NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imepanga kuanza kukamata maiti zitakazohusishwa kusafirisha dawa za kulevya nchini.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa mamlaka hiyo wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu ya oparesheni iliyofanyika nchini kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.
Katika Oparesheni tuliyoifanya katika mikoa 14 tumebaini uwepo wa maiti zinazosafirshwa hasa kwenda Kanda ya Kaskazini kuhusika kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi.
"Sasa tunatangaza rasmi tutazikamata maiti zote zitakazohusika na usafirishwaji wa dawa hizo pamoja na magari na watu watakaobainika na jambo hilo tutawakamata na kutahifisha magari hayo," amesema.
Pia ameongeza kwamba katika Oparesheni hiyo iliyofanyika kwa kipindi hicho cha miezi mitatu wamefanikiwa kukamata kilogramu 18,078.41 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro,Arusha, Mororgoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Aidha ameweka bayaba kwamba mikoa ya Morogoro na Tabora imekuwa kinara katika Kilimo cha zao la bangi na hatua mbalimbali za zinaendelea ili kudhibiti zao hilo kwenye mikoa hiyo.
Lymo ameongeza kuwa katika Oparesheni hiyo hiyo wamebaini pikipiki kutumika zaidi katika kusafirisha bangi na wamekamata pikipiki 40, Bajaji moja, magari nane yaliyohusishwa na kusafirisha dawa hizo.
Amesema magari hayo ni pamoja na Toyota Harrier yenye namba T. 878 ASJ, Toyota Land Cruiser namba T. 234 BUR, Toyota IST namba T215 DCJ Toyota Noah namba T. 231 AWP, Toyota Alphard namba T. 870 EDE na Toyota Discovery.
Gari lingine lililokamatwa ni basi la Kampuni ya Ratco lenye namba T. 443 likisafirisha bunda 238 zenye uzito wa kilogramu 125.33 likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam.
Pia amesema katika kipindi hicho wamewakamata raia wa kigenj sita akiwemo raia wawili wa Afrika Kusini wakiwa na gramu 65.8 za bangi, raia wa Kenya mmoja akiwa na gramu 3.89 za mirungi, raia wa Nigeria mmoja akiwa na gramu 4.6 za bangi, na raia wa Uturuki mmoja akiwa na gramu 1.87 za skanka.

Comments