DANIEL SILLO AZIDI KUPAA KISIASA.


Mbunge wa Babati Vijijini, Ndugu Daniel Baran Sillo, ameendelea kuandika historia katika medani ya siasa nchini, hususan mkoani Manyara. 

Safari yake ya kisiasa ilianza kwa uthubutu na ujasiri mwaka 2015, alipojitosa kwa mara ya kwanza kuwania ubunge, ingawa hakufanikiwa. 

Hata hivyo, hakurudi nyuma. Mwaka 2020 alirejea tena kwa nguvu mpya na kuibuka na ushindi, hatua iliyompa nafasi ya kuwa mwakilishi wa wananchi wa Babati Vijijini.

Katika muda mfupi wa uongozi wake, Sillo amekuwa miongoni mwa wanasiasa waliopanda ngazi kwa kasi, jambo ambalo halijazoeleka kwa wengi mkoani Manyara. 

Historia hiyo inamuweka sambamba na viongozi wakubwa waliotoka Manyara kama Frederick Sumaye aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mary Nagu, Mateo Qaresi, pamoja na Balozi Philip Marmo, waliowahi kushika nafasi muhimu za kitaifa.

Mara baada ya kuingia bungeni, Sillo alichaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Bunge, nafasi aliyochukua baada ya Mussa Zungu kuteuliwa kuwa Naibu Spika. Uongozi wake ulionekana na wabunge wengi kama wa kuaminiwa na wenye weledi.

Baadaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mwaka 2025-2030, baada ya kuendelea kuaminiwa na wananchi na kuchaguliwa tena kuwa Mbunge, jina lake limeibuka kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, hatua inayodhihirisha imani kubwa aliyonayo kwa wananchi na viongozi wenzake. 

Katika mitandao ya kijamii, wananchi wengi wameonekana kumuombea dua na kumtakia heri, huku wengine wakionesha matarajio kuwa huenda akafika mbali zaidi, hata kwenye nafasi ya uwaziri.

Mpaka sasa, waliowania nafasi za Uspika na Unaibu Spika ni:

Uspika:

Dkt. Tulia Ackson

Mussa Azzan Zungu

Stephen Julius Masele

Unaibu Spika:

Timotheo Paul Mzava

Daniel Baran Sillo

Najma Murtaza Giga

Mgeni Hassan Juma

Kwa nafasi hizi, Daniel Baran Sillo ameweka alama kuwa miongoni mwa viongozi wanaokua na kukubalika kwa kasi, na hivyo ameandika ukurasa mpya katika historia ya siasa za Tanzania, hususan kutoka Manyara.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

VITU 10 WANAUME WANAVYOPENDA ZAIDI TOKA KWA MWANAMKE — SIYO SURA, SIYO MWILI ❤️

WALIOCHUKUA FOMU CCM ZA KUWANIA USPIKA HAWA HAPA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

RAIS SAMIA SIO RAIS JOYCE BANDA WA MALAWI, TANZANIA SIO KENYA

MJUE VIZURI KOCHA MPYA WA YANGA PEDRO

MATOKEO YA DARASA LA 7 YATANGAZWA