
MENEJA wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bi. Veronica Simba,akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Brother Martin iliyopo jijini Dodoma mara baada ya kutembelea banda la WMA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Brother Martin ya jijini Dodoma wamepata fursa ya kujifunza kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi, baada ya kutembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Akizungumza na wanafunzi hao, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA, Bi. Veronica Simba, amesema kuwa utoaji wa elimu ya vipimo kwa wanafunzi ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kufikisha uelewa wa vipimo sahihi kwa jamii kuanzia ngazi ya chini.
“Elimu ya vipimo ni msingi muhimu katika maisha ya kila siku, hasa katika shughuli za biashara na matumizi ya kila siku. Tunataka watoto wajifunze mapema kuhusu haki zao na namna ya kutambua vipimo sahihi ili wawe raia wanaotambua thamani ya usahihi na uadilifu,” amesema Bi. Simba.
Katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wanafunzi wengi zaidi, Wakala wa Vipimo umedhamiria kuanzisha vilabu vya vipimo katika shule mbalimbali nchini. Lengo ni kuwajengea wanafunzi msingi thabiti wa kuelewa masuala ya vipimo na kuwa mabalozi wa elimu hiyo katika jamii zao.
Maonesho ya Nanenane hutoa fursa kwa taasisi mbalimbali kuonesha huduma na bidhaa zao, huku pia yakiwapa wananchi nafasi ya kupata elimu ya kitaalamu kuhusu sekta mbalimbali ikiwemo vipimo, kilimo, afya na teknolojia.
Comments