ZAO LA CHAI LAWA LULU RUNGWE

Moja ya mashamba ya Chai wilayani Rungwe
na Christopher Nyenyembe


  
MKOA wa Mbeya unasifika kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula, hivyo kuwafanya wananchi wake kupiga hatua kiuchumi ikilinganishwa na mikoa mingine.
Umaarufu wa mkoa huo umezidisha ushindani katika nyanja ya kilimo, huku wakulima wakiiomba serikali iwekeze zaidi kwenye kilimo cha tija cha kibiashara kwasababu mazao mengi yanayolimwa huiingizia serikali fedha za kigeni.
 Kwa kulizingatia hilo, Tanzania Daima iliwatembelea wakulima wa zao la chai linalolimwa kwa wingi katika Wilaya ya Rungwe na hivyo kusaidia kubadili mfumo wa maisha ya wakazi zaidi ya 15,000 wa wilayani humo.
 Ili kuweza kukidhi matarajio ya wakulima hao, Tanzania Daima katika uchunguzi wake ilitembelea vijiji mbalimbali ili kubainisha mafanikio na changamoto zinazowakabili wakulima wa chai.
 Harakati za kujua kitu gani kinajiri zaidi katika kilimo hicho zilianzia katika Kijiji cha Katumba ambapo mkulima Steven Mwaikuka anaelezea kilimo cha chai katika kijiji hicho kinachowajumuisha wakulima zaidi ya 200.
Mwaikuka anasema nguvu waliyonayo inatokana na uelewa wao ambao umewasaidia kufufua mashamba ya zamani na kupanda miche mipya iliyoongeza uzalishaji na kipato.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Chai kijijini hapo, Rajabu Sanga, anasema nguvu waliyonayo imetokana na Umoja wa Wakulima wa Chai Wilaya ya Rungwe (RSTGA) kuwaunganisha wakulima, kuwatetea na kuwa kiungo kikubwa na Kampuni ya Chai ya Wakulima (WATCO).
 Issa Mwanyumba mkulima wa Kijiji cha Syukula mwenye cheti cha ukulima bora cha mwaka 2007 na tuzo ya tani moja ya mbolea anaweka wazi mafanikio yake na kwa uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 25 tangu alipoanza kulima zao hilo.
Huku akijigamba kuwa kila mwisho wa mwezi hulipwa mshahara na kiwanda cha chai Katumba sawa sawa na mfanyakazi wa serikali, anasema anaishi maisha bora akiwa amejiajiri kwa ukulima.
Siri ya mafanikio hayo anasema imetokana na umoja wa RSTGA tangu ilipoanzishwazaidi ya miaka 10 iliyopita.
Umoja huo umewajengea sifa na heshima kubwa na kudai kuwa wale walioweza kung'oa miche yao awali sasa wanajutia uamuzi huo kutokana na zao hilo kugeuka lulu na linazidi kujibebea umaarufu wilayani humo.
 Mawazo ya mkulima huyo hayatofautiani na wengine katika vijiji kadhaa ambapo Tanzania Daima ilipita.
Wakulima wanadai wangeweza kupiga hatua zaidi kwa masuala mawili, kwanza bei ya zao hilo na pili ni serikali kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima wa chai.
"Kilimo cha Chai ni kizuri sana na tumeweza kupiga hatua mbalimbali kupitia umoja wetu wa RSTGA na kufanikiwa kuendesha miradi ya kijamii, kama shule, zahanati, maji na umeme wa jua vijijini na kuipunguzia serikali kazi ya kuendesha miradi hiyo.
"Serikali kwa kutambua mchango wetu itoe ruzuku kwenye pembejeo" anasema Rebecca Kanyilenge mkazi wa Kijiji cha Kagwina.
Anasema vurugu katika zao hilo zilizokuwa zikiletwa na Chama cha Ushirika Wilaya ya Rungwe (RUTECO) kilichofutwa mwaka jana na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika zilichangia kuleta ufaambao sasa umezibwa na serikali kupitia mrajisi.
Anasema na hao wanaoleta vurugu hizo kwa uchu wa madaraka watoto wao wanasoma shule zilizojengwa na umoja huo.
Kanyilenge anasema umoja wao umekuwa ukitoa ruzuku ya mbolea na dawa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima na sasa wanajivunia mbinu mpya ya uchumaji wa chai kwa kutumia mikasi ya kisasa ambayo imerahisisha wepesi wa kuchuma chai kwa haraka tofauti na kipindi cha nyuma walipokuwa wakitumia mikono.
 Mkulima huyo anaonekana kuumizwa na vurugu za kibiashara zinazofanywa na wakulima wachache waliokuwa wafuasi wa RUTECOambao nguvu zao sasa wamezielekeza kwa mwekezaji mwingine kinyume na umoja wao na ubia na WATCO kwani wapo upande wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL).
Mazingira hayo ndiyo yaliyoweza kuchokoza hali na moyo walionao wakulima katika kilimo cha zao hilo na kutafuta dawa ya kutibu mvutano wa kibiashara ambao baada ya kufutwa kwa RUTECO joto la kung'ang'ania soko limeelekezwa upande wa pili, kati ya RSTGA,WATCO na METL.
Hapo ndipo wimbi na misukosuko ya kibiashara ilipoanza kujitokeza na kuamsha makucha ya serikali ili kuweza kufikia suluhu na sababu za kimsingi za kuwaweka salama wakulima hao na mafanikio yao ya zaidi ya miaka 10 katika umoja wao huku wakiwa na hisa zipatazo 30 katika kiwanda chai Katumba na Mwakaleli.
 Tanzania Daima iliweza kusaka mahitaji ya msingi ya wakulima wengine katika kukuza uzalishaji wa zao hilo linalozidi kukua ikilinganishwa na miaka mingine ya nyuma iliyosababisha Kampuni ya Mamlaka ya Chai ife na kubinafsishwa.
 Joel Mwakalebela (76) wa Kijiji cha Segela aliyeanza kulima zao hilo mwaka 1965, anasema mbali ya chokochoko za soko zinazojitokeza hivi sasa zilizo ndani ya uwezo wa serikali kusuluhisha, wao kama wakulima wameapa kuulinda umoja wao uliosaidia kurudisha heshima ya zao hilo na wale walioacha kulima wameanza kupata miche upya.
 Anasema nguvu iliyopo umoja huo baada ya Kampuni ya Chai kuwakatisha tamaa awali kwa kukaa zaidi ya miezi sita bila kulipwa fedha zao, hivi sasa wamekuwa wakifanya biashara nzuri kwani kwa kupitia RSTGA na WATCO kila mwisho wa mwezi wanalipwa fedha zao za mauzo kwa wakati.
Mwakalebela anasema suala linalowaumiza ni pembejeo za kilimo kwa kusema kuwa serikali isipoweka mkono wake kwenye ruzuku faida haitakuwa kubwa kutokana na gharama zilizopo licha ya kudai wana umoja imara na wameweza kunufaika ila nguvu bado inahitajika katika msukumo wa bei.
"Sisi wakulima tunapaswa zaidi kuulinda umoja wetu, tusiwe watu wa kudanganyika kirahisi na wawekezaji wengine wanaotaka kujitajirisha kwa mgongo wetu na kutugawa, tuliumwa na nyoka huko nyuma sasa tunaona fahari kuwa na RATGA yenye nguvu na ni mali yetu kwa kuwa tuna hisa" anasema Mwakalebela.
 Mpoki Mwakalikamo mkazi wa Kijiji cha Katundulu anasema ili kuhakikisha chai inazidi kuongezeka na kuwa maarufu zaidi katika Rungwe ipo haja ya kuelekezwa zaidi kilimo cha kisasa cha umwagiliaji hasa wakati wa kiangazi kwani chai hukauka katika maeneo mengine kutokana na jua kali.
 Anasema kuna umuhimu wa kuwa na vitendea kazi na vifaa vya kumkinga mkulima kama vile viatu vya boti, makoti, miwani ya kujikinga na wadudu na vifaa vya kuvaa mdomoni wakati wa kupuliza dawa.
Endapo watajipanga kupitia umoja wao anasema vitu hivyo vinaweza kutolewa kwa mkopo na wakulima wakalipa polepole.
Merica Mwakajila (77) mkazi wa Kijiji cha Masebe na Andongwisye Mwasifila (86) wa Kijiji cha Lulasi ambao ni waanzilishi wa kilimo cha chai wilayani hapo wanasisitiza umuhimu wa zao hilo kuzidi kupanda thamani kwa kuwa limekuwa mkombozi kwa wakazi wengi kiuchumi.
 Huku wakisisitiza jitihada za serikali zinapaswa kuonyeshwa hivi sasa kwa kuwasaidia wakulima kwani hawajaona msaada wowote na kuusifia umoja wao unaojitahidi kuwajali, huku wakionyesha wasiwasi kutokana na ugomvi wa kibiashara ulioanza kuonyeshwa na METL kuwa unawagawa wanachama wa RSTGA.
 Miongoni mwa wakulima walioweza kutamba na manufaa ya zao hilo la biashara na kuonyesha dhamira ya kuliendeleza kwa kasi ni wakulima wa Kijiji cha Mpanda ambao Tanzania Daima iliweza kuwabahatisha wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Chai ya kijiji hicho pamoja na mambo mengine, waliweza kuwajadili wakulima wenzao wanaofanya uhasi.
 Mwenyekiti wa Skimu ya Lupata/Itete, Afwilile Mwakywaja akiwa na wanakamati zaidi ya 10 wanaeleza haja ya mwekezaji wa mashamba ya Msekela na Chivanje kufufua kwanza mashamba yake badala ya kujiingiza kwenye mgogoro wa kuwagawa wakulima.
"Zao la chai limetufanya watu wa Rungwe tuheshimike kupitia RSTGA...mimi na marehemu John Mwakangale ndio tuliokuwa waanzilishi wa umoja huu na hatutaki kuona ukifa kwa sababu ya wawekezaji wanaotaka kutuvuruga, ndiyo maana wakulima wa Nsoso, Lupata na Kabembe wamegoma kudanganywa" anasema Mwakywaja.
 Ili kuondoa malalamiko ya wakulima hao, Desemba 19, 2010; Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania, Anne Makinda, ambaye ni Spika wa Bunge la Muungano alifika Rungwe na kuelezea kile ambacho wakulima wanadai kuingiliwa na METL katika umoja wao hali ambayo imezusha mtafaruku.
 Katika jitihada za kumaliza mtafaruku huo wa kibiashara na kuurejeshea umoja huo matumaini makubwa ya kuendeleza zao hilo kwa lengo la kukuza uchumi, Makinda anasema pamoja na sababu nyinginezo za kushuka uzalishaji wa zao hilo, wapiganapo mafahari wawili nyasi huumia, hivyo ni wakulima wadogo wanaoumia.
"Zao la chai lipo kwa mujibu wa sheria hivyo bodi na wadau wote wana wajibu wa kufuata sheria na kanuni za zao hilo, mkuu wa wWilaya waite wale wote wanaowapotosha wakulima wadogo kuwaonya kutokuendeleza tabia na vitendo hivyo" anasema Makinda.
 Mkuu wa Wilaya ya Rungwe (DC), Jackson Msome, alipohojiwa kuhusuhali hiyo ili kuweza kurudisha mori ya wakulima, kulima kwa bidii na kuachana na misuguano mibaya ya kibiashara, anaweka wazi ukweli kwa kudai kuwa kufutwa kwa RUTECO ndiko kumeleta chokochoko na kwenda kujiunga na METL kwa lengo la kuingilia ununuzi wa zao la chai kwa wakulima wadogo bila kuwa na kibali.
 Msome anasema wakulima wanajitahidi, ila tatizo ni wanachama wa RUTECO ambao idadi yao haizidi 1,000 wanaotaka kuwayumbisha wakulima zaidi ya 14,000 waliopo kwenye umoja wao,kwa kumsaidia METL, hali ambayo inashughulikiwa ili kuhakikisha umoja huo unalindwa na serikali na wakulima wananufaika na kilimo cha chai.
"Mohamed Enterprises alituandikia barua ya kutaka RUTECO awe wakala wake huku ushirika huo ukiwa na ugomvi na mrajisi baada ya kuona hivyo akaandika barua nyingine ya kuomba kununua chai...sisi hatujamkatalia wala kumkubalia, tumemuagiza kuwa ni vema akakamilisha malengo yake ya kuboresha na kufufua mashamba yake kuliko kujiingiza kwenye ununuzi wa majani mabichi kutoka kwa wakulima" anasema DC Msome.
 Tanzania Daima ilifanikiwa kupata barua yenye kumb. namba Metl/AD/THO/09/02 ya Desemba 10, 2010 ya kuomba kibali cha kununua majani mabichi kutoka kwa wakulima wadogo, pamoja na kukataliwa kwa masharti yaliyotolewa na Kamati ya Ununuzi wa mazao ya biashara Rungwe, METL amekuwa akinunua majani kwa wakulima.
 Tanzania Daima ilipowailiana na Mkurugenzi wa Kampuni wa METL, Gulam Dewji, alidai kuwa yupo kwenye kikao na kutaka suala hilo lizungumziwe na mtendaji wao mwingine aliyemtaja kwa jina la George Mwamakula, ambaye simu yake haikuweza kupatikana.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

NDEJEMBI KUTOKA MFANYAKAZI WA GSM HADI KUWA MAKAMU WA RAIS