PINDA AONGOZA UPANDAJI WA MITI 7,000 DODOMA, KAMPENI YA “URBAN FOREST” YAANZA

 WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda,  ameongoza shughuli ya  upandaji wa takribani miti 7,000 katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuelekea utekelezaji wa mradi wa kuanzisha Msitu wa Mjini (Urban Forest) utakaohusisha upandaji wa miti 20,000 katika Jiji la Dodoma.

Shughuli hiyo imeandaliwa na Habari Conservation Organisation (HCO) kwa ufadhili wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP) na ni sehemu ya kampeni ya "Kijanisha Dodoma" iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Makamu wa Rais.

Akizungumza baada ya kushiriki upandaji wa miti hiyo, Pinda amesema uanzishwaji wa misitu ya mijini ni hatua muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza ongezeko la joto, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuboresha mazingira ya makazi.

Amesema ukuaji wa miji unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika maeneo ya kijani ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.

"Hatupaswi kupanda miti tu, bali tuihudumie mpaka ikue. Kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesisitiza Pinda.

Afisa Uhusiano wa HCO, Royce Joseph, amesema lengo la mradi huo ni kupanda miti 20,000 ya aina mbalimbali na kuanzisha msitu wa mijini utakaosaidia kufyonza hewa ukaa, kuboresha mfumo wa ikolojia, kuimarisha biashara ya kaboni na kuongeza maeneo ya kijani katika makao makuu ya nchi.

Amesema miti 7,000 iliyopandwa ni hatua muhimu kuelekea kufikiwa kwa lengo hilo, huku akiwataka wananchi, taasisi na kampuni kushiriki kwa kupanda miti wakati wa maadhimisho ya matukio mbalimbali ya maisha na shughuli zao.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa EG White Secondary School iliyoshiriki katika upandaji miti, Renata Kimata, amesema shule hiyo tayari imepanda miti zaidi ya 1,000, hatua ambayo imeboresha mazingira ya kujifunzia na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kuhifadhi mazingira.

Naye mdau wa mazingira, Mhandisi Athuman Futakamba, ameipongeza EACOP kwa kufadhili mradi huo na kutoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuunga mkono juhudi za kuongeza maeneo ya kijani nchini.

Mradi huo umewashirikisha taasisi za serikali, sekta binafsi, viongozi wa dini, wanafunzi na wananchi, huku HCO ikieleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza kampeni za upandaji miti, uhifadhi wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kampeni ya "Kijanisha Dodoma" inalenga kuifanya Dodoma kuwa jiji la kisasa lenye mazingira bora kupitia ongezeko la maeneo ya kijani, sambamba na kuhamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira.

Waziri Mkuu Mstaafu Pinda akimwangalia mwanafunzi wa EG White, Renata Kimata, akimwagilia mti alioupanda. 
Pinda akipanda mti.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza wakati wa upandaji miti.
Mwanafunzi wa EG White Secondary School iliyoshiriki katika upandaji miti, Renata Kimata, amesema shule hiyo tayari imepanda miti zaidi ya 1,000.
Afisa Uhusiano wa HCO, Royce Joseph, akisoma taarifa ya mradi huo.

Mdau wa mazingira, Mhandisi Athuman Futakamba akipanda mti.
Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Nickson Mwesigwa akipanda mti.
Mwanafunzi akielekezwa jinsi ya kupanda mti.
Pinda akikagua eneo la mradi huo.





Pinda akipiga picha za kumbukumbu na walioshiriki kupanda miti katika mradi huo.




IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DK MAGUFULI ATANGAZA KIAMA CHA MAJAMBAZI, WEZI NA MAFISADI KATIKA MIKUTANO YA KAMPENI SUMBAWANGA,TUNDUMA, ILEJE NA MBOZI

MAAFISA JENERALI WASTAAFU 17 WA JWTZ WAAGWA.

PICHA YA RAIS ILIYOBAMBA WIKI HII

JUA AINA NNE ZA KABILA LA WASUKUMA

18 WAPITISHWA KUGOMBEA UONGOZI YANGA

IJUE HISTORIA YA PACOME ZOUZOUA