DK NCHIMBI ATAKA MATUKIO YA UKATILI MBARALI YAKOMESHWE

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisikiliza kero kutoka kwa wananchi na kuzitafutia ufumbuzi katika mkutano wa hadhara katika Mji wa Ubaruku, Rujewa wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya  wakati wa muendelezo wa  ziara ya siku 10 katika mikoa 6 nchini.


PICHA NA RICHARD MWAIKENDA




 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewakosha wananchi wa Mbarali, alivyowaruhusu wawasilishe kero zao kwa njia ya maswali na yeye kuyajibu papo kwa papo kwenye mkutano wa hadhara, na kutoa maelekezo kwa Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali, kwa ajili ya hatua mbalimbali za kutatua na kuzimaliza. 


Kuhusu utatuzi wa mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Ruaha, ambayo iko chini ya TANAPA, Dk. Nchimbi ameelekeza Wizara ya Ardhi, kuhakikisha wataalam wa upimaji ardhi wanafika Mbarali mara moja kujiridhisha juu ya migogoro ya mipaka kwa wananchi dhidi ya taasisi za kiserikali.


Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara baada ya kusimama kuwasalimia wananchi wa Mbarali, katika Kata ya Ubaruku, pia amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, kwa pamoja, kuhakikisha wanasimamia na kufuatalia juu ya tuhuma za baadhi ya askari wa uhifadhi (TANAPA) kutumia nguvu zinazoumiza na kutweza utu wa binadamu.


Amewataka kuhakikisha matukio ya ukatili yanapingwa, kukemewa na kukomeshwa, baada ya kupokea kero zilizodai na kuwatuhumu baadhi ya askari wa TANAPA wanawapiga risasi wananchi, hasa vijana wanaokwenda kuvua samaki kukatiza kwenye maeneo yasiyo njia rasmi.


Aidha, Dk Nchimbi alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kusimamia na kuhakikisha watu wanapewa elimu ya kutosha na kuoneshwa maeneo sahihi ya njia za kupita wakati wakienda kwenye shughuli zao za kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.


Kuhusu kero iliyodai kuwepo kwa vitendo vya kuwatoza wakulima kwa mazao yaliyoko shambani, amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbarali kuishughulikia na kuimaliza ili wananchi wasihangaishwe. 


Dk. Nchimbi amuelekeza Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, kuanza mazungumzo mara moja na Ndugu Haroun Mulla ambaye ni mmoja wa wawekezaji wakubwa wa sekta ya kilimo katika eneo hilo, akimiliki Kampuni ya Mbarali Estates, aliyekubali kujadiliana kwa ajili ya kuachia shamba moja kwa matumizi ya wananchi wapate mahali pa kulima. 


Aidha, Dk Nchimbi alitumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za upendo za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa kata ya Ubaruku, Wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya walipakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha.


" _Rais Dkt. Samia yupo Nchini Uturuki kikazi lakani amenipa salamu zake niwapatie wananchi wa hapa Ubaraku, anatambua thamani yenu na anawataka kuendelea kuwa na imani na mbunge wenu na CCM kwa ujumla wake_ ."


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI