Tunawaletea Orodha ya viongozi waliowahi kushika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
1. Ndg. Dunstan A. Omari (1962 - 1964)
2. Ndg. Joseph A. Namata (1964 - 1967)
3.Ndg. Dickson A. Nkembo (1967 - 1974)
4. Ndg. Tomothy Apiyo (1974- 1986)
Ndugu Timoth Apiyo alitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia miaka ya 1960. Mara baada ya kuhitimu shahada yake katika masuala ya kilimo alifanya kazi katika Kituo cha Kilimo cha Ukiliguru. Mnamo mwaka 1960 alihamishiwa Wilayani Muheza mkoani Tanga kuwa Afisa Mifugo wa Wilaya na baadae alipata uhamisho kwenda mkoani Morogoro na kuwa Afisa Kilimo Mkuu katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo, Ilonga. Kati ya mwaka 1964 -1965 Ndugu Apiyo alifanya kazi katika Wizara ya Kilimo na baadaye alihamishiwa mkoa wa Shinyanga kuwa Afisa Mifugo. Kazi nyingine; Katika uhai wake amewahi kuwa Mkurugenzi wa Mipango katika Wizara ya Kilimo (1968) Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Vijijini (1969) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Mwaka 1974 aliteuliwa na Rais Julius K. Nyerere kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
5. Balozi Paul M. Rupia (1995 - 1986)
6. Balozi Marten Y.C. Lumbanga (1995 - 2006)
Balozi Lumbanga alitunukiwa Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam machi 1972. Alipata Shahada yake ya Uzamili katika masuala ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo cha Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa cha Geneva (Geneva School of Diplomacy and International Relations).
Historia Kwa Ufupi
Balozi Dkt. Martin Y.C. Lumbanga aliapishwa kuwa Katibu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma mwaka 1996. Aliwahi pia kuitumikia Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika nyadhifa mbalimbali. Kuanzia mwaka 1986 alipoteuliwa kushika nyadhifa za Ukatibu Mkuu katika Wizara mbalimbali mpaka alipoteuliwa kushika wadhifa huo wa juu katika utumishi wa umma na Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka kumi namoja kuanzia Februari 1995 hadi Januari 2006. Katika kipindi hiki alihusika na mabadiliko mbalimbali katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ndani ya utumishi wa umma. Kuanzia mwezi February 2006, Balozi Lumbanga aliteuliwa kuwa Balozi na Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Kudumu za Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa Geneva, Uswizi. Na pia aliwakilisha katika ofisi za Umoja huo za Vienna, Austria. Toka aliporudi nyumbani Tanzania, Balozi Lumbanga aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (Public Procurement Regulatory Authority (PPPA) ) na Mhe. Jakaya M. Kikwete, Rais wa Awamu ya nne.
7. Ndg. Philemon L Luhanjo (2006 - 2011)
Mwaka 1977, Bw. Luhanjo alitunukiwa Diploma ya Utawala kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo Mzumbe (sasa Chuo Kikuu cha Mzumbe).
Alipata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Utawala wa Umma na kubobea katika masuala ya Uchambuzi wa Sera za umma kutoka Chuo Kikuu cha Southern California mjini Los Angeles, California, Marekani (1981 - 1982).
Historia Kwa Ufupi
Ndugu Phillip L. Luhanjo, ameitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1975 katika nyadhifa mbalimbali. Kati ya Aprili 1975 hadi Juni 1976, Ndugu Luhanjo alikuwa Afisa Tawala katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini. Kati ya Aprili 1977 hadi Juni 1983, Ndugu Luhanjo alikuwa Afisa Mipango, Uratibu wa Nguvu Kazi katika mikoa 20 ya Tanzania Bara, katika Idara ya Tawala za Mikoa. Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mipango ya Nguvu Kazi na Mafunzo (Julai - Disemba 1983). Aliteuliwa kuwa Katibu Masaidizi wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu kwa Baraza la Mawaziri katika Ofisi ya Rais, Ikulu, kuanzia Januari, 1984 hadi Machi 1986. Kati ya Aprili 1986 hadi Disemba 2005, alifanya kazi kama Karani wa Baraza la Mawaziri katika Ofisi ya Rais, Ikulu.
8. Balozi Ombeni Yohana Sefue (2012- 2016)
Balozi Sefue amesomea masuala ya Utawala wa Umma katika Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo - Mzumbe (sasa Chuo Kikuu Mzumbe) na kutunukiwa Stashahada ya Daraja la Juu katika Masuala ya Utawala wa Umma mwaka 1977.
Mwaka 1981 alipata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Sera na Utawala kutoka Institute of Social Studies (ISS), (sasa inajulukana kama The International Institute of Social Studies of Erasmus University), mjini The Hague, Uholanzi
Mwaka 1986 alipata mafunzo katika ngazi ya cheti katika masuala ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia kutoka Kituo cha Mafunzo ya Diplomasia cha Tanzania na Msumbiji (Sasa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam)
Pia amepata mafunzo ya Upatanishi wa Kimataifa kutoka International Peace Academy, na mafunzo kuhusiana na changamoto za kuchumi na kijamii katika nchi zinazoendela kutoka International Relations and Socialist Integration with the Presidium of the Bulgarian Academy of Sciences (1984).
Balozi Ombeni Yohana Sefue aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 31 Disemba, 2011. Kama Katibu Mkuu Kiongozi, yeye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma.
Nafasi za Kiutendaji
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mjini New York tangu Agosti 31, 2010.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Mwakilishi Nchini Mexico, Juni 2007 hadi Agosti, 2010
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Canada na Mwakilishi Nchini Cuba, Oktoba 2005 hadi Juni, 2007
Balozi Sefue alikuwa Mwanadiplomasia na Mshauri katika Ubalozi wa Tanzania mjini Stockholm, Sweden 1987 hadi 1992
Kati ya mwaka 1993 na 2005, alifanya kazi ya uandishi wa hotuba na Msaidizi kwa Marais wawili wa Tanzania, Rais Ali Hassan Mwinyi (1993-1995) na Rais Benjamin W. Mkapa (1995-2005).
9. Balozi Mh. John William Herbert Kijazi (2016 - 2021)
Balozi Mhandisi Kijazi ana Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Kiraia (Bachelor of Science in Civil Engineering) yenye Heshima (Honours) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Pia, ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhandisi wa Barabara Kuu (Master of Science in Highway Engineering) kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza.
Historia Fupi
Balozi Mha. John W.H. Kijazi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi (Chief Secretary) wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 6 Machi 2016. Akiwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. Kijazi pia alihudumu kama Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (Kabineti), na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa.
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mha. Kijazi alikuwa Balozi wa Tanzania (High Commissioner) nchini India (kuanzia Juni 2007) na Singapore (kuanzia Mei 2013).
Kabla ya kuanza majukumu yake ya kidiplomasia, Balozi Mha. Kijazi alipangiwa kazi kwa muda mfupi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo alishika Majukumu Maalum.
Kazi ya Balozi Mha. Kijazi katika utumishi wa umma nchini Tanzania ilianza mwaka 1982, ambapo alishika nafasi zifuatazo katika Wizara ya Miundombinu/Ujenzi (Ministry of Public Works)
1. Mhandisi Mtendaji Msaidizi (Assistant Executive Engineer): 1982 hadi 1986.
2. Mhandisi wa Mkoa (Regional Engineer): 1986 hadi 1996.
3. Mhandisi Mwandamizi wa Matengenezo ya Barabara (Senior Road Maintenance Engineer): 1996 hadi 1999.
4. Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa (Director of Regional Roads): 1999 hadi 2002.
Kufuatia utumishi wake uliotukuka, Balozi Mha. Kijazi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Ujenzi (2002 hadi 2005) na baadaye katika Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu (Januari hadi Novemba 2006).
10. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (2021 - 2021)
Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma (BA in Political Science and Public Administration); Shahada ya Uzamili (MA); na Shahada ya Uzamivu (PhD), zote kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD). Balozi Dkt. Bashiru alianza Utumishi wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro kama Mhadhiri Msaidizi kuanzia Septemba, 2003 hadi Septemba, 2004. Aidha, Balozi Bashiru ametumia taaluma yake kama Mhadhiri (Lecturer) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya CKD kuanzia Oktoba, 2004 hadi Mei, 2018. Vilevile, amekuwa Kiongozi wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti kati ya mwaka 2014 na mwaka 2016. Balozi Dkt. Bashiru pia alikuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utandawazi, Mikutano/Mihadhara na Uendelezaji (Director of Internationalisation, Convocation and Advancement) katika CKD. Balozi Bashiru ni mwanafunzi wa falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) kuhusu harakati za ukombozi, sera za kutofungamana na upande wowote, Umoja wa Afrika, ujamaa na kujitegemea.
Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuanzia Juni, 2018 hadi Februari, 2021. Uteuzi huo ulitokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa Kiongozi wa Timu iliyofuatilia na kurejesha mali za CCM mwaka 2017/2018.
Tarehe 26 Februari, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alimteua Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi. Katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Balozi Bashiru ni Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (BLM), Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa (BUT).
11. Mhe. Balozi Hussein A. Kattanga. ( 2021 -2023)
Balozi Hussein A. Kattanga ni Mchumi wa Fedha kwa taaluma. Ana Stashahada ya Juu ya Fedha kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam, Tanzania na Shahada ya Uzamili ya Sayansi (MSc.) ya Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Glasgow - Uingereza.
Balozi Hussein A. Kattanga aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 31 Machi 2021, na kuapishwa tarehe 1 Aprili 2021. Katika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi H. A. Kattanga ni Katibu Mkuu wa Rais, Katibu wa Baraza la Mawaziri (BW), na Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa (BUT).
Kabla ya uteuzi wake, Balozi H. A. Kattanga alikuwa Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japani, na pia alikuwa akisimamia shughuli za kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zile za Australia, Papua New Guinea na New Zealand tangu 2020.
Kabla ya kuwa na majukumu ya kidiplomasia, Balozi H. A. Kattanga alikuwa Msimamizi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kutoka Agosti, 2012 hadi Oktoba, 2019.
Balozi Hussein A. Kattanga ana uzoefu wa miaka 27 ya utumishi Serikalini, na kwa zaidi ya miaka 20 amefanya kazi katika nyadhifa za juu Serikalini.
Kuanzia mwaka 1986 hadi 2005 alifanya kazi katika Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Mbinga katika ngazi tofauti; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya-Wilaya ya Mbinga (1996-2005); Mkurugenzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni - Dar es Salaam (2006-2007); Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) katika mikoa ya Singida na Morogoro (2008-2009); Naibu na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (2010-2011) na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) kuanzia Machi 2011 hadi Agosti, 2012.
12. Balozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka ( 2023 - Sasa).

Comments