*AWESO ATOA MAAGIZO YA KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI ARUMERU, ZAIDI YA KATA 20 KUNUFAIKA*

 


WAZIRI wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ametoa maelekezo mbalimbali ya kuharakisha utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Arumeru, huku zaidi ya kata 20 zikitarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama.


Maelekezo hayo yametolewa Novemba 25, 2026, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maji katika wilaya hiyo, iliyofanyika katika utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa Novemba 19, 2026, kuhusu kuhakikisha wananchi wa Arumeru wanapata huduma ya maji.


Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, alimfikisha Waziri wa Maji katika kata saba, zikiwemo tatu za Meru DC na nne za Arusha DC, ili kujionea hali halisi ya changamoto za upatikanaji wa maji pamoja na maendeleo ya miradi inayotekelezwa.


Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Aweso ni kuelekeza Shilingi bilioni 1.034 kwa ajili ya kukamilisha miradi minne ya maji ya Leguruki yenye thamani ya Shilingi milioni 500, Maji ya Chai milioni 194, Kikwe milioni 190 na Mlangarini milioni 150.


Kuhusu miradi ya Oldonyosambu na Oldonyowas yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni sita, Waziri amesema utengenezaji wa mabomba unaanza na Wizara itahakikisha fedha za kukamilisha mradi huo zinapatikana ili kuwaondolea wananchi adha ya kutumia maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya floridi. Aidha, amesema ana mpango wa kumwomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhudhuria uzinduzi wa mradi huo utakapokamilika.


Katika mradi wa Imbaseni unaotekelezwa na RUWASA, Waziri Aweso amesisitiza kuwa mkandarasi hataongezewa muda mwingine na ameelekeza mradi huo ukabidhiwe ifikapo Machi 2027.


Aidha, katika maeneo ya Bangata na Midawe, amesema maji yameanza kutoka katika hatua ya awali na wananchi wataanza kunufaika na huduma hiyo.


Akizungumzia miradi ya Musa na Likamba, Waziri ameelekeza Mkuu wa Wilaya kuitisha kikao kazi kitakachowakutanisha wadau na wataalamu kwa ajili ya kuweka mkakati wa kutatua changamoto za uendeshaji wa miradi hiyo.


Katika hatua nyingine, ameielekeza AUWSA kupanua wigo wa huduma za maji katika maeneo ya Arumeru, hususan kata zinazopakana na Jiji la Arusha, ili wananchi wa maeneo hayo nao wanufaike na huduma hiyo.


Vilevile, amesisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye vyanzo vya maji wanapaswa kuhakikisha wananufaika na rasilimali hiyo kwa kupata huduma ya maji kabla ya kupeleka huduma hiyo katika maeneo mengine.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake yaliyolenga kutatua changamoto ya maji katika wilaya hiyo, akieleza kuwa ziara hiyo imekuwa sehemu muhimu ya kuainisha changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua.


Lugangira amesema atashirikiana kwa karibu na RUWASA, AUWSA, madiwani na viongozi wengine kuhakikisha maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri yanatekelezwa ili wananchi wanufaike na miradi hiyo.


Amesema Waziri Aweso ameahidi kurejea Arumeru Januari 2027 kwa ajili ya kuzindua miradi itakayokuwa imekamilika na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mingine.


“Nimefarijika sana kuona nimechangia katika utatuzi wa mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wenzangu wa Arumeru. Nitaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa. Arumeru tunaendelea kusema ASANTE SANA MAMA, TUNAKUPENDA SANA MAMA!” amesema Lugangira.


Kupitia hatua hizo, zaidi ya kata 20 zinatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama, huku Serikali ikiendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa uhakika na endelevu.



#TukutaneSite #MaendeleoArumeru #ArumeruKimataifa

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

UJUE UKWELI KUHUSU JIJI LA MBEYA (GREEN CITY)

TIMU YA NGORONGORO KAMA DOUMBIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA