WAKULIMA WA MPUNGA WATAKIWA KUTUMIA MBEGU BORA ILIYOFANYIWA UTAFITI NA TARI

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Uyole na Mtafiti wa zao la mpunga Dkt. Denis Tippe (mwenye fulana ya kijani) akitoa elimu kwa wakulima kuhusiana na mbegu mpya za zao la mpunga wakati wa maonyesho ya mpunga.Mtafiti Veronica Twisa kutoka Kituo cha TARI Uyole akitoa maelezo kwa wadau waliotebelea maonesho ya mpunga kilimo biashara Wilayani Mbarali.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI katika maonesho ya Mpunga Kilimo Biashara Wilayani Mbarali Dkt. Richard Kasuga.


Na Evelyne Mpasha, MBARALI

Wakulima wa zao la mpunga  wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wametakiwa kuongeza matumizi ya mbegu bora zilizotafitiwa na Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa  Kilimo Tanzania (TARI) ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mpunga na kuachana na kilimo cha mazoea ambacho tija yake ni ndogo.

Wito huo umetolewa  Julai 2, 2022) na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wilaya ya Mbarali Bwana Geoffrey Mwaijobele wakati akifungua maonesho ya Kilimo Biashara cha Mpunga yaliyoandaliwa na Kituo cha TARI Uyole kwa kushirikiana na Vituo vya TARI Dakawa na TARI Ifakara pamoja na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Mpunga (IRRI). Maonesho hayo yamefanyika katika Kata ya Ubaruku Wilayani Mbarali iliyoko mkoa wa Mbeya.

Katika hotuba yake, Mwaijobele ameipongeza TARI kwa  kuleta matokeo ya utafiti wa zao la Mpunga  karibu na wananchi hususan katika Wilaya ya Mbarali na kutoa elimu kwa wakulima. 

Elimu iliyotolewa katika maonesho ya kilimo biashara cha mpunga ni pamoja na  sifa za mbegu mpya za mpunga, maandalizi ya shamba, matumizi bora ya mbolea, palizi na hatua za uvunaji hatua ambayo itasaidia wakulima wa Wilaya ya Mbarali na maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo cha mpunga kulima kisasa, kuwa na uhakika wa chakula na ziada ya kuuza kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla .

Awali,  Kaimu Mkurugenzi  wa Kituo cha TARI Uyole ambaye Dkt. Denis Tippe alieleza kuwa Kituo cha TARI Uyole kiliweka majaribio ya mbegu mpya sita katika skimu ya umwagiliaji Kata ya Ubaruku Wilayani Mbarali ili kuongeza matumizi ya mbegu bora za mpunga  na kuliongezea tija baada ya kubaini changamoto iliyopo ya kushuka kwa tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Dkt. Tippe aliongeza kuwa mbegu hizo mpya za mpunga za SARO 5, TARI RIC 1 & 2, Komboka, SATO 1 & 9 ambazo zina sifa za kutoa mavuno mengi kuanzia tani 7.5 hadi 8.5 kwa hekta, kunukia, kuwa na punje nzuri, kukomaa kwa muda mfupi  na baadhi zinavumilia maeneo  yaliyoathiriwa na magadi na chumvi chumvi zimeonyesha kufanya vizuri katika majaribio yaliyoandaliwa kwa ajili ya maonesho hayo  ambayo yanalenga mkusaidia mkulima kuchagua mbegu ambayo itamfaa kulingana na eneo lake.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI aliyehudhuria maonesho hayo Dkt. Richard Kasuga amesema maonesho hayo ni moja moja ya majukumu muhimu ya TARI ya kuhakikisha  teknolojia zinazotafitiwa zinawafikia wakulima na wadau wa kilimo kupitia njia mbalimbali  za mawasiliano ikiwemo  maonesho ya kilimo biashara, vituo mahiri, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Aliongoeza kuwa matumizi ya mbegu bora za mpunga zitasaidia kuongeza uzalishaji na hivyo kufikia malengo ya Serikali ya kujitosheleza kwa chakula na pia Malengo ya yaliyoainishwa katika Azimio la Malabo la kukabilana na njaa. 

Akizungumzia kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kasuga ameongeza kuwa katika mwaka wa 2022/2023 bajeti ya maendeleo ya utafiti imeongezeka kutoka takriban bilioni 11 hadi billion 41. 

Ameongeza kuwa, Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe ameweka mkazo na malengo ya AJENDA 10/30 yenye kaulimbiu KILIMO NI BIASHARA yenye lengo la kujitosheleza kwa chakula na ziada kwa ajili ya kuuza na kujiongezea kipato, Hivyo maonesho haya ni fursa katika kuwahamasisha wakulima kutumia fursa za masoko ambalo Wizara imeendelea kuyatafuta ikiwemo la Ubeljiji kwa ajili ya kuuza mchele.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wakulima wa zao la mpunga Wilayani Mbarali wameipongeza na kuishukuru TARI kwa kuwezesha kuweka majaribio ya mbegu mpya za mpunga Wilayani humo na kuuomba Uongozi wa Wilaya ya Mbarali kuwaletea wataalamu wa TARI  karibu yao ili waweze kuwasaidia kuwapimia afya ya udongo na kuwapa  elimu zadi ya matumizi ya mbegu mpya, matumizi sahihi ya udongo pamoja na ushauri ili waweze kupata tija zaidi katika kilimo chao ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika wa uwepo wa mbegu hizo Wilayani Mbarali.

Wakulima hao wameeleza kuwa muda wote walikuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakikuwa na tija kwani walikuwa wakipata gunia 8 -10 kwa ekari moja, lakini sasa wanataka kubadilika na  kutumia mbegu mpya za TARI ambazo humuwezesha mkulima kupata  kati ya gunia 30 - 40 kwa ekari moja.

Wakulima waliohudhuria maonesho hayo ya Mpunga Kilimo Biashara wametoka katika vijiji vya Ubaruku, Kapunga, Madibila, Uturo na Buyuni Wilayani Mbarali.
Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

NG'OMBE 'KIKWETE' AWA KIVUTIO MAONESHO YA NANE NANE DODOMA

HIZI NDIO DALILI ZA VVU KWA WATOTO WADOGO

DUWASA IMEJIPANGA VILIVYO KUHUDUMIA WANANCHI MAONESHO YA NANE NANE NZUGUNI DODOMA+video

GLOBAL DISCUSSION TOPIC ON: GLOBAL GREEN ECONOMIIE VS GLOBAL ENERGY SHORTAGE

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

RC MTAKA: KARIBUNI NJOMBE MWANDAE PENSHENI ZENU KWA KUPANDA MITI, PARACHICHI

MATOKEO YA DARASA LA SABA 2013 YATOKA, YAPO HAPA ... YAONE HAPA KWA NJIA RAHISI KABISA

REKODI YA SIMBA NA YANGA TANGU MWAKA 2010

RC SENYAMULE ATAMANII DODOMA IWE NA MUONEKANO WA KIMATAIFA+video

MAKAMU WA RAIS, DKT MPANGO AZINDUA MITAMBO YA KISASA YA UCHORONGAJI YA STAMICO