NDEGE ZA ATCL ZASHINDWA KUTUA UWANJA WA SONGWE MBEYA



 Ndege mbili za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) zilizokuwa zikifanya safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya jana Januari 04, 2026 zilishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Songwe kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokuwepo wakati wa kutua.


ATCL imethibitisha hayo kupitia taarifa yake ya leo Januari 05, 2026 ikizitaja Ndege hizo kuwa ni TC 106 (Airbus A220-300), iliyoondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa 2:08 usiku ikiwa na abiria 119, pamoja na TC 2106 (De Havilland Q400), iliyoondoka majira ya saa 2:15 usiku ikiwa na abiria 62.


Aidha ATCL imesema kutokana na hali ya hewa kutoruhusu kutua kwa usalama, marubani walilazimika kurejea Dar es Salaam kwa kuzingatia taratibu na viwango vya usalama wa anga na kubainisha kuwa abiria wote waliokuwa katika safari hizo walirejeshwa salama Dar es Salaam


ATCL, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliendelea kufuatilia kwa karibu hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Songwe ili kubaini uwezekano wa kuendelea na safari hizo kwa usalama lakini hewa haikuboreka kwa kiwango kilichoruhusu safari hizo kufanyika, hali iliyosababisha abiria kushindwa kusafiri kwa zaidi ya masaa kumi.


Aidha, kwa taarifa za awali za kuboreka kwa hali ya hewa, ATCL inatarajia kurejesha safari hizo kwa kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, kabla ya saa 6:00 mchana, na kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kabla ya saa 8:00 mchana, endapo hali ya hewa itaendelea kuimarika.



Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAPACHA WATATU FAMILIA YA MWAIKENDA WAPATA KIPAIMARA

MVUA KUBWA KUNYESHA MIKOA 20

AINA 4 ZA WANAWAKE WASIOWEZA KUDUMISHA NDOA.

NAMNA YA KUTENGENEZA MAISHA YAKO KIMYA KIMYA

Wasifu wa Kizza Besigye

MADAKTARI WALIPAMBANA KWA NGUVU ZOTE KUMNUSURU JENISTA MHAGAMA IKASHINDAKANA- MCHENGERWA