CHAKULA; SIRI INAYOWAPA NGUVU NA JEURI WAYAHUDI DUNIANI

*SEHEMU YA 11:*

...... _makala hii inakuja kwako kwa udhamini wa DRK Karagwe_

*Denis Mpagaze*
___________________________
Kwa Wayahudi, meza ya chakula siyo tu sahani ya ugali na bakuli la mboga, bali ni madhabahu ya mshikamano na upendo. Ndiyo maana wakatengeneza sheria kali za kuwaongoza katika kula.

Wayahudi hawali kila kitu hovyo kama wanavyofanya huko kwenu ambako mnakula kila kitu. Hii ni hatari sana. Maana hata wanyama hawali kila kitu. Wanachagua.

Kula kila kitu bila mipaka ni chanzo cha matatizo ya kiafya na kiakili. Unajua chakula kina mengi. Ukikifakamia lazima kikujeruhi kimwili, kiakili na kiroho pia. 

Magonjwa mengi yamejificha kwenye ulaji. Ulaji una taratibu zake ndiyo maana Wayahudi wako vizuri sanaa katika eneo hilo.

Wana miiko ya ulaji wa nyama, matunda, samaki, maziwa, ndege na wadudu. 

*Wanyama!*

Kwao, mnyama asiyecheua na asiye na asiyekuwa na kwato zilizopasuka ni najisi. Hawali! 

Unajua ni kwa nini? 

Shida ya wanyama wasio na kwato zilizopasuka kama farasi, punda na punda milia hutembea kwa kishindo. Wanakita na kugonga ardhi badala ya kunyata. 

Kwa tafsiri ya Wayahudi, mnyama anayekita ardhi ni ishara ya papara na ukosefu wa nidhamu kwa asili. 

Ukila mnyama wa namna hiyo, unajivika tabia za papara, uchafu na maisha yasiyo na utulivu. 

Wayahudi hawali kabisa mnyama asiyecheua. Kucheua ni tendo la kurudisha chakula tumboni na kukitafuna tena, ili kiwe rahisi kumeng’enywa. 

Kwao, kitendo hiki ni alama ya tafakuri na umakini wa kurudia jambo mara kadhaa kabla ya kulikubali. Fikiria mara mbili kabla ya kuanza kula vya watu!😀😀

Ukila visivyocheua, unakosa utulivu na umakini wa kufanya maamuzi. Nguruwe, kwa mfano, hacheui, ndiyo maana ni haramu kwa Wayahudi. 

Kula nguruwe ni kama kujivika tabia za papara na kukosa umakini katika maamuzi. Unafanya mambo kama nguruwe tu! Wala nguruwe eamefikwa.

*Wadudu*

Lakini pia wadudu wote wanaotambaa kama mende, sisimizi, buibui, nyoka na wale wanaotambaa kwenye mboga za majani ni haramu.

Kwa wayahudi, wadudu ni tafasiri ya uchafu na magonjwa. Huashiria maisha yasiyokuwa na thamani.

Hivyo kula wadudu kwao ni kama kuishi maisha ya kutojali afya na utu wako. Ni kujishushia thamani yako.

*Samaki*

Kwa wayahudi samaki wasiokuwa na magamba na mapezi kama kamba, kaa, chaza, ngisi na pweza ni najisi.

Kamba na kaa wanaishi chini ya bahari, wakikusanya na kula uchafu. Kwa Wayahudi, kula samaki hao ni kujivika tabia chafu kama kamaba na kaa!

Ngisi na pweza hutumia mikono mingi kutembea. Wakianza kutembea huwezi kujua wanaelekea wapi, halafu wako slow sana.

Kwa Wayahudi, kula ngisi na pweza utakuwa na maisha yasiyo na dira, maisha ya kukosa mwelekeo.

Myahudi anakula zake samaki wenye magamba na mapezi. Mapezi kwenye samaki ni kama usukani na injini, humsaidia kuogelea kwa kasi, kudhibiti mwendo, kubadilisha mwelekeo na kujikinga na hatari. 

Kula samaki wenye mapezi ni kuchagua maisha yenye mwelekeo.

Kula samaki wenye magamba ni kuchagua maisha yenye kinga.

Magamba hulinda samaki wasipate majeraha na maambukizi. Ni kama ulinzi kwa samaki. 

Magamba pia humsaidia samaki kujificha na hatari kama wanyama wanaomuwinda. 

Ukila samaki hao maana yake utakuwa na busara ya kujua lini ujifiche na kujilinda, na lini ujitokeze. 

Kujua lini ujifiche ni njia ya kujilinda na kuepuka aibu kubwa baadaye.

*Ndege*

Kwa Wayahudi kula ndege wanaokula nyama na mizoga, kama tai, kipanga na kunguru ni najisi kwa sababu huambukiza tabia zao za ukatili. 

Hakuna ukatili duniani kama kula mzogo. Kula mzoga ni sawa na kula marehemu. Sasa ndege anayekula marehemu ukimla lazima uwe na tabia hizo. 

You are what you eat alisema Anthelme Brillat-Savarin, Mwanasheria na mwandishi wa Kifaransa mwaka 1826. Niambie unachokula, nitakuambia wewe ni nani.

Kunguru anaweza kunyakua kuku mwenye vifaranga na kumla. Huu ni ukatili na tamaa isiyo na huruma. Binadamu anayekula kunguru anaweza kula mtu!   

Kula ndege wala mizoga kwa wayahudi ina maana utakuwa mtu wa kuishi kwa makombo badala ya kutafuta vitu freshi. Unakuwa mtu 
wa kutegemea vilivyopitwa na wakati.

Kwa wayahudi tai na kipanga ni mfano wa watu wanaotumia nguvu na ukatili kufanikisha mambo. 

Kunguru na bundi ni mfano wa watu wanaokula mizoga ya wengine na kufurahia maumivu ya wenzao.

Njiwa na kuku ni mfano wa maisha ya amani, usafi. Bata na goose ni mfano wa maisha ya heshima na mshikamano.

*Damu*

Wayahudi hawali damu kwa sababu ni uhai. Damu ni mali ya Mungu pekee. 

Kula damu kwa wayahudi ni ukatili na kuhujumu nafasi ya Mungu. Binadamu chake ni nyama.

Nyama ni mwili uliokufa, damu ni kiini cha roho na nguvu ya maisha.

Nyama ni riziki ya binadamu, damu ni riziki ya Mungu ukiigusa utamtambua.

Kumbe ni hatari kula damu. Kula damu ni kumtafuta Mungu.

Lakini hata hiyo nyama unayokula kuna taratibu zake za uchinjaji.Lazima utumie kisu kikali sana na kisichokuwa na pengo.

Mchinjaji hukata koo la mnyama kwa haraka, ili mnyama afe kwa haraka bila mateso. Marufuku kuchinja mnyama mwenye hofu na uoga.

Baada ya hapo, damu yote hutiririka kwa heshima ya Mungu. Huachwa imwagike kwenye ardhi kama ishara ya kurudisha uhai kwa Muumba, kwa sababu ardhi ndiyo chombo cha uumbaji na marejeo ya viumbe wote. 

*Damu na Maziwa*

Wayahudi pia walikatazwa kuchanganya nyama na maziwa katika mlo mmoja kwa sababu maziwa ni uzima na malezi, wakati nyama ni kifo. Huwezi kupata nyama bila kuua!

Kiroho, maziwa ni ishara ya uzima, malezi na upendo wa mama kwa mtoto. Ni chakula cha kwanza cha mtoto, kikiwa alama ya uhai unaoendelea na kulea. 

Nyama, kwa upande mwingine, ni ishara ya kifo kwa sababu inatokana na mnyama aliyechinjwa. 

Kwa hiyo, kuchanganya vyote viwili kungeonekana kama kuchanganya uzima na kifo katika sahani moja, jambo lililohesabiwa kama kumdhalilisha Mungu.

Hata mafuta ya ndani ya mnyama ni haramu kwa wayahudi. Haya ni mafuta yanayopatikana kwenye viungo kama figo, utumbo, ini nk.

Kwa wayahudi mafuta haya ni ya Mungu pekee na yanapaswa kuteketezwa kwenye madhabahu, si kuliwa na binadamu. Kula mafuta haya ni kuingilia ibada ya Mungu.

*OFA; Vitabu 14 kwa Sh 15,000. Mpesa 0740590451*

1. *Kula Chakula Kama Dawa, Epuka Kula Dawa Kama Chakula*  
2. *Malezi: Muandae Mwanao Kuwa na Hadhi Ukubwani*  
3. *Biashara Huanzia Kichwani Si Mfukoni*  
4. *Wasomi Huru Gerezani*  
5. *Maisha ni Kutafuta Si Kutafutana*  
6. *Ukombozi wa Fikra za Mwafrika*  
7. *Fungua Ubongo*  
8. *Miamba ya Afrika*  
9. *Viongozi Walioandika Majina Yao Vibaya*  
10. *Mbinu 16 Alizotumia Yesu Kutoboa*  
11. *Viongozi Wanaoishi Baada ya Kufa*  
12. *Fahamu ya Ndoa Kabla ya Ndoa!*  
13. *Ukombozi wa Fikra*  
14. *Fikra Tunduizi: Tungo za Kufikirisha* 

*Cheers*
*Mwl. Denis Mpagaze*
*Muhenga wa Karne ya 21!*



 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

Wasifu wa Kizza Besigye

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

KATI YA WATOTO 7 WA HAYATI MAGUFULI ANAYEJULIKANA ZAIDI NI JESCA

KIKOSI KILICHOITWA TAIFA STARS HIKI HAPA

KWA KHERI MAKARANGA UMEUTIMIZA MWENDO...

UBORA UNAONEKANA: BENKI YA NMB YANG'ARA TUZO ZA EUROMONEY 2026

WANAJESHI WAGOMA KWENDA IRAN KUPIGA

MCHIMBAJI MDOGO WA DHAHABU AFANYA MAKUBWA KWENYE HUDUMA ZA AFYA