Spika Makinda anataka kumtoa kafara Jairo?

 Mchanganuo wa matumizi ya fedha zilizoombwa na Jairo kwenye taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kwa ajili  ya kulipa posho kwa watumishi wa wizara na taasisi hizo wakati wa kujadiliwa bajeti ya Nishati na bungeni Dodoma mwaka jana.
Fomu inayoonesha posho walizolipwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja  na Naibu wake, Adam Malima wakati wa Kikakao cha Bunge cha kujadili bajeti ya wizara  hiyo, Dodoma mwaka jana.

WAKATI akiahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma wiki hii, hadi Juni 12 mwaka huu wakati wa kujadili Bajeti ya Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitoa kauli inayotatanisha.

Makinda alisema: "Ndugu zangu wabunge na mawaziri mliosemwa hapa bungeni, msichukie na kufika hatua ya kuumia bure mkanuniana... haya yaliyosemwa hapa ni maneno tu na yameishia hapahapa. Msiendelee kuyawaza sana wakati mwingine hata waliowasema wameshaondoka na hata hawayakumbuki."

"Yaliyojadiliwa yote ni kwa nia njema. Isiwe kiini cha chuki na uhasama. Msibebe chuki ndani ya roho zenu. Msichukue hasira mpaka mkapasuka mifupa. Mnaambiwa namna ya kufanya kazi vizuri. Mkichukulia kwamba ni uadui, mtapata shida," alisema Makinda na kusisitiza juu ya dhana nzima ya cheo ni dhamana kwa kuongeza: "Kama husemwi wamseme nani na wewe ni Waziri?"

Kauli hii ya Spika ambaye ni kiongozi mkuu wa Bunge inadhihirisha kwamba wabunge wetu ni wapiga porojo tu wawapo 'mjengoni'.

Spika akataa ripoti ya Jairo

Mantiki ya kuweka utangulizi wa kauli hiyo ya Spika Makinda katika uchambuzi wangu ni kutokana na kukataa taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Bunge juu ya tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa, David Jairo.

Taarifa hiyo ambayo ilikuwa iwasilishwe bungeni juzi na Serikali kwa mujibu wa ratiba, lakini haikuwasilishwa na Makinda aliliambia Bunge kuwa alilazimika kuikataa kwa madai kwamba majibu ya Serikali hayakumridhisha akidai haikidhi matakwa ya Bunge.

Ripoti hiyo ilitarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa Jumatatu, baada ya Jairo kuingia katika kashfa wizara yake ilipowasilisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 iliyoibuliwa na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, aliyedai alichangisha sh. bilioni moja kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya wizara yake ili kusaidia kupitishwa kwa bajeti hiyo.

Baada ya wabunge kutoa madai hayo, Serikali ilichunguza suala hilo kupitia ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh aliyebaini fedha zilizokusanywa hazikuwa kiasi hicho.

Uamuzi huo wa CAG ulitangazwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuwa Jairo hakuwa na makosa na akamwamuru arejee kazini kwa vile hakuna sehemu ambayo alivunja taratibu za kazi.

Kamati Teule

Hali hiyo iliwaudhi wabunge waliolazimika kuunda Kamati Teule ya Bunge ambayo katika uchunguzi wake ilimtia hatiani Jairo, hivyo wakataka Serikali ichukue hatua za kinidhamu juu ya mtumishi huyo wa umma.

Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza sakata la Jairo iliongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Mhandisi Ramo Makani (CCM), ilikuwa na hadidu za rejea tano zilizotakiwa kufanyiwa kazi.

Wajumbe wengine katika kamati hiyo walikuwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Umbula, Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF) na Mbunge wa Karagwe, Godbless Blandesi.

Majibu ya Makinda yalikuja baada ya Mbunge wa Karatu, Israel Natse(Chadema) kuomba mwongozo wa Spika na kuhoji ni kwa nini suala la Jairo liliondolewa katika orodha.

Mchungaji Natse aliyekuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati iliyoundwa kuchunguza sakata la Jairo kuhusu kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwezesha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, alionesha kukerwa na kitendo cha kuondoa kwenye orodha taarifa hiyo.

Spika Makinda alidai kuondoa ripoti hiyo ni kutokana na kutokamilika kama ilivyokusudiwa, hivyo akadai upungufu huo hauwezeshi wala haumshawishi kuruhusu itolewe mbele ya Bunge.

Kauli hiyo ya Makinda ndiyo imenipa msukumo wa kuandika uchambuzi kuonesha kuwa kuna walakini katika kushughulia suala hilo, na inadhihirisha kuwa ama wabunge au Spika wanataka kumtoa kafara Jairo!

Spika Makinda angefanya jambo la busara endapo angeipokea taarifa hiyo na kuisoma kwa wabunge ili kwa pamoja watambue ni upungufu gani uliomo, na si kukurupuka peke yake kudai kuwa ina walakini!

Ikumbukwe kuwa katika orodha ya fomu ya malipo kwa viongozi wa Bunge kuhusu semina ya wabunge ya sekta ya umeme nchini Juni 26, 2011 inaonesha jina la Spika Makinda akiwa miongoni mwa waliosaini kuchukua fedha zilizokusanywa na Jairo sh. 280,000, likiwamo pia ya Waziri Mkuu, Pinda.

Mpango uliosukwa

Lakini inaonesha kinachomtokea Jairo ni matokeo ya mpango uliosukwa tangu awali kwa lengo la kumuondoa madarakani kutokana na kuwaminyia ulaji baadhi ya viongozi wakiwemo wa kisiasa ambao walitaka kuitumia sekta ya nishati na madini kwa maslahi yao.

Mwanasheria nguli nchini, Dk. Masumbuko Lamwai aliwahi kukaririwa na Jambo Leo akisema kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatakiwa kuelewa kuwa kazi yake ni kutunga sheria na si kuongoza nchi, kwani dhamama ya uongozi wa nchi iko chini ya rais.

Dk. Lamwai alitoa kauli hiyo kuhusu utaratibu uliofanywa na Bunge katika kuchunguza tuhuma zinazomkabili Jairo.

Alisema yeye kama mwanasheria mwandamizi na aliyebobea, analoliona Bunge la Tanzania kutokuwa na uelewa wa kisheria, badala yake kufanya kazi ambazo kisheria ni kukiuka katiba ya nchi na taratibu za utawala bora.

Alisema Bunge lilikaa kama Mahakama ya Rufaa na kusikiliza kesi ya Jairo kisha kutoa hukumu kuwa ana hatia, mamlaka ambayo kikatiba na kisheria ni kuingilia mhimili wa Mahakama.

Bunge lilitumia ubabe

Niliwahi kueleza katika makala zangu siku za nyuma kwamba Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni, iliwasilisha taarifa yake huku ikiwakangaa Jairo na Luhanjo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Injinia Makani, aliliambia Bunge kuwa wengine wanaopaswa kuwajibishwa ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Naibu wake, Adam Malima na CAG, Utouh.

Fomu ya posho ya kujikimu inaonesha pia Waziri Ngeleja na Naibu wake, Malima kila mmoja alisaini kupokea sh. milioni 8 zilizokusanywa na Jairo.

Makani alisema baada ya kufanya uchunguzi wake uliowezesha kuwahoji watu 146, ilibainika kuwa utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kusaidia upitishaji wa bajeti bungeni, haukuwa wa kawaida na kwamba ulikiuka taratibu na sheria za fedha.

Hata hivyo, uchunguzi unaonesha utaratibu huo wa wizara kukusanya fedha kwa taasisi zake ni mfumo uliokuwepo tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Nasema hivyo kwa sababu ushahidi unaonesha kabla ya Jairo, Juni 19, 2009, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi aliwahi kuandika barua kama ya Jairo ya maombi ya fehda kwa taasisi ili kuwezesha uwasilishwaji wa hotuba ya bajeti ya mwaka 2009/10 bungeni Dodoma.

"Fedha zilizokusanywa zilikuwa kwa matumizi ambayo yasingehitaji uchangishaji kwa sababu yangeweza kugharamiwa na kasma zilizopo za wizara.

"Uchangishaji huo ulisababisha taasisi hizo kubebeshwa mzigo kwa kuwa hazina kasma mahususi kwa ajili ya kuchangia wizara kwa ajili ya maandalizi ya uwasilishaji wa bajeti bungeni," alisema Makani.

Alisema utafiti ulibaini kwamba Jairo akiwa Katibu Mkuu, aliomba fedha kiasi cha sh. milioni 180 kutoka taasisi nne ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililoombwa sh. milioni 40, Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) sh. milioni 40, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) sh. milioni 50 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) sh. milioni 50.

Hata hivyo, kiasi kilichochangwa ni sh. milioni 140 tu kutoka Tanesco, REA na TPDC wakati Ewura waligharamia chakula cha mchana wa siku tatu pamoja na tafrija iliyokuwa imepangwa kufanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti ambayo iliwagharimu sh. milioni 9.7.

Makani aliongeza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuwa mbali na fedha hizo, kulikuwa na kiasi kingine cha sh. milioni 428.8 kilichotoka katika idara mbili za wizara hiyo ambazo ni Idara ya Uhasibu sh. milioni 150.7 na Idara ya Sera na Mipango iliyotoa sh. milioni 278 kwa ajili ya kusaidia upitishaji wa bajeti.

Alisema fedha zote hizo jumla yake ikiwa sh. milioni 568.8, ziliingizwa kwenye akaunti ya taasisi ya GST iliyopo mjini Dodoma, lakini akasema kati ya hizo, sh. milioni 150.7 zilikuwa kwa ajili ya gharama za vikao na semina na kiasi kilichokuwa mahususi kwa ajili ya uwasilishaji wa bajeti bungeni kilikuwa ni sh. milioni 418.8.

Makani alibainisha kuwa maelezo waliyopewa na wizara husika, walifikia uamuzi wa kuomba fedha hizo kutokana na fungu ambalo hutumika kwa ajili ya shughuli za bajeti kubakiwa na sh. milioni 35 tu kati ya sh. milioni 207 zilizokuwa zikihitajika.

Hata hivyo, alisema wizara haikuzingatia kanuni husika za fedha katika kuomba fedha hizo, na kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo alipohojiwa na kamati hiyo, alisema utaratibu uliotumiwa si halali.

"Sababu zilizoifanya Wizara kuchangisha fedha haziwezi kutiliwa maanani kwa sababu hadi kufikia Juni 25, 2011 Wizara ya Nishati na Madini ilikwishapata mahitaji yote ya fedha za uwasilishaji wa bajeti baada ya kupokea sh. milioni 171.5 za matumizi mengineyo (OC) kutoka hazina," alisema Makani.

Mkono alionya

Ndiyo maana wakati wa mjadala wa awali kuhusu Jairo, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM) alipinga uamuzi huo kwa kuliambia Bunge linakwenda nje ya mipaka kwa kuingilia taratibu za mihimili mingine kwa kumhukumu Jairo tena bila kumpa nafasi ya kujitetea!

Katika mgawanyo wa madaraka, Bunge linatakiwa kutambua kazi yake ni kutunga sheria, Mahakama ni kuzitafsiri na Utawala (Serikali) ina jukumu la kuzisimamia! Kwanini Bunge lisiheshimu utawala wa sheria? Kinachofanyika, Bunge linataka kujitwika mamlaka ya kuajiri na kufukuza watumishi serikalini, ndiyo maana wanatishia kwamba eti kama Jairo anarejeshwa kazini, basi Pinda ajiuzulu! Si sahihi.

Athari za Bunge kuingilia kazi zisizo zake tumezishuhudia mara kadhaa nchini. Wabunge walijifanya ni wataalamu wa masuala ya umeme, wakashinikiza mitambo isinunuliwe au uwekezaji usifanyike kwa ushauri wa Bunge, wakasema bora nchi iingie gizani kuliko kuwasha mitambo ya Dowans ambayo sasa imewashwa kwa gharama baada ya kutofanya kazi kwa miaka mitatu!

Wabunge hawana budi kuheshimu watalaamu na mihimili mingine na kila chombo kifanye kazi yake badala ya kutafuta umaarufu usio na manufaa kwa Taifa.

Kinachofanywa na wabunge ni kituko kwa mtazamo wangu... Iliundwa tume ambayo tayari ilikuwa na majibu. Katika kikao cha Bunge kilichofikia tamati juzi, wabunge walitumia ripoti ya CAG kuwabana mawaziri... hapo ripoti yake inaaminika. Kwa nini alipotoa ripoti ya Jairo hakuaminika? Mbona taarifa zake zote hazijawahi kukataliwa na Bunge? Kwa nini hii ya Jairo?

Kinachoonekana ni kwamba Jairo tayari alikuwa amehukumiwa na wabunge hata kabla ya kesi yake kusikilizwa kwa haki. Binafsi nakosa imani na Tume iliyoundwa na Bunge kwa sababu wao walikwishamhukumu mapema kabla ya kesi yake.

Kwa hili hapana!

Katika uchambuzi wangu siku zilizopita, hasa lilipoibuka sakata hili la Jairo, niliwahi kuandika kwamba: 'Wabunge mnataka mtuhumu, mchunguze, mwendeshe kesi, mtoe hukumu... hapana!

Narudia kusema kwamba, waliofuatilia vikao vya Bunge vilivyomalizika mjini Dodoma, hapana shaka watakubaliana nami kwamba Bunge sasa limegeuka kuwa uwanja wa kuwashambulia na kuwasulubu watu ama walio au wasiokuwa wabunge.

Ninachokiona ni kwamba sasa wabunge wanakigeuza chombo hicho kuwa cha kuwaonea na kuwakandamiza watu walio nje ya Bunge, badala ya kulinda na kutetea haki za watu, hususan wanyonge wasio na sauti.

Ingawa Katiba ya Tanzania inawapa kinga wabunge ya kutoshtakiwa kwa makosa ya jinai au madai ya mambo wanayoyasema bungeni, kwa lengo la kulinda uhuru wa majadiliano ya Bunge, lakini kinga na uhuru huo haviwezi kuwa nyenzo ya kuwadhalilisha watu wengine.

Nashangazwa na hatua ya Bunge kuvuruga sheria za nchi na Katiba ambayo inampa haki zake za msingi  kila Mtanzania akiwemo Jairo.

Wabunge wamefikia hatua ya kujibinafisisha madaraka ambayo hawatakiwi kuwa nayo yakiwemo ya kuchunguza, kuendesha mashtaka na kuhukumu, kazi zinazotakiwa kufanywa na Polisi, Mahakama na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

Haiwezekani tuhuma ikaibuliwa bungeni na wabunge hao hao wakafanya kazi ya kuchunguza na baadaye kutoa hukumu. Kauli ya Spika Makinda inadhihirisha wabunge wanata Jairo 'anyongwe'.

Naamini wabunge wamekuwa wakitumia vibaya upendeleo huo wa kisheria, hali inayotia shaka kuhusu uhuru na kinga hiyo ya Bunge unaoonesha uonevu wa dhahiri kwa wanyonge.

Na sasa inaonesha dhambi hiyo ya kuwaonea walio nje ya Bunge, imeanza kuwageuka na sasa wanataka kutafunana wao kwa wao, ndiyo maana katika kikao cha Bunge kilichofikia tamati juzi, uliibuka msuguano uliotia shinikizo la kutaka baadhi ya mawaziri wajiuzulu kwa madai ya utendaji kazi wao usioridhisha.

Katibu wa Wabunge wa CCM ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa walikubaliana kwamba kikao cha wabunge wa CCM kilifikia uamuzi wa kuwashinikiza mawaziri nane kujiuzulu, na kwamba ungetolewa na Mwenyekiti wa wabunge wa chama hicho ambaye ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Pinda alikaririwa awali akisema kuwa angezungumzia mustakabali wa mawaziri hao Jumatatu, kwa vile alikuwa hajapokea barua yoyote ya waziri aliyejiuzulu.

Mawaziri waliotajwa kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Uchukuzi, Nundu, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Mkuchika.

Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Cyril Chami na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe.

Lakini uchunguzi unaonesha kuwa sehemu kubwa ya tuhuma zinazotolewa kwa mawaziri hao kwa mujibu wa ripoti za kamati za kudumu za Bunge, ni kutokana na chuki binafsi, mgongano wa maslahi na vyeo.

Sasa wanageukana!

Kwa mfano, Waziri wa Uchukuzi, Nundu, alilazimika kumwaga 'mboga' baada ya baadhi ya wabunge kumtuhumu kwamba amefuja fedha za umma. Ni dhahiri kuwa baadhi ya ripoti zinazotolewa na kamati za Bunge zimejaa walakini na watu kukomoana!

Waziri Nundu aliamua kumtwisha mzigo Naibu Waziri wake, Dk. Athuman Mfutakamba, kuwa ndiye aliyeshinikiza Kampuni ya China Communication Construction (CCC) kujenga gati namba 13 na 14 baada ya kugharimiwa safari nje ya nchi bila idhini yake!

Lakini inavyoonesha, Waziri Nundu anataka kutolewa kafara katika hili kwa sababu ya msimamo wake kuhusu CCC kwamba wasipewe tenda ya kujenga gati hizo kwa sababu zingeigharimu Serikali.

Mbali na mvutano wa Nundu na Mfuatakamba, katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Biashara pia kumeibua mambo mazito yanayoonesha kuwa Waziri, Dk. Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu hawapikiki chungu kimoja.

Nyalandu alifichua waraka wake uliombebesha mzigo Dk. Chami katika sakata la kumwajibisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege.

Waraka huo unaonesha kuwa Nyalandu alimshauri Dk. Chami amsimamishe kazi Ekelege kupisha uchunguzi wa CAG kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, lakini waziri hakuchukua hatua, hivyo kutafsiriwa kuwa alikuwa anamkingia kifua.

Waziri Chami alijitetea kuwa hakufanya hivyo kwa sababu Ekelege ni mteule wa rais, hivyo hakuwa na mamlaka ya kumsimamisha kazi; ingawa hakueleza kama alimshauri rais kuhusu hatua sahihi za kuchukua dhidi ya Mkurugenzi Mkuu huyo wa TBS.

Si kwamba nawatetea mawaziri wanaotuhumiwa, lakini isionekane dhahiri kuwa wanaundiwa vikundi vya hujuma ili waumizwe bila makosa.

Nasema hivyo kwa sababu wabunge wanaonesha wanataka kuligeuza Bunge kuwa mahali pa kumalizia hasira zao binafsi dhidi ya watu waliowakosea ndani na nje ya Bunge, wanalitumia Bunge kuwakomoa mahasimu wao, kinyume cha malengo ya kuchaguliwa kwao.

Wabunge wanafedhehesha kwa vile wanaonesha matumizi mabaya ya kinga na uhuru waliopewa, wanadiriki kuwashambulia na kuwahukumu watu wengi tu walio nje ya Bunge.

Ikumbukwe kuwa si kila linalosemwa na mbunge bungeni ni la kweli, kuna mambo mengi ya uongo yanasemwa na wabunge wanapozungumza 'mjengoni', wakilenga ama kuwafurahisha wapiga kura wao au watu wengine wanaowatumia kwa maslahi yao binafsi.

Tangu mwanzo wa suala la Jairo lilipoibuka bungeni, niliandika uchambuzi kwamba hana hatia kwa vile alitimiza wajibu wake, na ndicho CAG alichothibitisha, lakini nikashangaa wabunge wanamshupalia huku wakiungwa mkono na baadhi ya wana-habari.

Niliwahi kuandika kwamba inaonesha nchi hii itaangamizwa na watu wa aina mbili, wanasiasa na vyombo vya habari kwa sababu hakuna uchunguzi makini na upembuzi yakinifu, watu wanayugayuga (hangaika huku na huku) ilimradi siku zinapita.

Swali la kujiuliza, kama CAG aliyemchunguza Jairo alikuta hakuna makosa, wabunge wanadai kuna makosa, wanalazimisha kwa kutaka Jairo ashtakiwe, achukuliwe hatua, kwa kosa lipi? Kavunja sheria ipi?

Tukiendekeza haya mambo ya kila mtu akitoa tuhuma, fulani afukuzwe kazi tu kwa hisia, watafukuzwa wengi kwa kuonewa. Nimegundua nchi hii uzushi unatawala kuliko ukweli.

Jairo alisimamishwa na mkuu wake wa kazi, Luhanjo, na kwa niaba ya kupata ukweli akaamuru CAG afanye uchunguzi. Taarifa ya kumsimamisha na kumchunguza ilitolewa mbele ya waandishi, wabunge wanashupalia eti wapelekewe wao, kwani wao ndiyo walimtuma?

Uchunguzi ulipokamilika taarifa alipewa aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi, baada ya kuipitia akaamua kuitoa au kutangaza matokeo kwa waandishi, wabunge wakahamaki na kutaka ripoti hiyo ipelekwe kwao wao ndiyo waijadili, ina maana wao ndiyo waliamuru Jairo achunguzwe?

Ndiyo maana hata ripoti ya Kamati Teule ilimkandamiza, kwa vile tayari walikwishamhukumu, na waliounda kamati wasingeweza kwenda kinyume cha matakwa ya wabunge, lazima wangewalinda wenzao kama walivyofanya! Ndivyo anavyotaka kufanya Spika Makinda.

Wabunge wanadhani wao ni 'superior', wanatuhumu, wanataka wachunguze, waendeshe kesi na watoe hukumu, wanataka wawe mawakili wa utawala wa sheria na kanuni ... hii ni hatari.

Bunge letu linataka kuwa Mahakama. Kwa hili la Jairo (anayetafutwa zaidi), Bunge linavunja utaratibu wa kikatiba.Awali, Bunge lilitoa hukumu hata kabla ya kuundwa kwa Kamati Teule ya uchunguzi. Serikali ilitekeleza utaratibu wake, wabunge wakalalamika kwamba Bunge limedharauliwa! Kwanini walitaka Jairo akutane na wabunge ilhali yeye si mwanasiasia kama wao?

Ndiyo maana nasema Bunge linafanya ubabe, hasa ukirejea nukuu ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba: "Kama ni dharau zenu fanyeni huko huko, si hapa bungeni'! Hiyo tayari ni hukumu tosha.

Uonevu kwa Jairo ni kumtuhumu na kumhukumu, wakati mamlaka yake ya nidhamu ilimuondolea tuhuma zilizotolewa awali. Pia wakati wa mjadala husika, alionekana kwamba anapaswa kuondolewa kazini... tayari hapo ni hukumu bila hata uchunguzi.

Wabunge watambue kwamba wanatakiwa kushauri na kusimamia utendaji mzuri wa kufuata sheria na kanuni na si jazba na chuki! Walichokifanya wabunge wanataka kujihakikishia jinsi ya kurudi 'mjengoni' mwaka 2015. Hii ni vita ya ubinafsi.


Willy Edward ni Mhariri Mkuu Jambo Leo. 0786-294384 /

0655-294384 / 0763-394384.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI

π—₯π—”π—§π—œπ—•π—” 𝗬𝗔 π—¬π—”π—‘π—šπ—” 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—™π—¨π—‘π—šπ—” 𝗠π—ͺπ—”π—žπ—” 2024 πŸ”°

MONGELLA AWATEMBELEA HOSPITALI WALIOMWAGIWA TINDIKALI

GERSON MSIGWA AREJESHWA KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

AUCHO, BACCA, BOKA WAJUMUISHWA KWENDA ALGERIA LEO