Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Thobias Nyingo, amewataka vijana waliomaliza Mafunzo ya Awali ya Kijeshi kutumia ipasavyo elimu na mafunzo waliyoyapata ili kujenga maisha yenye mwelekeo mzuri, akiwakumbusha kuwa matumizi mabaya ya mitandao yanaweza kuwa na madhara katika maisha yao ya baadaye.
.
“Chochote ambacho mmekifanya au mtakachokifanya kuanzia leo, fahamuni kwamba kitakuwa kwenye rekodi yenu ya maisha na kamwe hakiwezi kufutika,” alisema Nyingo.
.
Mhe. Nyingo ameyasema hayo leo, Septemba 14, 2026, wakati akihitimisha Mafunzo ya Awali ya Kijeshi kwa Vijana wa Kujitolea OP Nishati Safi pamoja na Mujibu wa Sheria OP Linda Amani, yaliyofanyika katika Kikosi cha Makutupora JKT,mkoani Dodoma.
.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Shija Lupi, amewataka vijana hao kuishi kwa kuzingatia kiapo walichokiapa, kuepuka kurubuniwa na kuwaelimisha pamoja na kuwashauri wenzao ambao hawana taarifa sahihi.
.
Amesema vijana hao wanapaswa kutumia maarifa waliyoyapata kuwaelimisha wengine na kuhakikisha wanayafikisha kwa jamii kwa manufaa ya Taifa.
.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Makutupora JKT, Kanali Festo Mbanga, amewataka vijana hao kuyafanya mafunzo waliyoyapata kuwa msingi wa maisha yao ya baadaye, huku akiwataka watakaokwenda vyuoni kuzingatia taratibu na maelekezo ya taasisi zao.
Comments