NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Asha - Rose Migoro, anaelezwa kuwa sababu ya Rais Jakaya Kikwete kuchelewa kufanya mabadiliko katika Baraza lake jipya la Mawaziri, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Vyanzo vya habari kutoka serikalini vilisema kuwa Migiro ambaye ameomba kupumzika kuendelea na majukumu ya umoja huo kuanzia Juni mwaka huu ni mmoja kati ya watu wanaotegemewa na Rais Kikwete kuongoza moja ya wizara nyeti nchini.
“Rais kwa sasa yuko tayari kufanya mabadiliko kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mawaziri wake wamechoka, wengine ni wagonjwa na wengine wanafikiria urais mwaka 2015. Kinachochelewesha mabadiliko hayo ni ujio wa Mama Migiro kwani hataki kufanya mabadiliko sasa, baada ya mwezi mmoja apangue tena kwa ajili ya kumuingiza Migiro,” kilisema chanzo chetu cha uhakika cha habari.
Sababu nyingine inayotajwa kucheleweshwa kwa mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ni pamoja na kauli za shinikizo zinazotolewa na watu wa kada mbalimbali wakimtaka rais apangue baraza lake ili kumg’oa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Lucy Nkya, kutokana na mgomo wa madaktari uliosababisha vifo vya Watanzania wengi.
Mbali na mawaziri hao, Rais Kikwete pia amekuwa akipata shinikizo la kuwaengua katika baraza lake mawaziri wanaougua kwa muda mrefu, akiwamo Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya.
“Rais Kikwete hawezi kufanya mabadiliko hayo kwa sasa kwani akifanya hivyo ataonekana amefanya kutokana na shinikizo. Kwa vyovyote vile madiliko hayatakuwepo kwa sasa hadi Juni baada ya kurejea Mama Migiro,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Hata hivyo haikuweza kujulikana mara moja Migiro atashika wizara gani, lakini habari zinasema kuwa ataongoza moja ya wizara nyeti nchini.
Wakati akiondoka nchini kwenda kushika nafasi hiyo UN, Migiro ambaye anatajwa kuwa mmoja wa watu wanaotarajiwa kuwania nafasi ya urais mwaka 2015, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alitangaza mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi ndani ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, ambapo alithibitisha kuwa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Asha- Rose Migiro ameomba kupumzika. Vijar Nambiar ambaye ni Mkuu wa Ofisi yake (Chef de Cabinet), pia anaachia ngazi UN.
“Kama mlivyotangaziwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa katika nafasi za watendaji waandamizi, ningependa kuongezea na kuwajulisha kwamba, Naibu Katibu Mkuu, Migiro na Vijar Nambiar wamewasilisha kwangu maombi yao ya kutaka kuachia nafasi zao, ili kuniruhusu kuunda timu mpya ya maofisa waandamizi nitakaofanya nao kazi katika awamu ya pili ya uongozi wangu,” alisema Ban Ki Moon.
Katibu Mkuu huyo alimpongeza Migiro kwa ushirikiano mkubwa na usio na shaka wala doa aliompa katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita akiwa msaidizi wake wa karibu.
“Amenipatia ushirikiano mzuri sana, alinishauri kwa busara na amejituma sana na kwa kuadilifu mkubwa katika kukabiliana na changamoto nyingi zilizoikabili taasisi hii wakati wa awamu yangu ya kwanza ya uongozi,” alisisitiza Ban Ki Moon.
Hata hivyo alisema Migiro ataendelea kuwapo ofisini hadi Juni mwaka huu ili kuratibu na kusimamia kipindi cha mpito pamoja na maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (RIO+20).
Pamoja na Migiro kuwasilisha ombi lake, wapo pia baadhi ya watendaji waandamizi ambao nao wameonyesha nia ya kuachia nafasi zao ili kupisha menejimenti mpya.
Watendaji wengine watakaoondoka na ambao wengi wao walikuwa katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Ban ki Moon ni kutoka Idara za Utawala, Maendeleo, Huduma za Mikutano, Habari, Ofisi ya Upokonyaji wa silaha na Mshauri wa Masuala ya Afrika.
Wengine ni wasimamizi wa Idara za Uchumi za Afrika na Ulaya, waratibu wa mifuko ya maendeleo na Idadi ya watu UNDP na UNFPA.
Aidha, wamo pia wawakilishi maalumu wa katibu mkuu wanaohusika na masuala ya watoto katika migogoro ya kivita, na uzuiaji wa mauaji ya kimbali, ambao wanatarajiwa kuachia nafasi zao katikati ya mwaka huu.
Mchakato wa kujaza nafasi nane zitakazoachwa wazi katika ngazi za ukatibu mkuu msaidizi (Under-Secretary General) umekwisha anza na ujazaji wa nafasi hizo ambao utakuwa wa uwazi utazingatia sana sifa na uwezo wa mtu, uwiano wa kikanda na jinsia. |
Comments