MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Mwakibete, amewataka wakulima na wadau wa kilimo wilayani humo kuchangamkia fursa zinazotokana na zao la parachichi, akisema lina nafasi kubwa ya kuongeza tija na kipato kwa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini.
Mwakibete ametoa kauli hiyo baada ya kushiriki Mkutano wa Tatu wa Wadau wa Zao la Parachichi uliofanyika jijini Dodoma, uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mustakabali, mafanikio na mipango ya kimkakati ya kuendeleza kilimo cha zao hilo nchini.
Amesema kupitia mkutano huo alipata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo na wadau kutoka Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya, akiwemo uongozi wa Kampuni ya Itecado Farm pamoja na Umoja wa Wakulima wa Parachichi Busokelo (UWAPABU).
Amesema majadiliano hayo yalilenga namna ya kuongeza tija, uzalishaji na ushirikiano miongoni mwa wadau katika kuendeleza kilimo cha parachichi.
Aidha, Mwakibete ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa mipango yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwemo kugawa miche bora ya parachichi, kukamilisha ujenzi wa vituo vya kukusanyia mazao na kuwawezesha vijana kupitia mpango wa BBT Ugani ili kuwafikia wakulima katika maeneo ya vijijini.
Amesema fursa hizo ni muhimu kwa wakulima wa Kilolo, hivyo amewataka wananchi na wadau wa kilimo wilayani humo kuzitumia kikamilifu kwa kuanzisha na kuendeleza kilimo cha parachichi kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kipato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Comments