Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA imekamata gari lenye muonekano wa basi, huku kwa ndani likiwa limegawanywa mara mbili upande mmoja ukiwa ni basi la abiria na nusu iliyobaki likiwa ni lori la mizigo.
Basi hilo aina ya Scania la Kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili wa nchi ya Msumbiji namba AAM 297 CA na hufanya safari zake kati ya Nampula Msumbiji na Tanzania, limekamatwa likiwa na kilogramu 20.03 zikiwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba.
Kamishna Jenerali wa DCEA, ARETAS LYIMO amesema kufuatia operesheni hiyo wamewakamata watuhumiwa Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji.
Huko Sinza C mtaa wa Bustani nyumba namba 16, Mamlaka hiyo pia imemkamata raia wa Kenya Jefferson Kilonzo Mwende (35), akiwa na gramu 131.88 za Heroin, akitumia biashara ya kuuza chai kuficha biashara ya dawa za kulevya anayoifanya.
Katika operesheni zilizofanyika mwishoni mwa Desemba 2025, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogamu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki kumi na moja na magari matatu huku watuhumiwa 66 wakihusika na uhalifu huo.


Comments