KIKWETE AHIMIZA TANZANIA NA JAPAN KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA USALAMA WA CHAKULA NA UCHUMI WA BULUU

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Sasakawa Peace Foundation ya Japan, Bw. Masanori Kobayashi, katika ofisi yake ndogo iliyopo Masaki, Dar es Salaam.


Mazungumzo hayo yalilenga kufuatilia utekelezaji wa masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara ya kikazi iliyofanywa huko nyuma na Dkt. Kikwete nchini Japan tarehe 23 hadi 24 Julai 2025.


Katika ziara hiyo, Dkt. Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri sita kutoka Afrika walioalikwa na Serikali ya Japan kupitia taasisi za Sasakawa Peace Foundation na Nippon Foundation. Viongozi hao walishiriki katika kutoa ushauri kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Japan chini ya mwavuli wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD).


Mkutano wa tisa wa TICAD ulifanyika baadaye jijini Yokohama, Japan, kuanzia tarehe 20 hadi 22 Agosti 2025.


Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kikwete aliishukuru Serikali ya Japan, kupitia Sasakawa Peace Foundation, kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Japan, hususan katika kuimarisha mifumo ya uzalishaji na usalama wa chakula pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu.


Dkt. Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza tafiti na kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija katika shughuli za wavuvi wadogo na ufugaji wa samaki.


Aidha, alihimiza juhudi zaidi zielekezwe katika kukuza kilimo cha mwani kwenye maeneo ya mwambao wa Tanzania, hususan Zanzibar, ili kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na mapato ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo.


Kwa upande wake, Bw. Kobayashi alieleza utayari wa Sasakawa Peace Foundation kutumia nafasi na ushawishi wake kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.





 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

𝐌𝐉𝐔𝐄 𝐊𝐀𝐂𝐇𝐄𝐑𝐎 𝐌𝐙𝐄𝐍𝐀

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA