VETA YATEGUA KITENDAWILI CHA AJIRA

Na Richard Mwaikenda, Dodoma

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema tatizo la ajira nchini haliwezi kutatuliwa kwa kutegemea ajira rasmi pekee, bali kwa kuwajengea Watanzania ujuzi unaoendana na mahitaji ya uchumi unaokua kwa kasi.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema fursa za kazi zipo katika sekta mbalimbali, lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa watu wenye ujuzi unaohitajika katika maeneo hayo.

Kasore aliyasema hayo jana, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO kuhusu utekelezaji wa majukumu ya VETA kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27.

Amesema Tanzania inapopiga hatua katika uwekezaji, ujenzi, viwanda, madini, utalii, kilimo, nishati, usafirishaji na teknolojia, mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa vitendo yanaendelea kuongezeka.

“Tunapowaambia wananchi wajifunze ufundi stadi, tunawaambia wajifunze kwa sababu uchumi unaendelea kuwahitaji. Fursa zipo, kinachohitajika ni ujuzi,” amesema Kasore.

Amesema kila hatua ya maendeleo ya uchumi inahitaji wataalamu wa ufundi stadi, akitolea mfano sekta ya ujenzi ambayo inahitaji mafundi wa uashi, useremala, mabomba, umeme, uungaji na uundaji wa vyuma pamoja na mifumo ya viyoyozi.

Kwa upande wa viwanda, amesema mahitaji yapo kwa mafundi wa mitambo, umeme, welding, fabrication, instrumentation, automation na maintenance, huku sekta ya madini ikihitaji wataalamu wa mitambo mikubwa, umeme, welding, fitting and machining pamoja na waendeshaji wa mitambo maalumu.

Aidha, amesema sekta ya hoteli na utalii nayo inaendelea kutoa nafasi kwa wenye ujuzi katika upishi, bakery, housekeeping, food and beverage service na maeneo mengine ya huduma za ukarimu.

Kwa mujibu wa Kasore, kilimo kinachoelekea katika matumizi makubwa ya teknolojia nacho kinahitaji wataalamu wa mitambo ya kilimo, umwagiliaji, refrigeration, mifumo ya umeme na teknolojia nyingine zinazohusiana na uzalishaji wa kisasa.

Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa mjadala wa ajira unapaswa kuangalia zaidi uhusiano kati ya ujuzi wa mtu na mahitaji halisi ya soko la ajira, badala ya kuangalia ajira rasmi pekee.

“Tunapaswa kujiuliza, je, kweli hakuna kazi au kuna kazi ambazo hatuna watu wenye ujuzi unaohitajika kuzifanya?” amesema.

Amesema VETA imebeba jukumu la kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wanapata ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kuongeza tija, kuajiriwa na kujiajiri.

Pia amesema ujuzi wa ufundi stadi unaweza kumwezesha kijana kuunda ajira kwa wengine, badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini au sekta binafsi.

Amesisitiza kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, kwa kuwa taifa linalolenga uchumi imara linahitaji nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia.

Kwa mantiki hiyo, VETA imewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kubadili mtazamo kuhusu elimu ya ufundi stadi na kuitazama kama nyenzo muhimu ya kujenga maisha, kuongeza kipato na kushiriki katika fursa zinazozalishwa na ukuaji wa uchumi.

.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

NI MAKOSA WANAFUNZI KUFIKA SHULE SAA 1:15 ASUBUHI

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA