Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Mkoani Morogoro Mheshimiwa Dkt. Mecktridis Mdaku, mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mazingira na Maji, ameungana na Kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miradi ya kimkakati ya majisafi inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hii muhimu kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Wajumbe wa Kamati walitembelea mtambo wa uzalishaji maji wa Ruvu Juu, pamoja na miradi mbalimbali ya kimkakati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji ikiwemo mradi wa maji Msumi na mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo).
Dkt. Mecktridis alisema miradi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha huduma za maji na kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama kwa uhakika. Alisisitiza pia kuwa usimamizi wa karibu wa miradi hiyo ni muhimu ili ikamilike kwa wakati na kutoa matokeo yaliyokusudiwa.
Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) imeipongeza DAWASA kwa kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, ikieleza kuwa uwekezaji unaofanyika utaongeza uzalishaji wa maji, kuboresha miundombinu na kuimarisha huduma katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayolizunguka.
Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la Bunge la kusimamia utekelezaji wa miradi ya majisafi inayotekelezwa na Mamlaka na yenye kutoa huduma kwa wananchi, kwa lengo la kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi wote.
Comments