Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paulo Chacha akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Julai 11, 2025, kuelezea mafanikio ya miaka minne ya Mkoa huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ndg. Wanahabari,
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwakuendelea kutupa Afya njema na inayotuwezesha kutekeleza shughuli zetu. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
.............
Nipo mbele yenu leo kushirikiana nanyi kuutangazia umma mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mkoa wetu wa Tabora tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwaka 2021. Mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amesimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 - 2025.
1.1 WASIFU WA MKOA
Mkoa wa Tabora una ukubwa wa kilometa za mraba 75,685. Kilometa za mraba 75,173 ni eneo la nchi kavu, kati yake kilometa za mraba 20,199 sawa na asilimia 26.6 zinafaa kwa kilimo; kilometa za mraba 34,501 sawa na asilimia 45.6 ni eneo la misitu ya hifadhi na Kilometa za mraba 20,473 sawa na asilimia 27.1 ni eneo la makazi. Eneo la maji ni Kilometa za mraba 512 sawa na asilimia 0.7.
Mkoa una jumla ya Wilaya 7 za Tabora, Uyui, Igunga, sikonge, Urambo, Kaliua. Aidha, kuna Halmashauri 8 ambazo ni Manispaa ya Tabora, Halmashauri ya mji Nzega, Halmashauri za Wilaya za Igunga, Kaliua, Nzega, Sikonge,Urambo na Uyui. Aidha, Mkoa umegawanyika katika Tarafa 22, Kata 206, Vijiji 724, Mitaa 148 na Vitongoji 3,753.
Mkoa una idadi ya watu 3,391,679 kwa Mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, Wanaume ni 1,661,171, na Wanawake ni 1,730,508.
1.2 HALI YA UCHUMI
Uchumi wa Mkoa unategemea kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvunaji mazao ya maliasili, biashara, uzalishaji katika viwanda vidogo miundombinu, huduma za jamii na Utawala. Kilimo na Ufugaji huchangia asilimia 70 ya pato la Mkoa ambapo mazao makuu yalimwayo kwa ajili ya chakula ni Mahindi, Mpunga, Mtama, Muhogo, Viazi vitamu, Uwele na jamii ya mikunde. Aidha, mazao ya biashara ni tumbaku, pamba, alizeti, karanga na mchikichi.
Hali ya Uchumi ya Mkoa wa Tabora imeendelea kuimarika ambapo Pato halisi la Mkoa limekua kutoka Shilingi Trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi Shilingi Trilioni 6.3 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 17. Vilevile, pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka shilingi milioni 1.77 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 1.85 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.5.
2. MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA MKOA WA TABORA
Ndugu Wanahabari,
Ningependa kuwaletea taarifa fupi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mkoa wa Tabora katika kipindi cha Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Juni, 2025 Mkoa wa Tabora umetekeleza miradi mikubwa yenye thamani zaidi ya Shilingi Trilioni 15. Miradi imetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika sekta zote zikiwemo Afya, Elimu, Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji, Maji, Nishati, Kilimo, Mifugo, Viwanda, Biashara, Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Miradi ya kimkakati n.k. Mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi husika na nawasilisha sehemu ya mafanikio kwa baadhi ya sekta.
2.1 HALI YA ULINZI NA USALAMA
Ndugu Wanahabari,
Hali ya usalama ya Mkoa wa Tabora kwa ujumla ni shwari. Ijapokuwa kuna matukio machache ya uhalifu lakini mkoa unakabiliana nao ipasavyo. Hivyo, matukio hayo machache, hayaathiri shughuli za kila siku za Wananchi na mali zao. Jitihada zinaendelea kufanywa na vyombo vya usalama kwa kushirikisha Wananchi na viongozi wengine katika jamii ili kuwezesha Mkoa wa Tabora kuendelea kuwa katika hali ya utulivu na usalama wakati wote.
2.2 UTAWALA BORA
Ndugu Wanahabari,
Mkoa wa Tabora umeendelea kuisimamia vema kabisa ujenzi wa demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria ili kuwa na mazingira wezeshi kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo. Kuimarika kwa utawala bora kumewezesha kukuza demokrasia, kujenga moyo wa uzalendo, kudumisha amani na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:-
Kutekelezwa kwa programu na mikakati mbalimbali ya kushughulikia malalamiko ya wananchi ikiwemo Programu ya Msaada wa Kisheria wa Samia, wiki ya haki, kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mfuko wa Huduma za Sheria (LSF) ambapo jumla ya malalamiko 949 yalitatuliwa;
Kukamilika ujenzi wa mahakama Kuu Kanda ya Tabora.
Mwaka 2020 Mkoa ulikuwa Vituo vya Polisi 46 hadi kufikia 2025 Mkoa una jumla ya Vituo vya Polisi 48.
Mwaka 2020 Mkoa ulikuwa na Mahakama za mwanzo 41 hadi kufikia 2025 Mkoa una Mahakama za mwanzo 43. Pia Mkoa ulikuwa Mahakama za Wilaya 6 hadi kufikia Aprili, 2025 Mkoa una Mahakama 7.
Mwaka 2020 kulikuwa na vitendo vya rushwa 191, kutokana jitihada mbalimbali zilizofanyika vitendo vya rushwa vimepungua hadi 179 mwaka 2025.
Kukamilika kwa ujenzi/ukarabati wa majengo ya Utawala ikiwemo Ofisi na Makazi.
Ujenzi wa Ofisi kumi na moja (11) za Maafisa Tarafa
Ujenzi wa Nyumba saba (7) za Maafisa Tarafa na uzio kwenye Nyumba moja wapo.
Ujenzi wa Uzio kwenye Nyumba mbili (2) za Wakuu wa Wilaya na Ofisi moja (1) ya Mkuu wa Wilaya.
Ukarabati wa Nyumba ya Mkuu wa Wilaya Tabora
Ukarabati wa Ofisi nne (4) za Wakuu wa Wilaya pamoja na ujenzi wa uzio kwenye ofisi moja wapo.
2.3 UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Ndugu Wanahabari, Serikali imeendelea kutilia mkazo umuhimu wa maendeleo ya wananchi pamoja na ushirikishwaji wa makundi maalum ikiwemo Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu ili kuleta usawa wa kijamii na kiuchumi kwa wote. Katika kufikia azma hiyo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
Utoaji wa Mikopo ya 10% kwa Vikundi vya Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu umeongezeka kwa kipindi cha miaka mitano ambapo kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2024/25 jumla ya Shilingi bilioni 16.1 zimetolewa kwa vikundi 1,967; na
Mpango wa kunusuru kaya masikini unaendelea kutekelezwa ambapo jumla ya Shilingi bilioni 66.17 zilihawilishwa kwa kaya maskini 41,024, katika kipindi husika na miradi ya miundombinu 1,400 ya Elimu, Afya na Barabara imetekelezwa pamoja na kuwezesha walengwa kujiongezea kipato kupitia ufugaji na kilimo.
3. HUDUMA ZA KIJAMII
Sekta ya Afya
Ndugu Wanahabari,
Huduma za afya ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na Afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo. Katika kipindi cha Uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkoa umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 34.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za Afya. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya kutolea huduma za Afya, kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za Afya karibu na wananchi. Mafanikio mengine ni pamoja na:-
Kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali 5 za Wilaya za Uyui, Sikonge, Kaliua, Nzega na Tabora Manispaa.
Kukamilika kwa ujenzi wa majengo manne (4) ya huduma za dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mkoa wa Tabora-Kitete, Hospitali za Halmashauri za Mji wa Nzega, Urambo na Sikonge.
Kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mkoa wa Tabora-Kitete na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Ujenzi wa Vituo vya Afya vipya 30 na umaliziaji wa maboma ya zahanati 109 pamoja na ujenzi wa nyumba mpya 8 za watumishi.
Uboreshaji na kuongeza miundombinu mipya ya kutolea huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tabora – Kitete, ikiwemo Ujenzi wa wodi ya Wazazi ya Ghorofa 2 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora- Kitete, Ujenzi ambao umefikia asilimia 55% wenye lengo la kupunguza vifo vya Wajawazito na Watoto wachanga.
Ukarabati wa Hospitali Kongwe za Halmashauri za Wilaya za Urambo na Igunga.
Kuongezeka kwa idadi ya Hospitali za Wilaya kutoka 3 mwaka 2020 hadi 8 mwaka 2025;
Kuongezeka kwa vituo vya Afya kutoka 29 mwaka 2020 hadi 53 mwaka 2025.
Kuongezeka kwa idadi ya zahanati na Kiliniki kutoka 303 mwaka 2020 hadi 378 mwaka 2025,
Kuongezeka kwa nyumba za watumishi wa Afya kutoka 291 mwaka 2020 hadi 445 mwaka 2025.
Kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka asilimia 75 mwaka 2020 hadi asilimia 91% mwaka 2025. Ongezeko hili limechangiwa na ongezeko la bajeti ya dawa, vifaa na vifaa tiba kutoka Shilingi 4,238,075,963.07 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi 9,841,380,851 kwa mwaka 2024/2025.
Mapokezi ya vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Bilion 11,100,000,000 inayojumuisha mashine ya CT Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Kitete, mashine 6 za X-ray (Digital X-ray Mashine) katika Hospitali za Wilaya katika Halmashauri za Igunga, Uyui, Tabora MC, Urambo, Sikonge na Kaliua, Vifaa Tiba vya Majengo ya EMD na ICU katika Hospitali za Wilaya za Nzega Mji, Urambo, Sikonge, Igunga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Mapokezi ya magari 34 kwa ajili ya huduma za wagonjwa, chanjo na usimamizi wa Huduma za Afya. Ambapo magari ya wagonjwa (Ambulance) ni 23, Chanjo 1 na Usimamizi wa huduma za Afya 10.
Kuongezeka Vituo vya Afya vinavyotoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa Wajawazito katika Mkoa kutoka vituo 14 mwaka 2020 kufikia vituo 42 mwaka 2025.
Ongezeko la Idadi ya Watumishi wa Afya kutoka watumishi 1,773 mwaka 2020 hadi kufikia watumishi 3,798 mwaka 2025.
Sekta ya Elimu
Ndg. Wanahabari,
Utoaji huduma za elimu katika Mkoa umeimarika kwa kiwango kikubwa. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu umefanyika sanjari na kuongeza idadi ya walimu katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati. Jumla ya Shilingi 146.69 bilioni zimetolewa na Serikali kati ya mwaka 2021 hadi mwaka 2025 kwa ajili ya Sekta ya Elimu katika Mkoa. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa uandikishaji na udahili wa wanafunzi, ufaulu pamoja na kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata huduma ya elimu. Mafanikio mengine ni kama ifuatavyo:-
Mpango wa Elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita umeendelea kutekelezwa ambapo fedha za kugharamia mpango huo zimeongezeka kutoka Shilingi 12,835,612,200 mwaka 2020 hadi Shilingi 22,676,904,000 mwaka 2025;
Idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka 819 mwaka 2020 hadi 990 mwaka 2025 na idadi ya shule za sekondari zimeongezeka kutoka 197 mwaka 2020 hadi 264 mwaka 2025;
Idadi ya vyumba vya madarasa ya shule za msingi imeongezeka kutoka madarasa 6,074 mwaka 2020 hadi 8,100 mwaka 2025 na kwa shule za sekondari kutoka madarasa 2,251 mwaka 2020 hadi madarasa 4,047 mwaka 2025;
Nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari zimeongezeka kutoka 2,076 mwaka 2020 hadi 2,334 mwaka 2025;
Ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba umeongezeka kutoka Asilimia 69.8 mwaka 2021 hadi Asiilimia 70.8 mwaka 2025, kidato cha nne kutoka Asimia 88.4 mwaka 2020 hadi Asilimia 95 mwaka 2025 na kidato cha sita kutoka Asilimia 99.96 mwaka 2020 hadi Asilimia 100 mwaka 2025;
Idadi ya walimu walioajiriwa katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari imeongezeka kutoka walimu 10,719 mwaka 2020 hadi walimu 12,354 mwaka 2025;
Mwaka 2020 kulikuwa Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) 3 katika Wilaya ya Tabora, Urambo na Kaliua mpaka kufikia Aprili, 2025 vyuo vya VETA vimejengwa na idadi yake imefikia 6 katika Wilaya za Igunga, Uyui, Tabora, Nzega, Kaliua na Urambo.
Sekta ya Maji
Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Maji katika Mkoa wa Tabora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kaya nyingi zaidi zinaunganishwa na huduma ya maji.
Huduma ya Maji Mijini
Jumla Shilingi 147.9 Bilioni zilipokelewa katika kipindi husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji katika Mkoa wa Tabora, ambapo kiasi cha Shilingi 547.3 Milioni ilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya Uviko – 19, 1.862 Bilioni kwa ajili ya miradi ya Quick Win, 250 Milioni kutoka mfuko wa Maji, 1.628 Bilioni kutoka Serikali Kuu, 143 Bilioni kutoka mradi wa uendelezaji Miji 28 na 600 Milioni kutoka mfuko wa Maji. Kutokana na kupokelewa kwa fedha hizo mafanikio makubwa yamepatikana katika Mkoa ikiwa ni pamoja na:-
Kuimarika kwa huduma ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wa Mkoa kutoka asilimia 75.7 mwaka 2020 hadi asilimia 89.1 mwaka 2025.
Kuongezeka kwa uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 17.6 hadi 39.3 kwa siku na kuongezeka kwa muda wa upatikanaji wa huduma ya maji kutoka masaa 12 hadi 24 kwa kwa Maeneo ya Mijini;
Uboreshaji wa huduma ya usafi wa Mazingira kwa miji ya Tabora, Nzega na Igunga kwa ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka.
Kuongezeka kwa urefu wa mtandao wa majisafi kutoka kilomita 1,359.79 mwaka 2020 hadi kilomita 2,304.02 mwaka 2025 kwa maeneo ya Mijini.
Maji Vijijini
Jumla ya Shilingi 98.043 Bilioni zilipokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji Vijijini. Kutokana na fedha hizo miradi mbalimbali ilitekelezwa Vijijini, ambapo mafanikio yafuatayo yamepatikana:-
Huduma ya maji safi kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora imeimarika ambapo upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2020 hadi asilimia 68.2 mwaka 2025 kwa maeneo ya Vijijini;
Idadi ya vijiji vyenye huduma ya maji safi imeongezeka kutoka Vijiji 393 mwaka 2020 hadi Vijiji 505 mwaka 2025;
Miradi 73 ya Maji imekamilika na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini. Aidha, utekelezaji wa miradi 39 unaendelea iliyofikia wastani wa asilimia 69.8;
Kasi ya uchimbaji wa visima vya maji imeongezeka kutoka visima 1024 mwaka 2020 hadi visima 1118 mwaka 2025;
Mabwawa ya maji yameongezeka kutoka mabwawa 10 mwaka 2020 hadi mabwawa 13 mwaka 2025.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Sekta ya Kilimo
Ndugu Wanahabari,
Sekta ya Kilimo ni sekta muhimu inayogusa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora, Serikali ya awamu ya sita imewezesha Mkoa kusimamia sekta hii ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa wenye tija na usalama wa chakula unaimarika. Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa njia ya ruzuku ya mbolea na mbegu. Aidha, imetoa jumla ya Shilingi 52.8 bilioni kwa ajili ya ruzuku na miradi ya umwagiliaji.
Skimu za umwagiliaji zimeongezeka kutoka skimu 25 mwaka 2020 hadi skimu 46 mwaka 2025;
Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka ekari 16,453.25 mwaka 2020 hadi ekari 37,560.25 mwaka 2025;
Vyama vya umwagiliaji vimeongezeka kutoka 10 mwaka 2020 hadi vyama vya umwagiliaji 23 mwaka 2025;
Hali ya upatikanaji wa mbolea imeimelika kutoka tani 34,109 mwaka 2020/2021 hadi tani 61,504 mwaka 2024/2025; kutokana na ongezeko la upatikanaji wa Mbolea, uzalishaji wa Tumbaku umeongezeka kutoka kilo 29,829,742 mwaka 2021 hadi kilo 62,964,460 mwaka 2025.
Sekta ya Mifugo na Uvuvi
Ndugu Waandishi wa Habari,
Sekta ya Mifugo ni shughuli kuu ya kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora kama ilivyo sekta ya Kilimo. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga, tiba na utafiti wa mifugo ili ufugaji uweze kuwanufaisha wananchi. Mafanikio yafuatayo yamepatikana katika Mkoa wa Tabora:-
Ujenzi wa majosho 16 ya kuogeshea mifugo umekamilika katika Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora na hivyo kufanya idadi ya majosho kufikia 95 ambayo yana uwezo wa kuhudumia ng’ombe 889,183;
Huduma za ugani zimeendelea kuimarishwa ambapo Serikali ilitoa pikipiki 44 kwa ajili ya maafisa mifugo. Aidha, majokofu 6, vitunza baridi (Cool box) 180, automatic syringe 140 na sindano 2,160 zimetolewa kwa ajili ya kampeni ya chanjo Kitaifa;
Mashamba darasa ya malisho ya mifugo yameendelea kuanzishwa pamoja na uboreshaji wa mbari za mifugo kwa kusambaza mbegu bora za mifugo 368 kwa njia ya uhimilishaji; na
Uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 1,200,000 mwaka 2020 hadi lita 2,030,720 mwaka 2025.
Uvuvi
Kwa upande wa Uvuvi, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi na masoko ya mazao ya uvuvi ili kuhakikisha kuwa sekta hii inanufaisha pia wananchi wa Mkoa wa Tabora. Mafanikio katika Sekta hii ni pamoja na:-
Utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wavuvi wadogo umeongezeka kutoka Shilingi 21,750,000 mwaka 2020 hadi Shilingi 84,000,000 mwaka 2025;
Kujenga miundombinu ya ukuzaji viumbemaji (mabwawa na vizimba) yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 katika kituo cha ukuzaji wa viumbe maji Mwamapuli;
Boti yenye thamani ya Shilingi 32,000,000 imenunuliwa kwa ajili ya kuimarisha doria kwenye maeneo ya uvuvi;
Uzalishaji wa vifaranga vya samaki umeongezeka kutoka vifaranga 540,000 mwaka 2020 hadi vifaranga 5,420,410 mwaka 2025.
Madini
Kwa kutambua kuwa sekta ya madini ina nafasi ya kipekee katika kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa, upatikanaji wa fedha za kigeni na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Serikali imeendelea kuimarisha sekta hii katika Mkoa wa Tabora, ambapo kwa kipindi cha 2021-2025 mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na:
Kuongezeka kwa uzalishaji wa madini kutoka tani 0.34 mwaka 2020 hadi tani 0.8 mwaka 2025;
Kuongezeka kwa fedha za kigeni zilizotokana na uuzaji wa madini kutoka Dola za Marekani 15,068,988.01 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani 50,692,090.41 mwaka 2025 (thamani ya USD = 2,624.10);
Kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri yatokanayo na uchimbaji wa madini kutoka Shilingi 118,627,594.27 mwaka 2020 hadi Shilingi 399,063,343.30 mwaka 2025;
Kuongezeka kwa masoko ya madini kutoka soko 1 na kituo kidogo 1 mwaka 2020 hadi soko 1 na vituo 5 mwaka 2025; na
Kuongezeka kwa utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo kutoka leseni 136 mwaka 2020 hadi 574 mwaka 2025.
Viwanda na Biashara
Ndugu Wanahabari, Mkoa wa Tabora unatambua kuwa viwanda na biashara ni nguzo na kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi, kuongeza uwezo wa Taifa kujitegemea na uzalishaji wa ajira. Katika kipindi cha Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Tabora umefanikiwa katika yafuatayo:-
Kuanzishwa kwa viwanda vikubwa 3, vya kati 19, vidogo 984 na vidogo sana 324;
Kuanzisha na kuendeleza kongani 1 za viwanda; na
Kuongezeka kwa ajira za viwandani, ambapo jumla ya wananchi 3,325 wameajiriwa.
Maliasili na Utalii
Ndugu Waandishi wa Habari,
Nyote mnakumbuka kuwa mara baada ya kuingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua filamu ya Royal Tour, Filamu hiyo imewezesha sekta ya Utalii kuanza kupokea watalii wengi kila mwaka na hivyo kuongeza mapato katika sekta hiyo. Aidha, Mkoa wa Tabora umepata mafanikio makubwa katika sekta hii ambayo baadhi yake ni kama ifuatavyo:
Idadi ya watalii wa ndani waliotembelea Mkoa imeongezeka kutoka watalii 1,283 mwaka 2020 hadi 7,397 mwaka 2025;
Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka shilingi 6,167,860 mwaka 2020 hadi shilingi 26,622,674 mwaka 2025;
Viwanda 04 vya kuchakata na kufungasha Asali vimejengwa;
Uzalishaji wa Asali umeongezeka kutoka tani 1,868.6 mwaka 2020 hadi tani 2,002.48 kwa mwaka 2025;
Misitu ya hifadhi ya vijiji imeongezeka kutoka misitu 6 yenye ukubwa wa ekari 11,952.5 mwaka 2020 hadi misitu 37 yenye ukubwa wa ekari 330,780.75 mwaka 2025;
Miti takriban 1,500,000 imepandwa ambayo ni asilimia 80 ya lengo la Serikali kwa mwaka.
MIUNDOMBINU
Ndugu wana habari, Katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi dhabiti wa Rais Samia,Serikali ya mkoa wetu wa Tabora imeendelea kusimamia vema ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, madaraja, makalvati, Reli, Nishati na Viwanja vya ndege ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
Barabara
Katika kipindi tajwa Mkoa wa Tabora wenye mtandao wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 10,592 (TANROADS Km 2,188 na TARURA Km 8,404) ulipokea kiasi cha Shilingi 225.993 bilioni (TANROADS Shilingi 124.277 Bilioni na TARURA Shilingi 101.716 Bilioni). Kiasi hiki cha fedha kimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
Barabara za Wakala Ya Barabara Tanzania (TANROADS)
Kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami kutoka kilomita 753.17 mwaka 2020 hadi kilomita 853.4 mwaka 2025;
Comments