KATIBU MKUU VIWANDA NA BIASHARA AIAGIZA MENEJIMENTI WMA KUTEKELEZA MAONO YA RAIS SAMIA


๐ŸŸข Akabidhi magari kuboresha utendaji kazi 

๐ŸŸข Azindua Jarida maalum kupanua wigo uhabarishaji umma 

 Veronica Simba – WMA, Pwani 

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia utendaji kazi wenye weledi, ubora na viwango ili kupata matokeo chanya katika sekta ya biashara nchini.

Ameyasema hayo kwa waandishi wa habari Oktoba 3, 2024 Kibaha mkoani Pwani baada ya kufungua rasmi kikao cha Menejimenti ya WMA, kukabidhi magari ili kuboresha utendaji kazi na kuzindua Jarida maalum la Wakala lenye lengo la kupanua wigo wa uelimishaji na uhabarishaji umma kuhusu WMA.

“Lengo kubwa la kikao chetu ni kukumbushana wajibu na dhamira nzima ya majukumu yetu ambayo yanatakiwa yaakisi maelekezo na miongozo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kuwezesha ufanyaji biashara ndani ya nchi yetu.”

Ili kuhakikisha maono hayo ya Rais yanafikiwa, Dkt. Abdallah ameitaka WMA kuzingatia mambo kadhaa ambayo ni pamoja na utii wa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo kwa kuongeza uadilifu na weledi kazini.

Pia amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja na kuwa na kauli moja baina ya Bodi, Mkuu wa Wakala, Menejimenti, Viongozi wa Mikoa pamoja na wafanyakazi wote kwa lengo la kupata matokeo chanya katika kazi.

Vilevile ameielekeza Menejimenti kuondoa urasimu wa aina yoyote katika utendaji kazi huku akisisitiza kwamba Jarida alilozindua pamoja na kutoa habari mbalimbali za Wakala, litumike kama nyenzo ya utoaji taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na wadau wa WMA hususani katika ufanyaji biashara.

Katibu Mkuu amesisitiza Uongozi wa WMA kuzingatia yaliyomo katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja, ambao unaelekeza kutoa huduma bora na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Dkt. Abdallah amempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa sekta mbalimbali za umma na kwa muktadha huo kwa WMA ambapo ametoa jumla ya magari 10 kwa Wakala hiyo ili kuboresha utendaji kazi.

“Leo nimekabidhi magari mawili kwa WMA na mengine Nane yako kwenye mchakato na tutayakabidhi mara moja utakapokamilika. Kwa hili, tuendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais,” amefafanua.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti nzima, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla amesema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu.

Akidadavua kuhusu majukumu ya WMA ambayo ndiyo haswa yaliyotolewa maelekezo kuongeza nguvu, Kihulla amesema ni pamoja na uhakiki wa vipimo, ukaguzi wa vipimo pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa kwa lengo la kukuza uchumi katika sekta mbalimbali.

“Lengo ni kukuza uchumi katika sekta mbalimbali lakini pia kusaidia wananchi wanaonunua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na zinazotoka nje ya nchi, ziwe katika uzito sahihi, ujazo sahihi, urefu sahihi pamoja na namba yaani idadi sahihi.”

Kuhusu magari waliyopokea, Mtendaji Mkuu ameishukuru Wizara na kukiri kuwa yatapunguza changamoto iliyopo lakini akaomba Wakala iendelee kufikiriwa kupatiwa mengine zaidi pamoja na vitendea kazi vingine mbalimbali ili kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi.

Kikao hicho cha Menejimenti ya Wakala wa Vipimo ni utaratibu wa kawaida ambao Wakala umejiwekea ambapo hukutana kila robo ya Mwaka wa Fedha kujadili kuhusu maendeleo ya utendaji kazi na namna ya kuboresha zaidi. Kikao kiliketi kuanzia Oktoba 2, 2024 na kudumu kwa siku tatu ambapo kimejumuisha Menejimenti Kuu kutoka Makao Makuu pamoja na Mameneja wa Mikoa yote Tanzania Bara.




 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

๐— ๐—•๐—ข๐—ช๐—˜ ๐—”๐—ฆ๐—œ๐—ง๐—œ๐—ฆ๐—›๐—” ๐— ๐—”๐—”๐—ก๐——๐—”๐— ๐—”๐—ก๐—ข ๐—ฌ๐—” ๐—–๐—›๐—”๐——๐—˜๐— ๐—” ๐—ฌ๐—” ๐—ง๐—”๐—ฅ๐—˜๐—›๐—˜ ๐Ÿฎ๐Ÿฏ.

KAMATI YA UWT KUTOA MSAADA WA KISHERIA NCHINI

KIKOSI CHA CBE KIMEWASILI ZENJI KUVAANA NA YANGA

YANGA YAWASILI SALAMA ETHIOPIA

MAYELE AIMWAGIA SIFA LUKUKI YANGA