HISTORIA YA MAREHEMU MC PILIPILI

Emmanuel Mathias almaarufu kama Mc Pilipili mwenye uso wa uchekeshaji kama kazi yake ilivyo, alizaliwa mtaa wa Airport Dodoma mjini mnamo tarehe 1 mwezi wa 10 mwaka 1985 akiwa ni mtoto wa pili wa Bwana Mathias Matebe na Bi Mariam Matebe.

 Emmanuel alianza elimu yake ya shule ya msingi katika shule ya msingi Kiwanja cha Ndege ambapo alisoma mpaka darasa la nne na kuhamia shule ya msingi Ipagala ambako alimalizia elimu yake ya msingi hapo mnamo mwaka 2000.

Akiwa shule ya msingi Emmanuel kijana mdogo na mcheshi alijihusisha na masuala ya uchoraji, uimbaji na hata kucheza muziki ingawa alikua na ndoto za kuwa Muandishi wa habari.
“mimi nilivutiwa saana na kazi za waaandishi wa habari na nikatamani sana siku moja niwe muandishi wa habari kama wao, japo nilikuwa pia natamani kuwa Mchungaji”. Alielezea kwa Emmanuel kwa kukumbuka.

“Nkumbuka nikiwa na umri wa miaka nane, ilikuja bendi ya Afriso iliyokuwa chini ya Super Lovii Longomba, kaka wa Awilo Longomba, daah! Nilitunzwa hela nyingii na ndio ilikuwa hela yangu ya kwanza ambayo pia niliitumia kulipa kodi ya nyumba tuliokuwa tunadaiwa na pia kununulia debe la unga kwani kwa kipindi hicho baba yangu alikuwa muuza mishkaki na mama alikuwa anauza ndizi hospitali hivyo hawakuweza kwa kipindi hicho kulipa kodi hali iliyopelekea kutaka kufukuzwa tulipokuwa tunaishi, ilitusaidia sana”.

Akiwa bado na umri mdogo, aliweza pia kuigiza sauti mbalimbali kama ya mwalimu Nyerere, Mwakasege, Mr. Bean na pia kubadili nyimbo za wasanii mbalimbali wa kizazi kipya na kuziimba kwa Kigogo. Nyimbo

hizo ni kama Zeze, Mapozi, Seya na hata Zuwena.
Emmanuel aliweza kutunukiwa cheti cha ‘MTOTO WA NURU’ kama mtoto wa mfano na wa kuigwa katika kanisa la Baptist Bible Church ambapo alikuwa akisali na familia yake.

Baaada ya kumaliza darasa la saba Emmanuel alijiunga na Shule ya sekondari Dodoma (Dodoma sekondari) mwaka 2001 ambapo ndoto zake za kuwa muandishi wa habari zilipoanza kufunikwa taratibu.
Akiwa sekondari kama ilivyo kawaida huwa kuna masomo ya kuchagua, kutokana na tabia yake, mwalimu Kilela ambaye sasa ni marehemu alinishauri nichukue somo la ‘Theatre arts’ ambalo ni la Sanaa ya jukwaani somo ambalo alilipenda na kufaulu kuliko masomo mengine.

“Ilifikia hatua kila ninachoongea au watu wakiniangalia tu wanacheka, mpaka darasani ilifika hatua nikinyoosha mkono kujibu swali mwalimu hanichagui anajua ntachekesha tu”.

Emmanuel alipendelea masuala ya sanaa hali iliyopelekea kipaji chake cha uchekeshaji kukua na hata kuanza kuwa mshereheshaji (MC) katika matukio mbalimbali kama Birthday, Sendoff, Harusi na hata Vipaimara na baadaye kutunukiwa cheti cha ‘SPECIAL TALENT’ ama kipaji maalum alipohitimu kidato cha nne.
Aliendelea na kazi ya Ushereheshaji hata alipofika kuanza masomo ya kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Jubilee mkoani Dodoma.

Baada ya kuhitimu kidato cha Sita, Emmanuel alipata ufadhili kutoka kwa wahisani ambapo alipaswa kwenda kusomea Ualimu.

“nilipata wakati mgumu sana kufanya uamuzi kwani nilipenda kuwa Mwandishi wa habari na wakati huo huo mama yangu alisisitiza niende ualimu kwani hata katika Familia yetu tu hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa mwandishi wa habari”.

Emmanuel alikubali kwenda katika Chuo cha Ualimu Eckenforde kilichoko mkoani Tanga.
Alipofika chuoni hapo alipata changamoto ya kusitisha tabia yake ya Uchekeshaji kwani alionywa na familia yake kuwa makini kwani amefadhiliwa hivyo akazane na kitu alichofuata chuoni.

“Kwakweli nilipata shida sana kwani hata nikisimama kimya mbele za watu walikua wanaangua vicheko wengine mpaka wanatoka machozi”. Alihadithia Emmanuel.

Waswahili husema, Maji ukiyavulia nguo sharti Uyaoge. Emmanueli au MC Pilipili alijikuta akiyaoga maji ya Uchekeshaji kwani alijikuta akianza kusherehesha katika Matamasha mbalimbali ya kidini ndani na nje ya Chuo.

“Kila palipotokea matamasha ya kidini kama Joint mass au Graduation walinichagua kuwa MC na watu walikuwa wakisikia ni mimi ntaogoza walifurahi na kujaa kwa wingi. Nilipata fursa ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa kazi hii kama Dar es salaam na Morogoro”.

Mnamo mwaka 2009 Emmanuel alihitimu mafunzo yake ya Ualimu chuoni hapo na kupangiwa kufanya kazi Mkoani Manyara.
“Lakini sikupenda mkoa ule kwa sababu hauna sherehe nyingi kwahiyo nikaona kazi yangu ya uchekeshaji na uMC itakuwa ngumu kuifanya, ikabidi niombe kufundisha katika shule niliyosoma kidato cha tano na sita na walinipokea tayari kwa kazi ya ualimu hapo”.
Mwaka huo wa 2009 Emmanuel alijikuta ana majukumu makubwa ya kuhudumia familia kwani kwa kipindi hicho baba yake mzazi alikuwa mgonjwa hivyo mama ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mwalimu katika shule moja ya chekechea mjini hapo alikuwa anamuuguza baba nyumbani.
Itaendelea...
Chanzo: MC Pilipili Blog)

 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

VITU 10 WANAUME WANAVYOPENDA ZAIDI TOKA KWA MWANAMKE — SIYO SURA, SIYO MWILI ❤️

WALIOCHUKUA FOMU CCM ZA KUWANIA USPIKA HAWA HAPA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MATOKEO YA DARASA LA 7 YATANGAZWA

MJUE VIZURI KOCHA MPYA WA YANGA PEDRO

JESHI LA POLISI LATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA, LAONDOA KIZUIZI CHA KUTOTOKA NJE BAADA YA SAA 12 JIONI