SINTOFAHAMU YA MAUAJI YA KABILA




 KWA miaka kadhaa kumekuwepo sintofahamu ya kile kilichosababisha kuuawa aliyekuwa kiongozi wa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwaka 2001 mjini Kinshasa, LAURENT DESIRE KABILA (61).

ANDIKO hili linatoa picha kamili kuanzia mwanzo wakati Kabila (Baba) akiwa mfanyabiashara nchini humo na kisha kuwa Rais, na kujitokeza Kabila (Mtoto) kurithi madaraka hayo.

Sasa endelea...

Na Lugete Mussa Lugete

HYPPOLITE CHRISTOPHER KANAMBE KAZEMBEREMBE a. k. a JOSEPH KABILA KABANGE:

- Rais wa Nne wa Jamhuri ya Kidemokrasia Ya Kongo (DRC)

- Alimsaliti Baba Yake Wa Kufikia, LAURENT DESIRE KABILA

- Ni Baada Ya Kuujua Ukweli Kupitia Jenerali James Kabarebe wa Rwanda

JOSEPH Kabila (jina lake halisi ni Hyppolite Christopher Kanambe Kazemberembe), ambaye alizaliwa mwaka 1971 kwa baba wa Kinyarwanda, Christopher Kanambe, na mama wa Kinyarwanda, Marceline Mukambukuje.

Huyo baba yake alikuwa mpinzani wa Rais wa Zamani wa Rwanda, Juvénal Habyarimana.

Aidha, alikutana na Laurent-Désiré Kabila mwaka 1975, wakati (Kabila) akiwa mpinzani wa Rais wa Zamani wa Zaire (sasa ni DRC), Mobutu Sese Seko.

Harakati hizo za upinzani zilizokuwa milimani kwenye mpaka wa Rwanda na Zaire, ambapo kwa pamoja wawili hao walishirikiana kupambana na maadui wao, yaani Mobutu na Habyarimana.

Baada ya kifo cha rafiki yake, yaani Christopher Kanambe mwaka 1977, Laurent-Désiré Kabila alimuoa mke wa marehemu huyo, yaani Marceline, kwa kufuata taratibu za mila za kwao.

Kabila akiwa baba wa kambo aliwachukua watoto wa marehemu ambao ni mapacha, Jenny Kanambe na Hyppolite Kanambe (yaani Kabila mtoto) na kuwalea.

Taarifa za intelejensia kutoka kwa Jenerali James Kabarebe, zinaeleza kuwa Laurent Desire Kabila ndiye alimuua Christopher Kanambe Kazemberembe, kwa sababu ya wivu wa madaraka na pia akachukua mali zake zote, akiwemo mke na hao watoto wawili mapacha.

Aidha, Laurent-Désiré Kabila, ambaye alioa wake wengi (zaidi ya 13) wakati akiwa mafichoni na kupata watoto wengi (zaidi ya 25), hakuwa na muda wa kutosha kuwalea hao watoto wake.

Na kwa kuwa hakufanikiwa kuendelea na masomo yake zaidi ya kiwango cha sekondari, Hyppolite Kanambe alilazimika kufanya kazi mbalimbali za vibarua ili kujikimu.

Kazi hizi ni pamoja na dereva wa teksi, mhudumu wa baa, na fundi wa magari katika miji ya Dar es Salaam na Kigoma, Tanzania.

Kwa kweli, "baba yake mlezi" (yaani baba wa kambo), Laurent-Désiré Kabila, aliishi na familia yake yote akiwa uhamishoni Tanzania, akiwemo ambapo Hyppolite.

Kabila alitumia muda wake mwingi katika biashara ya magendo ya dhahabu na almasi, badala ya kupambana na utawala wa Mobutu.

Hiyo lilimfanya asafiri mara kwa mara kati ya misitu na milima ya Tanzania, Burundi, Rwanda, na Uganda kwa ajili ya hizo shughuli zake za magendo na biashara haramu.

Joseph Kabila alipata hifadhi nchini Tanzania na kufanikiwa kupata elimu ya sekondari, na pia mafunzo ya kijeshi.

Ndipo mwaka 1995 kijana Hyppolite Kanambe alipoamua kurudi kwao nchini Rwanda, ambako alipokelewa na mjomba wake, James Kabarebe, ambaye alikuwa Kanali na Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wanyarwanda (APR).

Kabarebe alimkaribisha nyumbani kwake ambapo mwanzoni alimpatia kazi ya "ukondakta wa lori la mizigo" (yaani 'turn-boy') jijini Kigali.

Baadaye alimpatia kazi ya kuwa dereva wake binafsi.

Mwaka 1996 wakati Wamarekani walipoanzisha kituo cha kijeshi kwa ajili ya maandalizi ya uvamizi wa Zaire, Paul Kagame alimteua Kanali James Kabarebe kuwa Mkuu wa Operesheni za Kijeshi na msimamizi wa "Jalada la Zaire" (yaani daftari la kuandikisha vijana jeshini).

Kabarebe alisimamia uandikishaji huo na pia mafunzo ya wanajeshi wapya, katika kituo hicho cha kijeshi maalumu kwa ajili ya kuingia Zaire.

Hapo ndipo alipomwandikisha mpwa wake, Hyppolite Kanambe, kwenye mpango wa mafunzo ya kijeshi, ili aweze kushiriki baadaye katika operesheni ya kuivamia Zaire.

Hiyo ikiwa na maana kwamba kijana Hyppolite Kanambe alihudumu katika jeshi la Rwanda mwaka 1996.

Mashuhuda kadhaa wanasisitiza ukweli usiopingika kwamba Hyppolite Kanambe, sasa akijulikana kama "Joseph Kabila," anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kinyarwanda, ambayo ni lugha inayotumiwa kwa wingi nchini Rwanda.

MAUAJI YA LAURENT-DÉSIRÉ KABILA

Hakika, sehemu zenye giza ambazo watu hawataki kuangazia (kuzungumzia), ni kuhusu kifo cha Laurent-Désiré Kabila, ambacho habari zake tayari zimeandikwa kwa wino mwingi katika majarida mbalimbali na pia bila fumbo wala kificho.

Hatuna nia mbaya ya kufichua hapa sababu zilizofichwa, lakini huu ni utambulisho halisi ambapo pia waandishi wengi wamekuwa wakieleza juu ya msiba huu.

Hili ni tukio ambalo limegeuza siasa ya Kongo kuwa kama tamthilia isiyoisha.

Hata hivyo, kwa kuchunguza baadhi ya matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya mauaji ya Laurent-Désiré Kabila, moja kwa moja tunaelekea kuona kupaa kwa Joseph Kabila katika ngazi za juu za mamlaka.

Ni katika muktadha huo ambapo hatuwezi kushindwa kushangazwa na mfululizo wa matukio haya, ambayo yanamweka "mwana" wa Laurent-Désiré Kabila katikati ya tukio hili.

Hebu sasa tuchunguze vipengele muhimu vilivyoandaliwa kabla ya tukio lenyewe:-

1. NI Kinshasa, Oktoba 2000 - Kukamatwa kwa Bi. Sifa Mahanya

Bi. Sifa Mahanya, ambaye kwa makosa amekuwa akitambulishwa kama mama mzazi wa Joseph Kabila (tutarudi kwenye hili baadaye), ni Mkongomani wa asili na mmoja wa wake wengi waliotambuliwa kuwa ni Laurent-Désiré Kabila.

Pamoja naye, Kabila alipata watoto 6, ambao ni Joséphine, Cécile, Masengo, Gloria, Kikii na Maguy.

Bi. Sifa alikuwa akiishi na mumewe katika Kasri la Marumaru ambalo ni makazi rasmi ya Mkuu wa Nchi, hadi kuelekea mwishoni mwa Oktoba 2000.

Katika kipindi hicho ndipo Laurent-Désiré Kabila alipatwa na hali mbaya baada ya kula chakula, ambapo vipimo vya haraka vya kitabibu vilibaini kuwa alipewa sumu.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya usalama wa Rais ulionyesha ushahidi wa kutosha kumhusisha Bi. Sifa, ambaye alishtakiwa kwa jaribio la mauaji ya mumewe.

Mara moja, kwa amri ya Laurent-Désiré Kabila, alikamatwa na kufungwa katika gereza la Makala, katika jengo namba 10.

2. Kinshasa, Januari 11, 2001 - Kutoroshwa kwa Bi. Sifa kutoka gerezani

Kwa siri na pia nyuma ya mgongo wa "baba" yake, Joseph Kabila aliratibu kutoroshwa kwa mfungwa huyo kwa msaada wa mkurugenzi wa gereza, Bw. Kelly Dido Kitungua.

Bi. Sifa Mahanya alihamishiwa kwa siri hadi Lubumbashi, ambako aliwekwa mahali pa siri.

3. Lubumbashi, Januari 12, 2001 - Laurent Desire Kabila ashauriwa kufuta safari yake kwenda nchini Cameroon.

Siku moja tu baada ya kutoroshwa Bi. Sifa Mahanya, Joseph Kabila alimpigia simu "baba" yake ambaye alikuwa akijiandaa kusafiri kwenda Cameroon kushiriki Mkutano wa Mataifa ya Francophonie (makoloni ya zamani ya nchi ya Ufaransa), na kumsihi asisafiri.

Alimwambia "baba" yake kwamba alikuwa amenasa taarifa za kiintelijensia, kuhusu njama inayomlenga Rais huyo wa DRC.

Kwa kuwa Kabila alimwamini mno "mwanawe", alighairi safari hiyo na kuamua kurudi Kinshasa moja kwa moja kutoka Lubumbashi.

4. Kinshasa, Januari 15, 2001 - Joseph Kabila aamuru wanajeshi wa Kinshasa kuendelea na majukumu yao kama kawaida wakati yeye akielekea Lubumbashi.

Siku moja kabla ya tukio, na pia kwa amri ya Joseph Kabila, wanajeshi wote wa kambi ya FAC - Kinshasa walinyang’anywa silaha zao bila maelezo.

Aidha, katika hatua nyingine, Kanali Eddy Kapenda alipokea amri kali kutoka kwa Joseph Kabila ya kumkamata Mkuu wa Ujasusi wa Nje wa ANR, Ismaël Tutwemoto.

Amri hiyo ilitekelezwa mara moja, ambapo pia baada ya kuchukua hatua zote hizo na bila maelezo kamili, Joseph Kabila aliondoka kwa haraka na kwa siri kwenda Lubumbashi; na akiwa huko alifanya safari ya ghafla kwenda nje ya mji huo na bila kujulikana alipo.

5. Kinshasa, Januari 16, 2001 - Laurent-Désiré Kabila anauawa.

Mchana wa siku hiyo, milio ya risasi ilisikika ndani ya Kasri la Marumaru la Rais Laurent-Désiré Kabila, ambapo ilibainika kuwa alikuwa amejeruhiwa vibaya kichwani.

Muda mfupi baadaye ilielezwa kuwa alikuwa amefariki, na ikiwa ni kabla ya kupakiwa kwenye helikopta iliyompeleka katika Hospitali binafsi ya Ngaliema.

Ilipofika jioni siku hiyohiyo, Joseph Kabila alitoa amri ya kufunguliwa Uwanja wa Ndege wa N’Djili, ambao ulikuwa umefungwa tangu kutangazwa kwa jaribio la mapinduzi.

Amri hiyo ilikuwa kuruhusu ndege yake kutoka Lubumbashi kutua katika uwanja huo.

Hapo ndipo ilizuka sintofahamu kwamba ilikuwaje mtoto ambaye alikuwa akilinda usalama wa "baba" yake kwa umakini mkubwa hadi siku moja kabla ya mauaji yake, na pia ndiye alimshauri kufuta safari yake kwenda Cameroon kutokana na tishio la kifo, abaki Lubumbashi baada ya kupata taarifa za shambulio dhidi ya "baba" yake?

Kwa nini alichelewa kurejea Kinshasa na kusubiri hadi jioni siku hiyo, muda mrefu baada ya kupata taarifa ya kifo cha "baba" yake?

Alikuwa wapi siku nzima na alikuwa anafanya nini muda wote huo?

Je, Lubumbashi haikuwa sehemu ya mpango wa kuudanganya umma?

Maswali haya na mengi mengine kuhusu sababu za msingi za kifo cha Laurent-Désiré Kabila, yalipaswa kuchunguzwa.

Aidha, ushahidi wa kitabibu kutoka kwa madaktari wa Kongo waliopokea mwili wa Laurent-Désiré Kabila mara baada ya kufikishwa kwenye matibabu, ulionyesha wazi kuwa kiongozi huyo alifariki kabla ya kuwasili hospitalini.

Hata hivyo, Joseph Kabila, ambaye alikuwa ameshikilia udhibiti wa hali nzima ya mambo, aliamuru mwili wa Laurent-Désiré Kabila usafirishwe hadi Harare, Zimbabwe.

Kisha alitoa matamko kadhaa ya uongo kwa wananchi wa Kongo, akiwadanganya kuwa Rais wao alikuwa hai.

Inadaiwa kuwa Dominique Sakombi anajua ukweli huu, na sababu ya mchezo huu wa kificho na mzunguko mzima wa ajabu wa mwili wa Rais wa Jamhuri.

6. Kinshasa - Wakati wa mazishi, Sifa Mahanya anatangazwa kuwa ‘mke mjane’ na ‘mama mzazi’ wa Joseph Kabila.

Wakati wa mazishi ya Laurent-Désiré Kabila, ambayo yalianzia mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, na kumalizika Januari 23, 2001 katika maziko yake jijini Kinshasa, Bi. Sifa Mahanya aliyekuwa ametoroshwa kutoka gerezani siku 5 kabla ya kuuawa kwa Mzee Laurent Desire Kabila, alijitokeza ghafla mbele ya umma.

Aliwasilishwa kwa vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kama "mke mjane" wa Rais aliyefariki na pia "mama mzazi" wa Joseph Kabila, ambaye sasa alikuwa amekalia kiti cha "baba" yake katika mazingira tata.

Ikumbukwe kuwa katika maisha yake yote wakati wa vita na wakati wa utawala wake, Laurent-Désiré Kabila hakuwahi kumtambulisha rasmi "mke wa kwanza" kwa wananchi wa Kongo.

Na yule aliyewasilishwa kama "mke mjane," ni yule alikuwa ametolewa gerezani alikokuwa amefungwa kwa jaribio la kutaka kumuua mumewe kwa sumu.

Na aliyemtorosha ni yuleyule ambaye sasa alikuwa amekalia kiti cha mamlaka ya mwathiriwa.

Na kwa mara ya kwanza kabisa, Bi. Sifa alitoa ushuhuda wa heshima kuwa yeye ndiye "mama mzazi" wa Joseph Kabila.

Imeandikwa na:

SIGNED BY LUGETE MUSSA LUGETE.
GURU OF PHILOSOPHY.
MASTER OF HISTORY.
GIANT OF THE AGE.
PAN AFRICANIST.
Kayonka Kikenke Kamasa Mwamgongo Kigoma.
0755988284

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

RAIS TRUMP ARARUANA NA RAIS WA UKRAINE

MWABUKUSI ATOA NENO SIMBA KUSUSIA DERBY DHIDI YA YANGA

SERIKALI YALIKUBALI OMBI LA DIAMOND

HOSPITALI YA MUHIMBILI YAANZISHA HUDUMA YA KISASA YA KUZIBA MAPENGO

ARAJIGA AULA KOMBE LA DUNIA