ushiriki wao katika kozi hiyo ni ushahidi wa maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya ulinzi na usalama unaimarishwa.
Alisema kuwa wanawake ni sehemu muhimu ya jumuiya ya kijeshi na kwamba kuhitimu kwao kunathibitisha kuwa wanawake wana uwezo wa kutekeleza majukumu ya ulinzi na usalama kwa ufanisi, weledi na kujituma bila kujali tofauti za kijinsia.
Aidha, alieleza kuwa Tanzania inajivunia kuongozwa na Rais wa kwanza mwanamke, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Kwa mujibu wa Waziri huyo, uongozi wake ni ushahidi wa uwezo wa wanawake kushika nafasi za juu za uongozi na mchango wao katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo ya taifa.
Aidha Dkt. Nyansaho akaongeza kwa kuwaambia wahitimu hao, “Natambua mmepewa dhamana kubwa ya uongozi, mawazo ya kimkakati na ustadi wa kufanya maamuzi. Nyinyi ni viongozi wa baadaye wa majeshi yetu, walinzi wa usalama wa mataifa yetu na walinzi wa uhuru wetu unaothaminiwa.”
Aliongeza kuwa elimu na ujuzi walioupata utakuwa msingi imara wa utekelezaji wa majukumu yao ya baadaye na utawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali watakazokutana nazo katika utumishi wao.
Waziri huyo pia aliwakumbusha wahitimu kuwa uongozi wa kweli hauhusu vyeo au nyadhifa, bali unahusu uwezo wa kuongoza kwa mfano, kuhamasisha wengine, kufanya kazi kwa ushirikiano na kudumisha maadili ya heshima, uadilifu, nidhamu na uwajibikaji.
“Ulimwengu tunaouishi unabadilika kila siku na changamoto za kiusalama zinazidi kuwa ngumu na zisizotabirika. Mnapaswa kutumia maarifa na uwezo mliopewa kukabiliana na changamoto hizo kwa ujasiri, ubunifu na uthabiti,” alisisitiza.
Vilevile, Waziri wa Ulinzi na JKT alizishukuru nchi rafiki za Burundi, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Kenya, Eswatini, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Uganda, Zambia na Zimbabwe kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja za mafunzo ya kijeshi kwa kutuma maafisa wao kushiriki katika Kozi ya Ukamanda na Unadhimu.
Alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini ushirikiano na urafiki wa muda mrefu uliopo kati yake na mataifa hayo, na kwamba ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa kupitia mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu na ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama.
Mahafali hayo ya 40 ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Wakuu wa Majeshi wastaafu wa JWTZ, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, Wakuu wa Kamandi za JWTZ, Wakuu wa Vyuo vya Ukamanda na Unadhimu vya Afrika Mashariki, Wakuu wa Vyuo vya Kijeshi vya JWTZ, Waambata wa Kijeshi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, maafisa wakuu kutoka Makao Makuu ya JWTZ pamoja na makamanda wa vikosi mbalimbali vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.





Comments