JAB YAWANOA WAANDISHI WA WASAFI MEDIA KUHUSU SHERIA NA MAADILI


Washiriki wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kutoka Wasafi Media wameeleza kuwa mada zilizotolewa katika mafunzo hayo zimewasaidia kutambua makosa yaliyokuwa yakijirudia katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwapatia mwongozo wa kuboresha utendaji.

Wakizungumza wakati wa tathmini ya mafunzo hayo yaliyofanyika Septemba 17 na 18, 2026, katika Ofisi za Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) jijini Dar es Salaam, Gerald Hando, Aggai Kifumu na David Rwenyagira wameeleza kuwa mafunzo yamewaongezea uelewa kuhusu sheria, maadili na uzalendo katika uandishi wa habari.




Wamebainisha kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili Waandishi wa Habari na wazalishaji wa maudhui ni shinikizo la kuongeza idadi ya wafuasi katika majukwaa ya kidijitali, kukidhi matakwa ya hadhira pana na kasi ya mabadiliko katika mazingira ya kidijitali kuwa kubwa kuliko maboresho ya baadhi ya sheria zinazoongoza shughuli zao.

Kwa mujibu wa washiriki hao, mazingira hayo yanaweza kusababisha baadhi ya Waandishi wa Habari kufanya kazi kwa mazoea au kujikuta wakifanya makosa ya kisheria na kimaadili bila kuwa na uelewa wa kutosha.



Wamesema mafunzo hayo yamewajenga kitaaluma, yamewafungua kutoka katika utendaji wa mazoea na kuwapatia mwongozo wa kufanya maamuzi sahihi katika majukumu yao ya kila siku.

Aidha, wameiomba JAB kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo vingine, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanaofanya kazi na kuzalisha maudhui kupitia majukwaa ya kidijitali, ambako changamoto za uzingatiaji wa sheria na maadili zimeendelea kujitokeza.



Wamesema kasi ya uzalishaji na usambazaji wa maudhui katika majukwaa hayo imeongeza uwezekano wa kutokea kwa makosa ya kisheria na kimaadili, hivyo elimu endelevu inahitajika ili kuimarisha weledi na uwajibikaji.

Mafunzo hayo yalihusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari na uzalendo, yakilenga kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari na watangazaji wa Wasafi Media kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, viwango vya taaluma na maslahi ya jamii.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

𝐌𝐉𝐔𝐄 𝐊𝐀𝐂𝐇𝐄𝐑𝐎 𝐌𝐙𝐄𝐍𝐀

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA