Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akimkakabidhi mkoba wenye fomu za kuomba kuteuliwa kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis aliyeambatana na Mgombea Mwenza,Dkt. Evaline Wilbard Munisi katika tukio lililofanyika Agosti 15, 2025 Njedengwa jijini Dodoma.
Chama kingine kilichochukua fomu leo Agosti 15 ni United Democratic Party (UDP), Mgombea urais akiwa Saum Hussein Rashid na mgombea mwenza Juma Khamis Faki.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuchukua fomu, Mgombea pendekezwa wa Urais wa chama hicho, Khamis amesema kuwa chama chake kikishinda watahakikisha wanarekebisha Katiba ya Nchi ndani siku 100.
Chama kilichochukua fomu Agosti 14 ni; Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias Mulumbe (Urais) aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Shoka Khamis Juma.
Vyama vingine vilivyochukua fumu Agosti 13, 2025 ni; Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya (Urais) aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Masoud Abrahman Khatib na Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Paul Kyara (Urais) aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Satia Mussa Bebwa.
Vilivyochukua fomu Agosti 12, 2025 ni; Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) ambacho mgombea wake urais ni Mwajuma Noty Mirambo aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Mashavu Alawi Haji pamoja na Chama cha Tanzania Democratic Alliance ( ADA-TADEA), ambacho mgombea urais ni Georges Gabriel Bussungu aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Ali Makame Issa.
Wagombea wengine waliochukua fomu Agosti 10, 2025 ni; Chama cha MAKINI ambacho wagombea wake ni Coaster Jimmy Kibonde. na Mgombea Mwenza, Aziza Haji Suleiman, National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo (Urais) na Mgombea Mwenza, Chausiku Khatib Mohamed pamoja na United Peoples Democratic Party (UPDP), Twalib Ibrahim Kadege (Urais), Mgombea Mwenza, Abdalla Mohd Khamisi.
Vyama vilivyofungua pazia ya uchukuaji fomu Agosti 9, 2025 ni; Chama Cha Mapinduzi (CCM) mgombea wake wa Urais ni Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza, Dkt. John Nchimbi, Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) walikuwa ni Hassan Kisabya Almas (Rais). na Mgombea Mwenza, Hamisi Ally Hassan pamoja na Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP),Kunje Ngombale Mwiru (urais). Mgombea huyo wa AAFP aliambatana na Mgombea Mwenza, Shum Juma Abdalla.Hadi leo hii vyama vilivyochukua fomu ni 12.
Tume inataraji kufanya uteuzi wa wagombea Agosti 27 mwaka huu na kampeni zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025. Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utafanyika Oktoba 29.

Khamis akipumgia mkono alipowasili Tume kuchukua fomu.
Comments