Kumbe Jenista Aliumwa Akazidiwa Dodoma Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amefichua kuwa licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuokoa maisha ya aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, hali yake ilikuwa mbaya sana alipowasili hospitalini hapo na baadaye alifariki dunia.
Akizungumza leo Jijini Dodoma, nyumbani kwa marehemu Itega, Mchengerwa amesema alipokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwamba madaktari walipambana kwa nguvu zote tangu walipompokea marehemu, lakini licha ya juhudi hizo, Mungu alimchukua.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru madaktari wote waliomhudumia pale Benjamin Mkapa. Walifanya kazi kubwa sana mpaka dakika za mwisho ambapo Katibu Mkuu alinifahamisha kuwa hali yake ilikuwa mbaya sana na baadaye Mwenyezi Mungu akamchukua,” amesema Mchengerwa.
Aidha, Waziri Mchengerwa amewataka madaktari wa hospitali hiyo kuendelea kuwa na moyo wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa wengine kama walivyofanya kwa marehemu Jenista Mhagama.
Vilevile, ameahidi kuwa Wizara ya Afya itaendeleza na kutekeleza maono, dira na miradi aliyoiacha Jenista Mhagama mara baada ya kumkabidhi kijiti cha uongozi ndani ya wizara hiyo hivi karibuni.

Comments