Klabu ya Young Africans imetangaza rasmi mwito wa kuwasilisha barua ya kuonesha nia (EOI) kwa wawekezaji na wabia wa kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa eneo la Jangwani/Twiga Street jijini Dar es Salaam.
Yanga iko tayari kuingia ubia kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Naming Rights, Sponsorship-led funding, PPP na DBFO, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha mapato na maendeleo ya klabu kwa muda mrefu.
Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha EOI, Yanga wamesema ni Januari 23, 2026, Saa 10:00 jioni
SIFA WALIZOZIOANISHA YANGA UWANJA WAO WANAVYOTAKA UWE
- Muwekezaji anapaswa kujenga uwanja wenye uwezo wa kuwa na viti 25,000 hadi 35,000 vya kukaa.
- Pitch (sehemu yake ya kuchezea) inapaswa iwe ni 'Hybrid' (mchanganyiko nyasi asili na bandia).
- Uwe na mifumo ya taa za Uwanjani, mifereji ya maji na umwagiliaji.
- Uwe na maeneo ya VIP/huduma maalum, vyombo vya habari, matangazo na uendeshaji.
- Uwe na mifumo ya usalama na udhibiti.
- Uwanja uwe na maegesho, barabara za kufikia, kazi za nje na upandaji miti (mahitaji ya mwisho yatatolewa wakati wa hatua inayofuata kwa washirika walioorodheshwa na wanaovutiwa).
Hatua hii inaonesha dhamira ya Yanga ya kujenga uwanja wa kisasa wa viwango vya kimataifa na kuendelea kuimarisha hadhi ya klabu kitaifa na kimataifa.

Comments