SERIKALI YAFIKISHA UMEME KATIKA MAENEO 582 YA WACHIMBAJI WADOGO, KILIMO NA VIWANDA TANZANIA BARA


NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme katika maeneo 582 ya wachimbaji wadogo, kilimo na viwanda Tanzania Bara, kwa gharama ya Shilingi bilioni 115.


Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mwanahamisi Athumani, Mbunge wa Viti Maalumu, aliyetaka kujua ni lini Serikali itatekeleza Mpango Mkakati Maalumu wa kuhakikisha maeneo ya wachimbaji wadogo yanafikishiwa umeme wa kutosha kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.


Akijibu swali hilo,  Makamba amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili, 2023 na kwa sasa umefikia hatua za mwisho za utekelezaji.


Aidha, amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuainisha maeneo ya kipaumbele yatakayofikishiwa huduma ya umeme katika hatua zinazofuata, kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.


Pia Makamba amesema Serikali kupitia TANESCO, kwa kutumia fedha za ndani, inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kupoza umeme katika mikoa mbalimbali nchini, hususan maeneo yenye changamoto ya low voltage.


Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji yanafikiwa na huduma ya umeme ya kutosha na ya uhakika.


Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo, wakulima, viwanda na maeneo mengine ya uzalishaji yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote, ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA