Kocha wa Gaborone United, Sean Connor, amefanya uchambuzi wa kina wa Yanga SC kabla ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, akisema mabingwa hao wa Tanzania si timu rahisi kukabiliana nayo wanapocheza nyumbani.
Connor amefichua kwamba baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza wa mtoano, amekuwa akitazama mikanda ya mechi mbalimbali za Yanga walizocheza nyumbani, ikiwemo michezo ya msimu uliopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini amesema amegundua namna Yanga wanavyoweka presha kubwa kwa wapinzani wao mbele ya mashabiki wao, hivyo amewaonya wachezaji wake kujiandaa kwa mchezo mgumu.
«“Si rahisi kukabiliana na Yanga ikiwa nyumbani. Wana rekodi kubwa na wanacheza kwa njaa kubwa ya ushindi. Haitakuwa mechi rahisi,” alisema Connor.»
Connor pia amesema amefuatilia hata mechi zilizochezwa katika uwanja ambao utatumika kwenye mchezo huo na amewaambia wachezaji wake kuwa wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na presha kutoka uwanjani na kwa mashabiki wa Yanga.
Yanga na Gaborone United zitatoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza, hivyo ushindi katika mchezo wa marudiano utampeleka mshindi hatua inayofuata.
Kwa Gaborone United, sare ya 2-2 au zaidi pia inaweza kuwapa nafasi ya kusonga mbele kutokana na mabao ya ugenini.
Je, Yanga itatumia nguvu ya nyumbani kuwavusha kwenda hatua inayofuata?
#YangaSC #CAFChampionsLeague #GaboroneUnited #GoalSportsTanzania
Comments