BRELA, MAOFISA BIASHARA KUSHIRIKIANA KUTEKELEZA DIRA 2050


NA MWANDISHI WETU, DODOMA

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amewaelekeza Maofisa Biashara nchini kushirikiana kwa karibu na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo, ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ili kutekeleza kikamilifu Dira 2050.


 Londo ametoa maelekezo hayo leo, tarehe 17 Agosti 2026, alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tatu cha Wizara na Maafisa Biashara Nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.


Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi, Londo alieleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini hivyo ni muhimu kushirikiana.


“Ninawasihi mkatumie nafasi zenu kuwa wawezeshaji wa kweli wa biashara na uwekezaji hapa nchini. Nendeni mkawafikie wafanyabiashara, tembeleeni viwanda, tambueni fursa, tatueni changamoto kwa wakati na hakikisheni huduma mnayoitoa inachangia kukuza uchumi wa wananchi na Taifa,” alisisitiza Londo.


Aliongeza kuwa Dira 2050 inataka sekta ya umma kutoka kuwa mdhibiti wa biashara kwenda kuwa mwezeshaji wa Viwanda, biashara na uwekezaji.


 Hivyo, Maafisa Biashara mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutambua na kuondoa urasimu usio wa lazima, kutoa taarifa sahihi, kurahisisha upatikanaji wa leseni, kusaidia urasimishaji wa biashara na kuhakikisha wafanyabiashara hawapotezi muda kwa kuzunguka katika ofisi nyingi kupata huduma.


“Katika mwaka 2025, thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi iliongezeka kwa asilimia 16 na kufikia dola za Marekani milioni 10,080.9, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,702 mwaka 2024 ongezeko hilo limetokana na kupungua kwa baadhi ya vikwazo vya biashara pamoja na sababu nyingine,” ameeleza Waziri Londo. 


Awali, akimkaribisha Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,  Balozi Waziri Rajab Salum, aliwahimiza Maofisa Biashara kwenda kupambana, kudhibiti na kuondoa tatizo la uwepo wa bidhaa feki zinazoingizwa katika maeneo yao ya kazi. Aidha, aliwataka kuzingatia misingi ya ukweli, uchapakazi, uaminifu, utu na kumcha Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao.


Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alibainisha kuwa kuelekea katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (Dira 2050), BRELA imeendelea kufanya maboresho makubwa ya mifumo yake pamoja na marekebisho ya sheria inazosimamia, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za usajili na leseni, kupunguza muda na gharama za kuanzisha na kuendesha biashara nchini.


“Maboresho hayo yanaongeza uwazi katika utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi na kupunguza mianya ya rushwa na uzembe katika utoaji wa huduma.


Kupitia maboresho ya mfumo wa BRELA Online System (BOS), huduma zote za Wakala zimeunganishwa katika mfumo mmoja.


 Mfumo huo una uwezo wa kuwezesha utoaji wa leseni za biashara Kundi A na Kundi B, hivyo kutoa fursa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) kutumia mfumo huo katika utoaji na usimamizi wa leseni za Kundi B bila kuathiri mapato ya kila Halmashauri,” alisema Nyaisa.


Kikao hicho cha siku mbili kinafanyika kwa mara ya tatu na kuwakutanisha Maafisa Biashara kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, kikiwa na kaulimbiu: “Ofisa Biashara Kinara: Kukuza Biashara, Viwanda na Masoko kuelekea Dira 2050.”









Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

KOCHA WA MC ALGERS AIHOFIA YANGA

VIONGOZI NA WATENDAJI WA MATAWI UVCCM PANGANI WANOLEWA

NMB YAWAUNGANISHA WANANCHI NA HUDUMA, FURSA ZANZIBAR

HIZI HAPA TAKWIMU ZA PETER SHALULILE MCHEZAJI MPYA WA YANGA SC 🔰 🔥