MKATABA WA UBORESHAJI RELI YA TAZARA UNA MANUFAA MAKUBWA KWA TANZANIA- MSIGWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amewahakikishia Watanzania kuwa mkataba ambao Tanzania na Zambia zimeingia na China wa uboreshaji wa reli ya TAZARA utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kiuchumi na kijamii.

Msigwa aliyekuwa akitoa ufafanuzi kufuatia baadhi ya watumiaji wa mitandao kupotosha kwa kubeza hatua hiyo, amesema reli ya TAZARA ambayo ilijengwa kwa mkopo usio na riba kutoka China kati ya mwaka 1970 na 1975 na kisha mwaka 1976 kukabidhiwa kwa Tanzania na Zambia ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiuendeshaji  hali iliyosababisha kukosa tija, kushindwa kujiendesha na kulazimu Serikali kutumia fedha zake kuiendesha.

Amefafanua kuwa kupitia mkataba ambao Tanzania na Zambia zimeingia na nchi ya China kupitia kampuni CCECC, China itawekeza kiasi cha dola za Marekani Bilioni 1.4 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 3 na Bilioni 450 ambazo zitaboresha miundombinu ya reli, kujenga vituo, kununua treni ya abiria na pia kujenga kituo kikubwa cha Kidatu Transshipment Joint ambacho kitawezesha mizigo kutoka reli ya kati ambayo ina kiwango cha MGR kuhamishiwa katika reli ya TAZARA ambayo ina kiwango Cape Gauge.

Amebainisha kuwa pamoja na uboreshaji huo, kampuni ya CCECC ambayo itaboresha reli kwa miaka mitatu na kuiendesha reli hiyo kwa miaka 30 itakuwa inatoa kwa Serikali dola za Marekani Milioni 30 kila mwaka (sawa na shilingi Bilioni 35) ikilinganishwa na sasa ambapo Serikali ya Tanzania pekee inalazimika kutoa shilingi zaidi ya Bilioni 28 ili kuchangia uendeshaji wa TAZARA.

Kutokana na uwekezaji huo TAZARA inatarajiwa kuchochea uchumi wa Tanzania na Zambia kwa kiwango kikubwa kwa kuwa reli hiyo inaunganishwa na mtandao wa reli za kiwango cha Cape Gauge zenye urefu za zaidi ya kilometa 50 Barani Afrika.

Baadhi ya manufaa ambayo Tanzania itanufaika ni pamoja na kurahisisha usafirishaji wa madini mbalimbali yakiwemo madini adimu yaliyopo Tanzania (rare earth elements, cobalt, granite, makaa ya mawe na chuma pamoja na mazao mbalimbali ya kilimo kwenda nchi za SADC na kwenda Bandari ya Dar es Salaam.

Msigwa ametoa wito kwa Watanzania kupuuza wanaobeza mafanikio ya kupata uwekezaji huo mkubwa ambao umefanikiwa baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kukutana na Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping kukubaliana nae kuwekeza katika uboreshaji wa TAZARA na pia Rais Samia alipokwenda kuhutubia Bunge la Zambia na kutoa wito kwa Serikali ya Zambia kukubali uboreshaji wa reli hiyo kufanyika.

Tayari Waziri Mkuu wa China Bw. Li Qiang amezindua uboreshaji wa TAZARA nchini Zambia ikiwa ni utekelezaji wa mradi huo.



 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAPACHA WATATU FAMILIA YA MWAIKENDA WAPATA KIPAIMARA

๐Œ๐‰๐”๐„ ๐Š๐€๐‚๐‡๐„๐‘๐Ž ๐Œ๐™๐„๐๐€

MVUA KUBWA KUNYESHA MIKOA 20

NAMNA YA KUTENGENEZA MAISHA YAKO KIMYA KIMYA

Wasifu wa Kizza Besigye

AINA 4 ZA WANAWAKE WASIOWEZA KUDUMISHA NDOA.

NAPE AWAPA UKWELI VIJANA

HAKUNA DHEHEBU LA DINI AMBALO LIKO JUU YA LINGINE, MADHEHEBU YOTE YAKO SAWA KISHERIA - RAIS SAMIA